MAPISHI YA KIZANZIBARI
Adeladius
Makwega-DODOMA
Mara nyingi
nilikuwa mvivu wa kula chakula kwa akina pangu pakavu tia mchuzi kutokana na namna
mapishi yake yalivyokuwa yanapikwa, kidogo ilikuwa sijayazoea. Si kwamba
mapishi haya yalikuwa mabaya la hasha bali mapishi mengi yalikuwa katika namna nisiyozoea.
Mapema
mwaka huu 2022 ulianza kwa neema kwa siha yangu kwani walikuja wapikaji wapya, nilijulishwa
kuwa wanatokea huko Zanzibar bila ya kufahamu kama walikuwa Wagunya, Washirazi
au Watumbatu.
Wenzangu
waliniambia kuwa ndugu hawa wanapika vizuri sana.
“Kichungu
huonjwa ”
Waswahili
husema hivyo, lakini leo mwanakwetu mimi nakwambia, hata kitamu huonjwa pia.
Kwa hiyo
nilisogelea genge(Mkahawa) la Kizanzibari na kuanza kula. Mapishi haya yalikuwa
matama mno, mwanakwetu nilijinoma mno.
Chakula
chao kilikuwa na kipimo kikubwa na huku wakiweka Nyama, Maharage, Dagaa na
Kisamvu.
Kisamvu
hichi kiliungwa vizuri huku wakikiwekea pilipili kwa mbali.
Kwa
kuwa walikuwa wananiletea chakula hicho niliwauliza namna wanavyounga Kisamvu
chao.
“Tunakichemsha,
kikiiva tunakitia nazi, kinawekwa maziwa, kinawekwa karanga na kinawekwa viungo
vingine kama chumvi, vitunguu maji na vitunguu swaumu kwa kiasi.”
Wakati
ninaambiwa mapishi haya, moyoni nilisema kuwa haya kweli mapishi ya Kizanzibari
na yalikuwa yamekamilika kweli kweli. Nikasema Wazanzibari Kidogo wanaweza
kupika kama Binti Mkomangi (bibi yangu mzaa baba).
Kila
siku niliendelea kula chakula hiki huku nikiogopa kulishwa LIMBWATA LA KIZANZIBARI
maana Binti Mkomangi aliniambia kuwa ukiwa mwanaume usipende kula sana vyakula
vya wanawake mbalimbali, vingine huwa haviliki, ukionja tu hauwezi kuviacha
milele.
“Usipende
kula vyakula vya wanawake mbalimbali, vingine huwa haviliki, ukionja tu,
hauwezi kuviacha milele.”
Niliyakumbuka
maneno hayo ya Binti Mkomangi mara mbili mbli kwangu kwani mwaka 2004 wakati
nakwenda Isimani-Iringa kuanza kazi bibi aliniambia kuwa Wahehe, Wakinga na
Wabena wana LIMBWATA lao linalofahamika kama LITAMBULILA kwa hiyo niwe makini
sana.
Nikiwa
Iringa akina Segito, Semuyala,Semdeke, Sechaula, Semlelwa walinipikia vyakula
lakini sikuweza kuvionja kuogopa Litambulila. Lakini sasa mapishi ya
Kizanzibari yamenivutia mno nikawa nakula kila siku tangu Januari hadi Machi 2,
2022. Nikiwa naliogopa limbwata la Zanzibari huku sifahamu linaitwaje?
Siku ya
Jumatano ya Majivu, nilifika kwa akina pangu pakavu tia mchuzi, nikatulia tuli
na ilipofika saa sita juu ya alama dada wa Kizanzibari alikuja na chakula chake
kuniletea.
Nilimjulisha
kuwa leo kidogo nina dharura.
Binti
huyu alijisikia vibaya mno, akitambua kuwa sasa amempoteza mteja wake, nilimwambia
kuwa usiwe na shaka mimi bado ni mteja wako lakini leo nina jambo langu.
Alipokuja
nilipo alikuwa na kikapu chake kikubwa kilichojaa mikeba ya plastiki yenye
vyakula, alikaa katika kiti na kuanza kutoa machozi.
Binafsi
ni muda mrefu kumuona mtu analia jirani yangu, hata mimi hulia sana lakini si
hadharani, nikiwa na jambo langu huingia chemba na kutoa machozi yangu,
nikitoka nje nanawa uso wangu na kuendelea na maisha kama kawaida.
Alipoanza
kulia nilijiwa na shaka mno, hapa inakuwaje? akija mtu akimuona binti huyu
analia si nitaonekana nimemdhulumu kitu, lakiani nikasema namuachia Mungu jambo
hilo.
Alilia
kwa dakika kama tatu hivi, nilimpa maji akanawa. Nikamuuliza kulikoni?
“Ninapokuwa
na jambo moyoni mwangu linaniumiza huwa ninalia, nikimaliza kulia jambo hilo
huwa limetoka moyoni.”
Alisema
binti huyu kutoka Zanzibar.
Nilimuuliza
swali lingine mbona kando ya Mikahawa yenu kuna makambi mengi ya ujenzi huko
hakuna wateja?
Alisikitika
tu akasema kaka kwenye makambi haya hakuna wateja na wala hakuna watu. Mwanzoni
tulitarajia kuwa kuanza kwa ujenzi huu makambi haya yangeongeza wateja lakini
sasa hakuna.
Binti
huyu huku hasira yake ikiwa inapoa ya kupoteza wateja nilimchokoza nikamwambia
sasa si ukawashitakie kwa Mama Samia kuwa makambi hayana watu ili wakija upata
wateja.
Binti
huyu alicheka sana, akasema we waache tu, nitafanya hivyo, umenipa hekima
kubwa.Binti huyu aliondoka na kikapu chake cha chakula kurudi mkahawani.
Mwanakwetu
tangu siku hiyo binti huyu wa Kizanzibari nilipompa hekima ya kuwashitakia
sijamuona tena.
Swali
ni Je amekwenda kushitaki?
Mie
sifahamu.
Nakutakia
siku njema.
0717649257
No comments:
Post a Comment