Habari za Punde

Kambare wa Uzaramoni

 


Na.Adeladius Makwega. Dodoma.

Nilikuwa najiuliza mbona kiwanja chetu kina umbo la sambusa? Nilipatiwa majibu kuwa katika eneo hilo sisi tulikuwa wakwanza kununua ardhi hiyo lakini kwa bahati mbaya hatukujaliwa kulijenga mapema, wakati majirani waliotuzunguka wanajenga kila upande. Ikiaminika kuwa walijaribu kumega sehemu ya kiwanja chetu ambacho wakati huo kilikuwa na umbo la mraba.

Eneo hilo lilikuwa si kiwanja bali lilikuwa ni sehemu ya shamba, maana haya mambo ya kupima viwanja ni mambo ya siku hizi. Ndiyo kusema na nasie tulipojaliwa kujenga makaazi yetu ndipo umbo hilo la sambusa la kiwanja chetu lilionekana.

Wakati ninakuwa mtu mzima, nilipouliza juu ya umbo hilo la sambusa la kiwanja chetu Babu aliniambia kuwa hapa kuna jirani ambaye ndiye aliyekuwa wa kwanza kujenga ndiye aliyetufanyia hilo na kwa hakika alisababisha eneo hilo likamegwa bila woga na kila aliyejaliwa kujenga ambaye alipakana na sisi.

“Binadamu walio wengi ni mabingwa na hodari wa kuiga uhuni kuliko kuiga wema.”

Babu yangu aliniambia.

Babu aliniambia kuwa aliamua kukaa kimya ili maisha yaende kwa kuwa jambo hilo lilifanywa na mtu ambaye anatoka naye mkoa mmoja wa asili. Kukaa huko kimya hakukuwa na maana kwa kuwa mzee huyu aliridhishwa na dhuluma hiyo, la hasha bali kila aliyezaliwa wa familia hiii alisimuliwa juu ya umbo la sambusa la kiwanja chetu na mzigo wa lawama hizo alibebeshwa jirani huyu. Akizaliwa mtoto, akizaliwa mjukuu na hata kitukuu kiliambiwa dhuluma hiyo.

Kwetu wana msemo kuwa dhuluma fanya kwa mgumba/tasa na wewe unayedhulumu kuwa na mgumba/tasa, vinginevyo unaweza kuleta balaa kwa vitukuu, watu wakataka kumalizana kwa kosa ulilofanya wewe babu/bibi. Watu wanatabia ya kudanganya kuwa hawakumbuki dhuluma, kumbe wanakumbuka vizuri, wanalolifanya ni kugubika kombe. Kumbuka tu kombe linalogubikwa lazima litagubuliwa tu, iko siku yake. Msemo huu unasemwa ili kusisitiza watu kutendeana mema na kuacha kufanyiana mabaya. Kumbuka pia nguvu ulizonazo wewe, hawezi kuwa nazo mwanao au mjukuu, mambo huwa yanazunguka leo nguvu kwa huyu na kesho kwa yule.

Tukiwa watoto, mimi na watoto wa jirani huyu tulikuwa tunacheza pamoja, shule tunaenda pamoja hakukuwa na baya lolote. Maisha yaliendelea kama kawaida. lakini yale yanayosemwa sirini yalikuwa mengi na yanatisha kabisa. Kwa bahati mbaya mzee huyu jirani alifariki na kumuacha mkewe na watoto kadhaa, naye babu yangu alifariki dunia pia.

Mimi nikiwa mdogo, nilikuwa na mazoea ya kucheza na watoto wa jirani huyu lakini nikiambiwa niwe makini, hawa si watu wazuri lakini urafiki na hawa jamaa ulidumu kwa miaka mingi sana. Huku tukishirikiana kwa hili na lile lakini kwa mashaka mashaka.

Maisha yaliendelea na miaka ilisogea taratibu, kuna wakati mke wa jirani huyu aliyefariki aliamua kurudi kwao huko Mwanadilatu Tambani ambapo ni vijiji vya Uzaramoni kwani mama huyu ndipo alipozaliwa, akirudi kuangalia mashamba yake ya urithi.

“Mwanangu mimi naondoka naenda Mwanadilatu, kule ni kwetu ndipo nilipozaliwa, hapa Mbagala maeneo yamejaa na watu ni wengi, siwezi kulima muhogo wala chochote naenda nyumbani kwetu kuishi, hapa pameshakuwa mji mambo ya mjini mjini siyawezi, nakuacha na ndugu zako hawa mkae vizuri, karibu kwetu upate hata shamba la kupanda mpunga” Mama huyu aliniaga na kwenda zake.

Kweli nilikaa na ndugu hawa vizuri sana na baada ya muda niliamua kwenda kumsalimia mama huyu huko Mwanadilatu, wakati huo usafiri ulikuwa mgumu sana tulipanda daladala hadi Rangitatu, alafu Rangitatu hadi Mbande Magengeni. Tuliposhuka hapo tulitembea kwa mguu hadi Mwanadilatu mwendo saa moja na nusu kwa mguu tukipita katika mashamba ya mpunga, viunga vya minazi na mikorosho.

Tulipofika hapo tulipokelewa vizuri, tulipikiwa wali mpya na kuku ambaye hakuungwa chochote, kilikuwa chakula kizuri sana, nilikula wali huo barabara na ndugu yangu niliyeambatana naye.

“Mwanangu nashukuru kwa kuja kunisalimu huku ndiyo kwetu Uzaramoni, Mbagala kulikuwa ni mbilini (sehemu alipoolewa mwanamke).”

Alisema mama huyu. Nilikabidhiwa mpunga katika kikapu wa kurudi nao Mbagala.

Kwa kuwa niliagiza kutafutia eneo la ekari mbili nililiona na nililipia kiasi fulani cha fedha na mimi kuwa mwanakijiji wa kijiji hicho cha Mwanadilatu.

Katika eneo langu hilo, kuna bwawa la samaki ambalo msimu wa mvua huwa linabahatika kuwa na Kambare wengi. Mama huyu hufika hapo bwawani na kuwavua samaki hao, wengine anawauza na kwa kuwa ni wengi na mimi mwenyewe nipo mbali, wengine huwapelekea hadi kwa ndugu zangu waliopo Mbagala.

“Jamani samaki wa ndugu yenu hawa, pia hapa nina fedha zake tulivua samaki tukawauza.”

Mama huyu hupewa nambari yangu ya simu hunitumia pesa zangu za samaki hao kutoka Uzaramoni Mwanadilatu na imekuwa desturi hata nikifika nyumbani Mbagala naambiwa alifika Mama yake Ustadh ametuletea Samaki Kambare na ndiyo tunamalizia malizia kuwala ndugu zangu huniambia. Huku ndugu zangu wakiniambia kuwa kumbe ni jamaa zako sana hawa? Mimi hujibu ndiyo.

Mwaka huu naambiwa kuwa mvua zinanyesha sana, mwakani itabidi niende nikawavue Kambare wangu mwenyewe angalau niwakaushe na kuwapelekea wanangu huko Tanga.

Kwa kuwa mtoto mkubwa wa huyu jirani ameniambia mvua kubwa inanyesha, ni rafiki yangu mkubwa huyu jamaa nitajaribu kumuuliza kwa kina ili aniume sikio na pengine hata ardhi niliyouziwa kule Mwanadilatu ilikuwa kwa bei ya chini kulingana na gharama halisi ikiwa kama wanalipa deni la kiwanja mraba kilichogeuzwa sambusa, haya ni mawazo yangu tu.

Hoja yangu ya leo ni moja tu, yule unayeambiwa kuwa ni adui usimfanye adui, hakikisha kumfanya rafiki yako wa karibu, kwani una uhakika gani hao unaodhani ni marafiki zako wa jana na leo wataendelea kudumu na wewe kuwa marafiki zako? Kumbuka mwenzako mie nakula Kambare wa Uzaramoni na wanangu pia watakula Kambare wa Uzaramoni na hata vitukuu vyangu pia vitakula Kambare wa Uzaramoni.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.