Habari za Punde

Waathirika wa Masterlife Unguja na Pemba Wanatarajiwa Kulipwa kwa Awamu ya Kwanza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Masterlife ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya kuzuwia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi  Zanzibar (ZAECA) Khamis Ahmedi Makarani akielezea  kuhusu utaratibu mzima wa kulipwa Fedha kwa Wahanga waliyoweka katika Kampuni ya Masterlife, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari , Ukumbi wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mjini Znzibar.
Kamishna wa Bajeti kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Saumu Khatib Haji akifafanuwa kuhusu Utaratibu  Utakaotumika waulipaji wa Fedha za Wahanga wa Masterlife zoezi linalotarajiwa kuanza Decemba 8 hadi 14 kwa Unguja na Pemba.

JUMLA ya waathirika wa kampuni ya masterlife, Unguja na Pemba kwa awamu ya kwanza wanatarajiwa kulipwa fedha zao waliowekeza katika kampuni hiyo.

Mwenyekiti wa kamati ya Masterlife ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamalaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) Khamis Ahmed Makarani alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Vuga Mjini Unguja.

 

Alisema serikali itaanza kurejesha fedha hizo kwa waathirika hao kuanzia Disemba 8 hadi Disemba 14 na watakaohusika na zoezi hilo ni wale ambao waliweka kuanzia kiasi cha shilingi 100,000 hadi shilingi 1,000,000 ambapo kiwango cha fedha zitakazolipwa kinakaribia kufikia shilingi bilioni 2.5.

 

Aidha alisema wameanza na wananchi waliowekeza kiwango hicho na baadae zoezi hilo litakwenda kwa wananchi wa awamu ya pili.

 

Mwenyekiti Makarani, alibainisha kwamba zoezi hilo kwa Unguja litaanza Disemba 8 hadi Disemba 10 kwa Mjini ni kiwanja cha kufurahishia watoto Kariakoo na Kaskazini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kisiwa cha Pemba zoezi hilo litaanza Disemba 13 na 14 katika kituo cha Makonyo Kusini Pemba.

 

Aliwasisitiza wananchi ambao wamo katika hatua hiyo kuhakikisha kwamba wanakwenda na vielelezo muhimu ikiwemo mkataba wake original, kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi au Mtanzania alichotumia wakati wa usajili wa kuweka fedha na picha moja ya paspoti saizi.

Alisema hatua hiyo inatokana na kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwahakikishia wahanga hao kila mmoja anapatiwa haki yake.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashitaka Salma Ali Hassan, akizungumia jambo hilo alisema kwa mujibu wa sheria na kijinai wananchi na kampuni hiyo wote walikuwa ni washitakiwa.

 

“Kwa kweli wananchi tumshukuru Rais Mwinyi kwani ametumia busara katika jambo hili kwani kisheria nilikuwa na washitakiwa wengi ikiwemo wamiliki na wananchi kwani pande zote mbili zilikuwa zimefaya makosa,” alisema.

 

Hivyo, aliwakumbusha wananchi wanapofanya miamala yao kuhakikisha wanafuata taratibu za kisheria ili kadhia hiyo isijirejee tena kwani jambo walilofanya halirusiwi.

 

Saumu Khatib Haji ni Kamishna wa Bajeti Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, alisisitiza kwamba wanapofanya malipo hawatokubali uwakilishi wa mtu katika zoezi hilo kwani kamati tayari imeshaandaa utaratibu maalum wa wale wagonjwa ambao wamo katika orodha hiyo basi wanapatiwa haki yao.

 

Aliwasisitiza wananchi kuhakikisha wanafuata maelezo na taratibu zilizowekwa katika zoezi hilo kwa kuchukua vitu vyao vyote ili waweze kupatiwa amana yao.

 

“Nazungumzia hili kwa sababu katika uhakiki tulipata changamoto kubwa ya watu wengi kutojua mikataba yao walipoweka sasa ni wakati kwao kujipanga na kuwa tayari ili kuhakikisha wanapata haki yao kama ilivyokusudiwa,” alishauri.

 

Kwa upande wa wale ambao hawataweza kuhudhuria katika awamu hiyo kutokana na sababu mbalimbali alisema utaratibu mwengine utatumika katika kuwalipa fedha zao.

 

Hivyo aliwaasa wananchi ambao hawamo katika orodha ya awamu ya kwanza ya wanaotakiwa kulipwa basi wasubiri siku nyengine.

 

Sambamba na hayo alisema Serikali imeamua kuvipiga mnada vitu vyote vilivyokuwa vikimilikiwa na kampuni ya masterlife kwa lengo la kuongeza fedha katika mfuko wao na kuweza kuwalipa wananchi.

 

“Kama tulivyomsikia Rais Mwinyi kwamba mpaka sasa pesa zilizopatikana kwa kampuni hiyo ni shilingi bilioni 6.7 ni fedha kidogo mno n ahata tukiuza vitu hivi basi haifikii kiwango cha fedha wanazodai wananchi,” alisema.

 

Alisema ukiangalia wananchi wengi waliothirika zaidi ni wafanyabiashara wadogo wadogo ikiwemo mama lishe na kuhakikisha wanaanza nao ili  waweze kuendeleza kazi zao za kujipatia uchumi.

 

Naye Mwenyekiti wa wahanga wa master life

Thabit Mohammed Saleh aliishukuruserikali kwa hatua waliyofikia kuona inawasaidia wananchi wake katika kuwapatia haki yao.

 

Alisema wanatambua kwamba jambo hilo lilianza zamani katika hatua za taharuki kubwa kwa wahanga walioweka fedha zao katika kampuni hiyo.

 

Walimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa hatua ya kuteuwa kamati ambayo imefanya kazi kwa bidii katika kuona kila mwananchi aliwekeza fedha zake anapata.

 

Aliwaomba wananchi kuiamini kamati hiyo kwa yale yote waliyoyapanga katika hatua za ulipaji na kuona kwamba kila mmoja anapata haki yake aliyoiwekeza katika kampuni hiyo.


Rais wa Zanzibar DK Hussein Ali Mwinyi wakati akihutubia taifa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake alisema Kampuni hiyo ilikusanya kiasi cha shilingi Bilioni 38.7 kwa wananchi 10,317wengi wao wakiwa wanyonge na kusema kuwa Serikali imeamua kuwalipa wananchi hao amana zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.