Habari za Punde

TUWASAIDIE WANANCHI WANUFAIKE KUPITIA UCHUMI WA BULUU - ULEGA

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wataalam na Watendaji wa Serikali wa Mkoa wa Lindi na Mtwara wakati akifungua kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika Mkoani Lindi .

 

Na Mbaraka Kambona, Lindi

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka Wataalam na Watendaji wa Serikali katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kuwahamasisha Wananchi kutumia fursa zilizopo katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi hususan ufugaji wa  Majongoo Bahari, Kaa na Ukulima wa Mwani ili waweze kukuza kipato chao.

Naibu Waziri Ulega alitoa agizo hilo jana katika kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika Mkoani Lindi.

"Uchumi wa buluu ni moja ya vipaumbele vya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya Sita, lakini namna gani tumetumia fursa hizo kulingana na uhitaji wa soko ili kuwainua watu katika uchumi wao na Taifa letu ndio kazi yetu sisi wataalam tuliopo hapa", alisema  Ulega

Alisema kuwa wataalam hao kuanzia Maafisa Ardhi, Maafisa Maendeleo na Ushirika, Maafisa Uvuvi na Maafisa Biashara wakishirikiana vyema watakuwa na mchango mkubwa katika kuwainua watu kiuchumi kupitia Rasilimali Bahari.

Aliongeza kwa kusema kuwa uchumi wa buluu una fursa kubwa ya biashara, hivyo ni lazima maafisa hao waweze kuwasaidia wananchi kuwaonesha fursa zinazopatikana humo ili waweze kuzalisha kwa wingi na kupelekea katika masoko makubwa na kukuza kipato chao.

Aidha, aliwataka wataalam hao kujipanga vyema na kwenda kuwajengea uwezo na kuwahamasisha Wananchi kutumia fursa hizo huku akifafanua kuwa wananchi wachache wakielewa fursa hizo kutashawishi watu wengi zaidi kuingia katika shughuli hizo.

"Ninaamini sisi Wataalam tukiwa na utayari wa kuwasaidia hawa wananchi kutumia fursa hizi vizuri basi tutaweza kuwaondoa katika hali ya uduni na wakawa na kipato cha uhakika", alisisitiza

Kuhusu mikakati ya Serikali kukuza Sekta ya Uvuvi ukanda wa kusini, Mhe. Ulega alisema katika Wilaya ya Kilwa Masoko panajengwa bandari kubwa ya Uvuvi itakayotoa fursa nyingi za kujiongezea kipato wananchi  lakini fursa hizo zote ili ziweze kuwa na tija ni muhimu timu ya wataalam hao ikapanga na kuwa na dhamira ya dhati ya kusaidia wananchi kunufaika na fursa hizo.

"Kwa kuanzia ni lazima muunde vikundi vya ushirika ambavyo vitakuwa na watu walio tayari ili Serikali itakapoleta pesa za kuwasaidia ikute vikundi hivyo vipo tayari", alifafanua

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.