Habari za Punde

Mhe Chande: Awataka Bodi ya Wakurugenzi NBAA Wakafanye Kazi kwa Kufuata Sheria.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi YA Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano APC Bunju jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), baada ya kuizindua rasmi Bodi hiyo. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NBAA, Prof. Sylivia S. Temu na kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA CPA Pius Maneno jijini Dar es Salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini)

Na.Josephine  Majura WFM – Dar es Salaam.                                                                             

Serikali imeitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania  (NBAA), wakati wa utelekezaji wa majukumu yao kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa.


Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano-APC Bunju jijini Dar es Salaam.


“Hii Bodi  kazi yake kubwa ni kuweka sera na mikakati itakayoiongoza na kuishauri Menejimenti katika kutekeleza majukumu ya Taasisi kwa kuzingatia sera za serikali katika kutoa huduma kwa wananchi” alisema Mhe. Chande.


“Ni matarajio ya Serikali kwamba mtafanya kazi yenu kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu kwa maslahi mapana ya Taifa letu”alisema Mhe. Chande.


Aidha aliwataka wajumbe wa Bodi kutumia vitendea kazi walivyopewa ikiwemo nyaraka mbalimbali zenye maelezo ya majukumu ya Bodi na Taasisi  zinavyofanya kazi ili iwe rahisi wakati wa  utekelezaji wa majukumu.


“Nimesikiliza maelezo ya Mtendaji wa NBAA, nimeweza kufahamu japo kwa uchache kuhusu majukumu ya Taasisi yetu ya NBAA kwa kuzingatia kuwa nami nimeteuliwa siku za hivi karibuni kushika wadhifa huu wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango”, alisema Mhe. Chande.


Aliongeza kuwa atafanya ziara rasmi za kuzitembelea Taasisi zote zilizo chini ya wizara ikiwemo ya NBAA ili  kufahamu kwa undani majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Taasisi za Wizara ya Fedha na Mipango.


Mhe. Chande aliitaka Bodi hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano katika kuisimamia Taasisi ya NBAA kwa mustakabali wa kada za Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu ambao ni muhimu katika kusimamia rasilimali fedha.


Natoa pongezi binafsi kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kukuteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, nawapongeza pia wajumbe wote 11 wa Bodi ya NBAA mlioteuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA, Prof. Sylivia S. Temu alisema wapo tayari kufanya kazi na kuahidi kushirikiana kwa pamoja katika kusimamia taaluma ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini.


Prof. Temu alimshukuru pia Mhe. Rais kwa kumuamini na kumteua kusimamia Bodi hiyo na kuahidi kuwa watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa na Serikali ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Pius Maneno, alimshukuru Naibu Waziri kwa kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA.


CPA Maneno, alimuahidi Mhe. Chande kuwa Taasisi hiyo itaipa ushirikiano wa kutosha Bodi ya Wakurugenzi walioteuliwa ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.