Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Amekutana na Kuzungumza na Balozi wa Uingereza Nchini na Kushuhudia Utiaji wa Saini ya Makubaliano Kuzuia Uhalifu na Dawa za Kulevya Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Mhe. David Concar.(kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa Mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu akiwa na ujumbe wake.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Mhe. David Concar.(kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu na kushuhudia utiaji wa saini ya makubaliano ya kupambana na Dawa za Kulevya na uhalifu hafla hiyo imefanyika leo 15-12-2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisuhudia utiaji wa Saini ya Makubaliano ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu Zanzibar, (kulia ) Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Kanal Burhani Zuberi Nassor na Afisa Muandamizi wa Ubalozi wa Uingereza Nchi Tanzania anayeshughulikia masuala ya Haki na Usalama Bw. Saimon Charters,hafla hiyo ya utiaji wa saini iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kubadilishana mawazo na Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Mhe. David Concar, baada ya kumaliza mazungumzo yao na kushuhudia utiaji wa saini ya makubaliano ya kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu Zanzibar, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa misaada mbali mbali inayoipatia Zanzibar. 

Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo  Ikulu Jijini Zanzibar, wakati alipozungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David Concar.

Amesema hatua ya Serikali ya Uingereza ya kusaini Hati ya makubaliano (MoU)  kati yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwa ni miongoni mwa hatua muhimu katika kukabiliana na uhalifu.

Alieleza kwa vile  Zanzibar ni kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki , kuna umuhimu mkubwa wakuhakikisha  suala la kuopambana na uhalifu linapewa nafasi,  hivyo akatumia fursa hiyo kuiomba Uingereza kusaidia vifaa vya uchunguzi (body scanner) katika viwanja vyake vya Ndege  na Bandarini.

Aidha, alimweleza Balozi huyo kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na hali ya uhalifu  ilivyo hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi alimhakikishia Balozi Concar kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari kutoa udhamini kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi mbalimbali, sambamba na kupongeza  azma ya kufanyika kwa Jukwaa  la kibiashara kati ya Uingereza na Zanzibar, baadae mwakani na kusema hatua hiyo itaitangaza Zanzibar Kimataifa.

Aidha, alisema suala la udhibiti wa uhalifu katika eneo la bahari linahitaji Teknolojia  mbali mbali, hivyo akaiomba Uingereza kusaidia katika nyanja hiyo ili kukimarisha Kikosi cha kuuzuia magendo (KMKM).

Alisema pamoja na kuwepo janga la ugonjwa wa Covid – 19 Duniani, kumekuwepo na ongezeko la idadi ya Watalii wanaoingia Zanzibar mwaka huu, hususan kutoka Mataifa ya Ulaya Mashariki.

Nae, Balozi David Concar  alieleza kufurahishwa na utayari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusaini Hati hiyo ya makubaliano  huo na kusema mashirikiano ndio njia pekee ya kukabiliana na uhalifu.

Alisema Kihistoria Zanzibar ni kitovu cha Biashara, hatua inayoifanya muda wote kuwa katika shabaha ya wahalifu.

Balozi Concar alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi na kusisitiza azma ya kufanya kazi nae kwa karibu, huku akitumia fursa hiyo kumpongeza kwa mafanikio yalioanza kupatikana.

Alisema Serikali ya Uingereza itafanya juhudi kusaidia upatikanaji wa  taasisi zinazotoa mikopo nafuu ili iweze kuimarisha miundo mbinu ya barabara pamoja na Uwanja wa Ndege wa Karume Pemba.

Wakati huo huo, akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Saada Mkuya Salum alisema Hati ya Makubaliano (MOU) iliotiwa saini kati ya Serikali ya Uingereza  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaiwezesha Uingereza kuisaidia Zanzibar katika nyanja mbali mbali za kukabiliana na uhalifu, hususan wa dawa za kulevya.

Alisema wiki ijayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kubadili sheria kutoka Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya na kuwa Mamlaka ili kuiwezesha kuwa na nguvu za kisheria katika kupambana na uingizaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, alisema Serikali ya Uingereza itasaidia katika kuwajengea uwezo watendaji wa Mamlaka hiyo katika maeneo tofauti ili waweze kusimamia vyema utekelezaji wa sheria, sambamba na  kusaidia upatikanaji wa vifaa.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kupamba na dawa za Kulevya Kanali Burhan Nassor alisema lengo la kutia saini MOU ni kuijengea uwezo Tume hiyo ili iweze kupambana kikamilifu na wahalifu wa dawa za kulevya.

Alisema kuna wahisani mbali mbali wanaosaidia mapambano hayo, ikiwemo UNODC ambayo imenoyesha nia ya kuleta vifaa vya uchunguzi (body screen mashine) kw aajili ya matumizi katika milango yote ya kuingilia nchini.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kuachana na biashara hiyo kwani hivi sasa wataweza kushikwa kupitia teknolojia ya kisasa.

Katika hafla hiyo,  Ofisa mwandamizi wa Ubalozi wa Uingerza n#chini Tanzania anaeshughulikia masuala ya haki na Usalama Simon Charters alitia saini kwa upande  wa Serikali ya Uingereza, wakati ambapo Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya Kanali Burhan Nassor  alitia saini kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.