Habari za Punde

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Watiliana Saini ya Ujenzi wa Madarasa na Vikosi vya SMZ.


Na.Maulid Yusseuf  WEMA. Zanzibar.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetiliana saini  na vikosi mbalimbali vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya ujenzi wa madarasa  mapya 805.

Hafla hiyo ya utiaji wa Saini imefanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mazizini Mjini Unguja ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa UVIKO 19, ambao fedha zake zinapatikana katika mfuko wa IMF.

Akizungumzia baada ya Utiaji huo wa Saini , Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Ali Khamis Juma amesema hana mashaka na utendaji wa kazi zao na kuwakumbusha kuwa kazi hiyo inatakiwa kufanywa kwa ufanisi na kumalizika kwa wakati.

Amesema kazi hiyo ya ujenzi wa madarasa ndefu na inawapasa kuwajibika kwa pamoja ili kuona Nchi inafaidika kutokana na Mkopo huo.

Hata hivyo amesema kwa upande wa Wizara ya Elimu tayari imeshajipanga katika kuona wanatumia nguvu yote ya Serikali kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwani tayari wameshawaandikia Wakuu wa Mikoa wote kuwajuilisha kazi hiyo muhusika ni nani ili nao waweze kuchukua nafasi yao katika ufuatiliaji wa ujenzi huo.

Hata hivyo amewataka kutambua kuwa miradi hiyo itatembelewa na watu wa chama ili kufuatilia ilani  ya Chama cha Mapinduzi inavyotekelezwa, hivyo amewataka kuwapa ushirikiano wakati watakapofika ili kila mmoja kutimiza jukumu lake.

Nae Mkurugenzi Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Khalid Masoud Waziri amesema pamoja na vikosi hivyo kujenga madarasa hayo mapya pia  watamalizia ujenzi wa madarasa yaliyoanzwa kujengwa na wananchi ambayo yanahitaji kumalizwa.

Bwana Khalid amevitaja vikosi hivyo kuwa ni pamoja na JKU ambao watajenga madarasa 118  mapya na kukamilisha madarasa yaliyoanzishwa na wananchi 40 katika Mkoa wa Mjini Magharibi , Kikosi cha  Mafunzo watajenga madarasa mapya 120 na kukamilisha madarasa yaliyoanzwa kujengwa na wananchi 66 katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Pia amesema Kikosi cha  FAYA kitajenga  madarasa mapya 57  na kukamilisha madarasa yaliyoanzwa kujengwa na wananchi 53 katika Mkoa wa Kusini Unguja,   ambapo kikosi cha KMKM  watajenga madarasa mapya 56  na kumalizia yaliyoanzwa na wananchi 152 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Pia kikosi cha KVZ watajenga madarasa 95 mapya na kukamilisha madarasa 48 yaliyoanzwa kujengwa na wananchi katika Mkoa wa Kusini Pemba,  ambapo amesema mikataba hiyo inaendana na Mkoa.

Wakitoa maelezo namna walivyopokea kazi hiyo Mkuu wa Kikosi cha KMKM Komodoo Azana Hassan Msingiri na Mkuu wa kikosi cha Zimamoto na Uokozi,  Kamishna Rashid Mzee Abdalla wameushukuru Wizara kwa kuwaamini na kuwakabidhi kazi hiyo na kuahidi kuifanya kwa mujibu maagizo yaliyotolewa  na Serikali katika ubora na uwezo wa hali ya juu ili malengo yaliyowekwa yaweze  kufikiwa.

pia wameiomba Wizara kuangalia suala zima la BOQ katika masuala ya  kukamilisha kazi yao kwani kunaonekana kuwepo kwa utofauti wa bei na maandishi yao kitokana na bei halisi za bidhaa katika masoko.

Jumla ya shilingi bilioni 16 milioni 452 laki 584 elfu zitatumika katika ujenzi wa Madarasa 805 katika Mikoa mitano ya Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.