Habari za Punde

Kuhakikisha Vijana wanapata Elimu bora.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Sulumein Abdulla akimkabidhi Cheti mwanafunzi Mudrik Salum ambae ni mwanafunzi bora wa mwaka wa kidato cha sita Skuli ya fedha katika mahafali ya sita ya skuli hiyo yaliyofanyika kisauni wilaya ya magharibi B.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Abdulla Suleiman akihutubia katika mahafali ya sita ya kidato cha sita ya skuli ya feza zanzibar yaliyofanyika kisauni wilaya ya magharibi B ambapo aliwaasa wanafunzi kuendelea kuwa na maadili mema wanapokuwa katika jamii.

Na.Abdulrahim Khamis. 

Serikali ya Mapinduzi ya itaendelea kuthamini mchango wa Skuli Binafsi katika kuhakikisha Vijana wanapata Elimu bora ambayo itazalisha wataalamu wa kulisimamia Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo katika Mahafali ya Sita  ya Wanafunzi wa Kidato cha Sita ya Skuli ya Feza Zanzibar yaliyofanyika Kisauni Wilaya ya Magharibi ‘’B’’.

Amesema Sera ya Elimu ya Mwaka 2006 inaeleza kuthamini Sekta Binafsi katika kutoa Elimu ambapo mategemeo ya Serikali na Taifa kupata wataalamu mbali mbali kupitia Skuli za Serikali na Binafsi.

Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Skuli ya Feza kuwa ni mfano kwa  kujitolea katika kuwafinyanga watoto na kuibua vipaji walivyokuwa navyo na kuwahakikishia Serikali itaendelea kuthamini juhudi hizo.

"Kwa dhati kabisa naupongeza Uongozi wa Skuli ya Feza kwa kuwa Taasisi ya mfano na ya kipekee katika kutoa Elimu Bora kwa miaka mingi hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla"Amesema Mhe. Hemed

Aidha Mhe. Hemed ameeleza faraja yake kuona ufaulu mzuri wa Wanafunzi ambao unapelekea kupata fursa mbali mbali za kujiunga na Vyuo Vikuu mbali mbali vyandani na nje ya Nchi.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali imekuwa ikifurahishwa kuona Taasisi Binafsi zinajitolea kwa kuifikia Jamii katika kuunga mkono Miradi mbali mbali ambapo amefarijika kuona Uongozi Feza School umeweza kuchimba Visima Ishirini (20) vya kisasa katika Skuli za Serikali kwa Mwaka 2020-2021 pamoja na udhamini wa wanafunzi Mia Nne (400) wanaosoma Skuli za Serikali.

"Nimearifiwa kuwa Uongozi wa Feza Schools umeanzisha miradi mbali mbali inayolenga Jamii moja kwa moja kila mwaka Skuli hii hutoa Udhamini kwa ujumla ya Wanafunzi Mia Nne (400) wanaosoma Katika Skuli za Serikali ikiwa ni pamoja na Zanzibar, kwa kuwapa Shilingi Laki Mbili na Hamsini (250,000/=) kwa kila Mwanafunzi ili ziweze kutumika kwa kuwalipia Sare na vifaa vyote vya Skuli pamoja na fedha za Mfukoni. Hongereni sana" Mhe. Hemed

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wazazi na walezi kuendelea kutoa mashirikiano kwa walimu kwa kufatilia watoto wao ili kujua mwenendo wa watoto wao.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwaasa wahitimu hao kuwa mstari wa mbele katika kuwasikiliza na kuwatii wazazi wao pamoja na kuthamini juhudi za walimu waliojitahidi katika makuzi yao.

Aidha amewataka kutambua kuwa jamii inathamini mwenye Elimu kwa ujuzi wao pamoja na Nidhamu bora na kuwataka kutumia elimu zao kujenga jamii iliyobora.

Aidha Mhe. Hemed amewataka wahitimu hao kujiepusha na makundi maovu akitolea Mfano Udhalilishaji na utumiaji wa Madawa ya Kulevya ambayo yanapelekea kuporomosha maadili ya Zanzibar na kuwa mabalozi kwa Vijana wenzao kujiepusha na makundi hayo maovu.

" Hatutaweza kufanikiwa bila nidhamu haipendezi muhitimu wa Feza School na Skuli Nyengine akitoka Skuli hana nidhamu suruali Makalioni, Nywele mikato ya ajabu, na wengine kujihusisha na madawa ya kulevya kuweni na nidhamu mujenge heshima na nidhamu ya Nchi yetu Taifa linahitaji wataalamu mfano wenu" Mhe. Hemed

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amewataka wahitimu hao kuwa mabalozi katika Jamii kwa kuhamasisha suala la Sensa ya watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti mwaka huu.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa ameeleza kuwa Skuli ya Feza ni miongoni mwa Skuli zinazofanya vizuri Nchini jambo ambalo linasaidia kupata wasomi wazuri wanaotegemewa na Taifa.

Aidha Mhe. Lela ameeleza kuwa Sekta ya Elimu inakabiliwa na Changamoto nyingi ambapo Skuli hiyo imekuwa mstari wa mbele kukabiliana nazo kwa lengo la kupata wataalamu bora wenye nidhamu, maadili na Uzalendo

Akisoma risala ya wahitimu mwanafunzi Mudrik Salum ameushukuru wa Skuli pamoja na walimu kwa mashirikiano na wazazi kwa kuwajenga kifikra na kitaaluma ambapo wamewahakikishia kuendeleza mema yote waliyofunzwa wakiwa skulini hapo.

Akitoa Shukurani kwa Niaba ya Wazazi wa wanafunzi waliohitimu Bi Amria Masoud Ali amewashukuru Walimu wa Skuli hiyo kwa kuwasimamia watoto wao katika Taaluma na  malezi na kueleza imani yake kuwa wahitimu hao watakuwa kioo kwa Jamii pamoja na kuwa Taifa bora lijalo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.