Habari za Punde

Wahamasishaji Wanawake Kudai Haki Zao za Uongozi na Demokrasia Kisiwani Pemba.

Na Gaspary Charles- TAMWA ZNZ

MKURUGENZI wa Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania, TAMWA- Zanzibar Dkt. Mzuri Issa Ali, amewataka wahamasishaji jamii kwa wanawake kudai haki zao za uongozi na demokrasiua kisiwani Pemba kuendelea kufuatilia na kuibua changamoto zinazowakwaza wanawake kukosa haki zao katika nyanja mbalimbali kwenye jamii.

Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano baina ya watendaji wa TAMWA ZNZ, PEGAO na wahamasishaji hao wenye lengo la kujadili na kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo kisiwani humo unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway.

Alisema lengo la mradi kuwatumia wahamasishaji hao ni kutaka wafanye kazi ya kukutana na wanajamii kwa lengo la kubaini changamoto zinazowakabili na kuwasaidia uwezo wa kudai haki zao katika masuala mbalimbali ikiwemo demokrasia na uongozi.

Alisema, “jukumu letu ni kumlika uwajibikaji wa kila mmoja au taasisi ili kufuatilia uwazi, uwajibikaji na upatikanaji wa haki za wanawake kwenye jamii katika kila nyanja.”

Aidha alisisitiza ufuatiliaji wa karibu changamoto zote zinazoibuliwa katika jamii ili ziweze kutatuliwa na ngazi husika kwa wakati kutokana na kwamba mradi huo haujajikita katika masuala ya uongozi pekee.

”Kuendelea kufanya mikutano na wanajamii na kuibua changamoto nyingi pasipo kuzitaftia ufumbuzi wa suluhu yake itakuwa hatujafanya kitu na lengo la wahamasishaji jamii katika mradi huu ni kuhakikisha tunaibua changamoto na kuzifanyia ufuatiliaji wa karibu ili wanawake wapate haki zao zote,” alisema Dkt. Mzuri.

Alitaja miongoni mwa maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa ufuatiliaji wa karibu na wahamasishaji hao kuewa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za afya, wanawake kukosa vitambulisho Pamoja na uhaba wa huduma nyingine zote za kijamii.

Alisema, “kama kuna huduma yoyote ambayo kwa njia moja ama nyingine inamuathiri mwanamke na nyinyi mmeshaibaini jukumu lenu la kwanza ni kuifanyia ufuatiliaji kwa mamlaka husika ili tatizo hilo liweze kutafuta ufumbuzi wa kudumu.”

Mapema mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said, alisema wahamasishaji hao wamefanya kazi kubwa ya kuifikia jamii na kufanikiwa kuibua changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi.

“Baada ya kufanya kazi kubwa ya kuifikia jamii kuihamasisha imeonekana zipo changamoto nyingi zilizoebuliwa na zinahitaji kufanyiwa kazi ili malengo ya mradi wetu yakamilike,” alisema Hafidh.

Rukia Ibrahim mmoja wa wahamasishaji hao kutoka Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba alisema hamu yao ni kuifikia wilaya yote na kuzibaini changamoto zinazowakabili wanawake na kuzifanyia utetezi kwenye ngazi husika.

‘Kwa mfano kwenye mikutano yetu tulibaini uwepo wa huduma dhaifu kwenye vituo vya afya mbamimbali katika Wilaya ya Wete, baada ya kulibaini hilo tutalifikisha kwa wahusika nah atua zaidi zinaendelea kuchukuliwa,’’alifahamisha.

Maryam Said alieleza katika uhamasishaji wanawake kushiriki kwenye uongozi walishajihisha wanawake kutumia haki yao ya kujiunga katika vyama vya siasa ili kujiwekea mazingira mazuri ya kuchaguliwa kuwa viongozi.

Alieleza, “tuliwahamasisha wanawake kujiunga katika vyama vya siasa mapema ili waweze kuwa na haki ya kushiriki kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia vyama vya siasa.”

Nae Khalfan Amour Mohame kutoka wilaya ya Micheweni, alisema uwazi na uwajibikaji ndio njia pekee itakayosaidia ufikiaji wa malengo katika jamii.

Mradi wa kuhamasisha wanawake kudai haki zao za uongozi na demokrasia katika jamii unatekelezwa kwa miaka minne Zanzibar na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar ZAFELA Pamoja na PEGAO kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Norway Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.