Habari za Punde

Zanzibar yaadhimisha siku ya kimataifa ya watu wenye Ulemavu duniani


 Ndugu Wananchi,

Ifikapo tarehe 3 Disemba ya kila mwaka, wananchi wa Zanzibar huungana na wenzao duniani kote katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu

Duniani.

Ndugu Wananchi,

Mnamo mwaka 1976 nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, baada ya kuangalia maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu duniani imeona kwamba, bado masuala ya Watu Wenye Ulemavu hayajatiliwa mkazo wa kina hususan kwa upande wa haki za binadamu. Kati ya mwaka 1983 hadi 1992 hatua mbali mbali zilichukuliwa, ikiwani pamoja na maamuzi ya mwisho ya Umoja wa Mataifa, kuitangaza tarehe 3 Disemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Maadhimisho ya Watu wenye Ulemavu Duniani.

Ndugu Wananchi,

Kauli mbiu ya mwaka huu ‘‘Uongozi na Ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu, kuelekea ujumuishwaji na ufikiwaji endelevu baada ya uviko 19 Duniani’’ Kaulimbiu hii inakwenda sambamba na Sheria ya Zanzibar ya Watu wenye Ulemavu (Haki na Fursa) Na 9 ya mwaka 2006. Vilevile, Mkataba wa Kimataifa wa haki za Watu wenye Ulemavu ambao, Tanzania imeuridhia na kutia saini mwaka 2009 kwa lengo la kuutekeleza.

Ndugu wananchi.

Katika kuimarisha maisha ya Watu wenye Ulemavu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza yafuatayo:

Kuanzisha Sera mpya ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2018 pamoja na Mpango wa utekelezaji wa Sera hiyo, Mpango Mkakati wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu umeandaliwa, kuanzishwa kwa Mfumo wa Takwimu, “Jumuishi Data Centre”, Serikali imeandaa Muongozo wa Miundombinu Rafiki kwa Watu wenye Ulemavu na Kuanzishwa Mfuko wa Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu wenye lengo la kutoa Ruzuku ya Afya na Elimu na uwezeshaji kiuchumi.

Ndugu wananchi.

Bado Serikali yetu inaungana na Watu wenye Ulemavu wote katika mipango ya maendeleo ikiwemo Dira 2050 na ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM 2025.

Madhumuni ya siku hii ni, kukuza uelewa wa haki za Watu wenye Ulemavu katika kila Nyanja za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Kwa mwaka 2021 siku hii itaadhimishwa kitaifa katika viwanja vya "NUNGWI - HAMBURU, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe: Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe, Othman Masoud Othman.

Shime kila mmoja wetu mkubwa, mdogo, kike kwa kiume kuhudhuria katika viwanja vya Hamburu ili kuwaunga mkono Watu wenye Ulemavu Zanzibar.

Mungu Ibariki Afrika,

Mungu Ibariki Tanzania,

Mungu Ibariki Zanzibar.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.