Habari za Punde

Waziri Mhe.Dkt.Mwigulu Aagiza Chuo cha Mipango Kupanua Wigo wa Huduma za Utafiti Nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) akimtunuku cheti mwanafunzi wa Shahada ya udhamili Bw. Sterwad Vidoga, katika Mahafali ya 35 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Jijini Dodoma.

Na. Ramadhani Kissimba, WFM, Dodoma.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewaagiza watendaji na watalaamu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kupanua wigo wa huduma za utafiti ambazo ni muhimu katika kutatua changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazowakabili wananchi.

Dkt. Mwigulu ametoa maagizo hayo wakati wa mahafali ya 35 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini katika Kampasi Kuu ya Dodoma, ambapo wahitimu 5,562 wakiwemo wanaume 2,299 na wanawake 3,263 wametunukiwa tuzo za shahada katika kozi mbalimbali zinazohusu Mipango, Maendeleo, Fedha na uwekezaji.

Mhe. Mwigulu amesema Kwa bahati mbaya, machapisho mengi ya wanataaluma  huishia kwenye majarida na maktaba ambazo zinasomwa na watu wachache hivyo matokeo ya utafiti kushindwa kuwafikia walengwa wakuu ambao ni wananchi wa vijijini na kukiagiza chuo hicho kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zinazofanywa yanawafikia walengwa kwa lugha wanayoielewa ambayo ni kswahili rahisi.

Aidha Dkt. Mwigulu amewataka wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuwa tayari kuwasaidia vijana wanaohitimu elimu ya juu ili waweze kuingia kwenye soko la kujiajiri kwa kujiamini wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kukuza ajira rasmi.

‘’Mathalani, pamoja na uhalisia kuwa katika nchi yetu kati ya vijana 100 wanaoingia kwenye soko la ajira, ni vijana 7 tu ndio wanapata ajira kwenye sekta rasmi’’ Aliesma Dkt. Mwigulu.

Kwa upande wa Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Dkt. Nchemba alisema Serikali itaendelea kuboresha mikopo hiyo kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu ili iwafikie wanafunzi wengi zaidi wenye sifa na kwamba maelekezo aliyopewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kulipa fedha za mikopo hiyo kwa wakati yanatelezwa

 ‘’Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza nguvu kubwa katika miundombinu ya vyuo nchini na kunielekeza kuwa kijengwe chuo Kikuu cha Tehama na yupo macho sana kuhakikisha kuwa miundombinu ya vyuo vyetu inaboreshwa na chuo hiki cha Mipango ni miongoni mwa vyuo vitakavyonufaika na mpango huo” alidokeza Mhe. Mwigulu

Katika mahafali hayo Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Hozen Mayaya alisema kutokana na changamoto ya ajira, Chuo chake kimeanzisha Kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali ambapo mawazo ya ubunifu ya vijana hulelewa na kuwawezesha mawazo yao ya ubunifu kuwa ya kibiashara.

Prof. Mayaya alisema kuwa kwa miaka mingi fursa kubwa kwa wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini imeelekezwa kuwafundisha wanavyuo kujiajiri, hivyo kuwataka wahitimu kuchangamkia fursa za kuajiriwa ama kujiajiri katika sekta mbalimbali za uchumi nchini.

‘’Hatuna shaka baada ya wanafunzi wetu kuhitimu watatumia ujuzi walioupata hapa chuoni kuajiriwa, kujiajiri na kuwaajiri vijana wenzao’’. Aliongeza Prof. Mayaya

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Prof. Martha Qorro, alimpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambapo katika kipindi cha siku mia moja madarakani ametekeleza mambo kadhaa ya maendeleo yakiwemo, kuanzisha zaidi ya miradi 90 iliyotoa ajira zaidi ya 24,000.

Aliyataja mafanikio mengine yaliyopatikana chini ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kuwa ni pamoja na Kupunguza urasimu katika uwekezaji na usajili wa miradi ya uwekezaji, kuondoa tozo 232 zilizokuwa zinawakwaza wafanyabiashara, Kuendeleza na kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na nchi jirani na Ujenzi wa shule za sekondari za wasichana kila wilaya.

Awali kabla ya mahafali hayo Waziri wa Fedha na Mipango aliweka mawe ya msingi katika majengo mawili ya ujenzi wa Ukumbi wa Mihadhara ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.9 na ujenzi wa Bweni la Wanafunzi wa Kike lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 200 ambalo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 1.7

Baada ya uzinduzi wa ujenzi wa miradi hiyo, Mhe. Mwigulu alilihakikishia Baraza la Chuo kuwa Serikali itaendelea kukisaidia Chuo hicho kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ili kukidhi viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa.

Dkt. Christina Geofrey akiongoza maandamano wakati wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, jijini Dodoma. Watatu kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na kulia ni Mkuu wa Chuo hicho Prof. Hozen Mayaya.







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.