Habari za Punde

Zoezi la ugawaji wa kadi za CCM za Kielektroniki katika Wilaya ya Kusini Unguja

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla, akizungumza na wanachama wa wilaya ya kusini Unguja katika zoezi la ugawaji wa kadi za CCM za Kielektroniki katika Wilaya ya Kusini Unguja Kichama.

 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla,akimkabidhi kadi ya uanachama wa CCM Ndg. Soud Nahoda Hassan katika hafla hiyo ya ugawaji wa kadi za kielektroniki katika Wilaya ya Kusini Unguja.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Sadalla , ameataka viongozi wa Chama Wilaya ya Kusini Unguja kuhakikisha kadi mpya za uanachama za Electroniki zinawafikia wanachama wote wenye sifa na vigezo vya kupata kadi hizo.

Wito huo aliutoa katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa kadi hizo katika wilaya ya Kusini Unguja, alisema lengo la kadi hizo ni kuwafikia walengwa kwa haraka ambao ni wanachama ili zitumike katika shughuli mbali mbali za Chama.

Alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni taasisi ya kisiasa inayoenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, ndio maana ikaweka mfumo imara wa kadi za kisasa zinazohifadhi kumbukumbu zote za wanachama wa ccm.

“Matarajio yetu ni kuwa kadi hizi hazitokaa maofisini mwenu, hakikisheni kila mwanachama anayestahiki kupata kadi anapewa bila vikwazo.”,alisisitiza Dk.Mabodi.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi, alieleza kuwa ugawaji wa kadi hizo ni mwendelezo wa zoezi la uzinduzi wa kadi lililotekelezwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndg.Samia Suluhu Hassan katika kilele cha kuadhimisha kutimiza miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM kilichofanyika Mkoani Mara.

Kupitia hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo aliwasihi wanachama,viongozi,watendaji na makada wa CCM kuhakikisha wanazitunza vizuri kadi hizo kwani uzalishaji wake ni gharama kubwa.

Alisema hatua kubwa za kimaendeleo katika nyanja za Kisiasa,Kiuchumi na kijamii zilizofikiwa na Chama Cha Mapinduzi, zinatakiwa kwenda sambamba kasi ya wanachama kukitumikia chama bila kuchoka.

Pamoja na hayo aliwataka wanachama waliokabidhiwa kadi kuendelea kusimamia na kuishi katika Itikadi ya CCM ya ujamaa na kujitegemea.

 “Chama Cha Mapinduzi ni itikadi inayoamini kutoka moyoni, hivyo endeleeni kujitoa kwa ari na mali kukitumikia Chama chetu bila kujali vikwazo vyovyote viwe vya kimazingira au baadhi ya watu wasiopenda maendeleo yetu", ”alisema Dk.Mabodi.

Alisisitiza kwamba itikadi ya CCM ndiyo inayoamua masuala yote muhimu ya maendeleo ya nchi zikiwemo uimarishaji wa huduma za Afya,Elimu,Kilimo bora,maji safi na salama,miundombinu ya barabarani,majini,angani na nchi kavu.

Aliwataka wanachama wa zamani kuwaenzi na kuwaheshimu wanachama wapya kwani ndani ya CCM hakuna ubaguzi wanachama wote wana haki sawa.

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa Chama Dk.Mabodi, aliwakemea baadhi ya wanachama walioanza kutengeneza makundi ya kukigawa chama wa kuwafanyia kampeni za siri baadhi ya watu wakati bado viongozi wa Chama na Serikali hawajamaliza muda wao wa uongozi.

Dk.Mabodi, akizungumzia zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu 2022, aliwasisitiza wanachama na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa ili serikali iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa takwimu sahihi ya Watu na Demografia.

Naibu Katibu Mkuu huyo, alikemea vitendo vya udhalilishaji na kuwataka wanachama na wananchi wa Wilaya ya kusini kupinga vitendo hivyo na kuhakikisha wanaendelea kuishi  katika maadili,mila na desturi sahihi za kizanzibar.

Katika hatua nyingine Dk.Mabodi, alikemea tabia za baadhi ya wananchi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kukosoa na kubeza kwa kejeli hatua za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“ kuna kundi linatumia mitandao ya kijamii kubeza juhudi kubwa za maendeleo zinazofanywa na Serikali yetu, tunajua lengo lao ni kudhohofisha juhudi hizo  na sasa tunawambia hatuwezi kurudi nyuma ni mwendo wa kasi hadi  2025 “, alisema Dk.Mabodi.

Kupitia kikao hicho aliwapongeza Wana CCM wote walioshiriki katika uzinduzi wa sherehe za miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika Wilayani humo.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Amina Imbo, alisema walipokea kadi mpya 4,000 ambapo Wilaya ya Kusini Unguja wamepewa kadi 1,782 na Wilaya ya kati walipewa kadi 2,218.

 Naye Katibu wa CCM Wilaya hiyo Asha Mzee, alisema wanachama wote ni 14,484 ambapo waliosajiliwa awali ni 8,800 na usajili mpya ni 1,140 ambapo waliosajiliwa mpaka sasa ni wanachama 9,940.

 

Akieleza kazi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji ,Rahma Kassim Ali ambaye ni Mwakilishi wa Viti Maalum mkoa wa Kusini Unguja alisema tayari serikali imekwishamaliza maliza kufanya upembuzi ya kinifu barabara za ndani zenye urefu wa umbali wa kilomita zaidi ya 200 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema katika barabara hizo tayari wapo eneo la mradi kwa ajili ya kumalizia michoro ya ujenzi wa barabara hizo.

Naye Waziri wa Kilimo,Maliasili,Umwagiliaji na Mifugo,Soud Nahoda Hassan ambaye ni Mwakilishi wa jimbo la Paje alisema tayari serikali imekwishaanza utafiti kwa ajili ya matumizi bora ya mbolea za asili na wamefanya hivyo baada ya kubaini kuwa mbolea za kisasa zichangia maradhi mengi za binadamu.

 

Alisema serikali inatarajia kuanza kuhakikisha wakulima wanaanza kutumia miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika mabonde yote ya kilimo cha mpunga ili kuhakikisha Zanzibar inajitosheleza kwa chakula na badala ya kutoagiza nje ya Zanzibar.

 

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.