Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Azindua Chanjo ya Polio ya Matone Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa Kampeni ya kutoa Chanjo ya Matone ya Polio Kitaifa iliyofanyika katika Viwanja vya Mkokotoni Sokoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimpatia Chanjo ya Matone ya Polio Mtoto Pili Juma Suleiman ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa zoezi hilo lililofanyika Viwanja vya Mkokotoni Sokoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Na.Abdulrahim Khamis

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mkakati muafaka wa kupunguza watu wasio na kinga ili kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa wa Polio Nchini.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa Chanjo ya matone ya Pilio iliyofanyika katika Viwanja vya Mkokotoni Sokoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itafanya Zoezi hilo kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa kuwafikia walengwa waliokusudiwa.

 

Mhe. Hemed amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika jitihada inazozichukua hasa kwa zoezi hilo na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo hiyo kwa lengo la kuwakinga na maradhi ya mripuko.

 

Aidha Mhe. Hemed amewatoa wasi wasi juu ya usalama wa chanjo hiyo na kueleza kuwa mashirika ya Afya Duniani pamoja na Wataalamu wa Wizara ya Afya wamethibitisha usalama wake.

 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufuatilia uwepo wa magonjwa ya miripuko yakiwemo yanayozuilika kwa chanjo kama vile Surua, Rubella na Polio na kueleza kuwa Serikali baada ya kupata Tetesi za uwepo wa magonjwa hayo kwa Nchi jirani inachukua tahadhari za haraka ili kudhibiti magonjwa hayo yasiingie Nchini.

 

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya kuendelea kufanya tathmini ya hatari ya ugonjwa wa Polio katika Mikoa yote ya Zanzibar pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa wote wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa Polio Nchini.

 

Aidha Mhe. Hemed ameushukuru na kuupongeza  Uongozi wa Wizara ya Afya, Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ pamoja wadau wa maendeleo kwa kusimamia maandalizi ya  zoezi hilo kikamilifu.

 

Kwa upande wake Waziri ya Afya Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameeleza kuwa miongoni mwa mikakati ya Wizara ni kuhakikisha Zanzibar inasalimika na Maradhi mbali mbali ikiwemo ya Mripuko ambapo juhudi walizochukua ni pamoja na kutoa elimu ya kinga kwa kushirikiana na mashirika ya maendeleo ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la kuhudumia watoto duniani (UNISEF).

 

Aidha Mhe. Mazrui amewataka wananchi kuchukua jitihada kwa kuweka mazingira safi katika maeneo wanayoishi pamoja na ujenzi wa vyoo katika majumba yao wanayoishi na kueleza kuwa Serikali inaendelea na juhudi zake ili kuhakikisha huduma ya maji safi na Salama inapatikana kila eneo.

 

Nae Muwakilishi wa Shirika la Afya Duniani anaefanya kazi zake Zanzibar Dr Ande Michael ameeleza kuwa WHO itaendelea kuunga Mkono juhudi za Serikali ikiwemo kupambana na maradhi mbali mbali yakiwemo Polio.

 

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Muhamed Mahmoud ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja imejipanga vyema kusimamia zoezi hilo kwa kuwafikia wananchi wote na kuhakikisha watoto wote wa mkoa  huo wanapata chanjo hiyo.

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais

19/05/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.