Habari za Punde

ZBC Watakiwa Kutowa Taarifa Kwa Wananchi Pale Linapotokea Tatizo.-Waziri Tabia.

WAZIRI wa Habari,Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita ameuagiza uongozi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi pale linapotokea tatizo au hitilafu yeyote ya kiufundi.

Kauli hiyo ameitoa baada ya kufanya ziara ya kuangalia hali halisi iliyojitokeza baada ya kuathirika  kwa baadhi ya maeneo kufuatia radi na mvua kubwa iliyonyesha mwezi uliopita.

Alisema Serikali na Wizara inatambua changamoto zinazowakabili Shirika hilo katika uendeshaji baada ya kuharibika baadhi ya vifaa ,hivyo amewataka wafanyakazi kuwa watulivu  huku jitihada kubwa zinachukuliwa katika kuhakikisha matangazo yaliyojitokeza yanatatuliwa.

Waziri Tabia alisema kuna changamoto ambazo zimetokea za kitaalamu ambazo hazihitaji wataalamu wa ndani bali ata wa nje ya Zanzibar ambapo mda wowote ndani ya wiki  hii watawasili ili kusaidia tatizo hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo Salum Ramadhan amewataka wananchi kuwa na subra  kwani jitihada zinachukuliwa ili ZBC  kurejesha matangazo yake yatakayo kuwa na ubora zaidi.

Kwa upande wake fundi wa ZBC ambaye pia Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Tehama Iddi Mohamed alisema  wanatarajia kupokea wataalamu hivi karibuni kwa ajili ya kufanya matengenezo ya baadhi ya vifaa vilivyoharibika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.