Habari za Punde

Mhe Harusi asisitiza mashirikiano sehemu ya kazi


 Na Raya Hamad – OMKR                                                      

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman amesema kuwa mashirikiano ya pamoja yanaleta maelewano katika sehemu ya kazi na kukuza uhusiano mwema unaojenga imani na mapenzi baina yao

 Mhe Harusi ameyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na wafanyakazi wa ofisi hio kwenye ukumbi wa mkutano uliopo Migombani na kuwasisitiza kuwa suala la nidhamu na heshima katika kazi ni jambo la msingi huku wakijua kuwa taifa linawategemea

Bi Harusi amesisitiza kuwa mashirikiano ya wenyewe kwa wenyewe yanawaleta karibu wafanyakazi na watendaji jambo ambalo linaleta ufanisi katika sehemu za kazi ndipo mipango ya utekelezaji na ujenzi wa taifa inapoendana na kasi ya utendaji

“hakikisheni mnajikita katika majukumu ya kazi na mmoja wenu anapoondoka majukumu hayalali bali kazi iendelee ndio maana nawasisitiza kupendana pia msifanye kazi kwa mazowea badala yake jitahidini kuleta ufanisi ili maendeleo yaweze kupatikana” alisisitiza Mhe Harusi

Aidha Bi Harusi amewakumbusha wafanyakazi kuzingatia muda wa kuingia na kutoka kazini na inapotokea hali ya dharura kutoa taarifa kwani si vyema kunyamza unaweza kupoteza haki zako za msingi mambo ambayo hayana tija kiutendaji

Kuhusu suala la uwajibikaji amewataka wafanyakazi kuhakikisha wanatoa huduma stahiki kwa jamii hivyo kila mfanyakazi afahamu majukumu yake pamoja na kuzingatia suala la utowaji wa huduma kwa walioko nje ya ofisi kuhakikisha wanafikiwa

Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak amemuhakikishia Mhe Waziri kuwa nidhamu na mashirikiano ndio yenye kuleta uhai wa taasisi jambo viongozi wa Ofisi hio wanalisisitiza kwa watendaji na wafanyakazi wote


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.