Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amewashukuru Wananchi wa Zanzibar kwa Kudumisha Amani na Utulivu.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kutowa Salamu za Mwaka Mpya kwa Wananchi kupitia vyombo vya habari katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2022, katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 31-12-2021.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewashukuru wananchi wa Zanzibar  kwa kudumisha amani na utulivu na kuwaomba kuendelea kuzidisha tunu hizo katika mwaka mpya wa 2022 kwani ni msingi muhimu wa juhudi za kuleta maendeleo na kuwavutia wawekezaji.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika risala yake aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2022, risala aliyoitoa huko ofisini kwake Ikulu Zanzibar.

Katika risala yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa katika mwaka wa 2021 unaomaliza viongozi, wawakilishi wa taasisi mbali mbali za Kimataifa pamoja na Mabalozi na watu mashuhuri waliitembelea Zanzibar na kuonesha kuridhishwa kwao na hali ya amani, mapenzi, ukarimu pamoja na mshikamano uliopo.

Rais Dk. Mwinyi aliwasisitiza wananchi kuazimia kuendeleza utamaduni huo kwa faida ya nchi na watu wake huku akisisitiza kwamba kati ya mambo makubwa ya kumshukuru MwenyeziMungu katika mwaka 2021 ni kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu pamoja na umoja na mshikamano wa wananchi.

Aliongeza kuwa katika kipindi chote cha mwaka 2021 hali ya amani imeweza kudumu nchini na kuiwezesha Serikali kutekeleza vyema majukumu yake ya kuwahudumia wananchi katika kukuza uchumi, kuimarisha miundombinu mbali mbali na kuendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, vitendo vya udhalilishaji pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo bila ya muhali au kumuonea mtu yeyote.

Katika risala hiyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ni vyema kila mwisho wa mwaka ukaendelezwa utamaduni wa kutathmini mafanikio na changamoto kwa yale mambo yaliyopangwa kufanywa.

Alilieleza tukio la kihistoria lililotokea nchini katika mwaka 2021 ni kuanza kwa uongozi wa Serikali ya Jamhui ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Sita, ikionozwa na Rais Samia SuluhuHassan akiwa Rais mpya wa kwanza mwanamke nchini.

Pia aliyaeleza matukio yaliyoacha alama katika historia nchini katika kwa a2021 ambayo ni misiba ya Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyefariki Machi 17,2021 na Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliyefariki dunia Februari 17,2021.

Alieleza changamoto ambayo iliendelea kukabiliana nayo katika mwaka 2021 kwa Zanzibar, Tanzania na duniani kote kuwa ni janga la maradhi ya UVIKO-19 ambalo limechangia sana kuzorotesha uchumi nchini kama ilivyo kwa mataifa kadhaa duniani.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali imechukua hatua mbali mbali za kukabiliana na ugojwa wa UVIKO -19 kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa, nchi marafiki, sekta binafsi na Watumishi wa sekta ya afya.

Alisema kuwa Serikali imeshaanzisha vituo 41 vyenye kutoa huduma za chanjo ya UVIKO 19, kati ya hivyo 29 viko Unguja na 12 viko Pemba na kuwataka wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika mwaka 2022 huku wakichukua hadhari ya maradhi ya UVIKO 19 hasa kwa kujikinga na virusi vipya vya Omicron.

Katika juhudi za kukabiliana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO -19,  Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali imepata mkopo wa dola za Kimarekani milioni 100 sawa na TZS za Kitanzania Bilioni 230 ambazo zitatumika  katika ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, maji na nishati ya umeme.

Pia, alisema kuwa Serikali imetenga TZS Bilioni 81 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali wadogo wadogo na wakati.

“Nawasihi wananchi wote tushirikiane katika kutekeleza miradi tuliyoipitisha na mikopo itakayotolewa kwa wajasiriamali”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwakubusha Watanzania wote umhimu wa Sensa ya Watu na Makaazi ambapo inatarajiwa kufanyika katika mwaka 2022 ambapo aliwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa maofisa  wahusika ili zoezi hilo muhimu lifanyike kwa mafanikio.

Kadhalika aliwakumbusha wananchi kwamba kuanzia Januari 01 hadi Januari 12,2022 kutakuwa na shamra shamra za maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hivyo, aliwahimiza kujitokeza kwa wingi katika matukio mbali mbali yaliyopangwa kwa ajili ya sherehe hizo.

“Natoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Zanzibar, Tanzania kwa jumla, Viongozi wa nchi rafiki, taasisi na washirika wetu wa maendeleo “,alisema Dk. Mwinyi.

Imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.