Habari za Punde

Menejimenti ya Wizara ya Ardhi Maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Wizara Mtumba Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Amosy Zephania akizungumza wakati timu ya Menejimenti ya Wizara ilipokagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Wizara katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma Mei 17, 2022.

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Timu ya Menejiment ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la Wizara unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma.

Ujenzi wa jengo hilo la ghorofa sita ulioanza Desemba 2021 unatarajia kuchukua muda wa miezi 18 na unafanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Ujumbe wa Menejimenti ya Wizara Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukioongozwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara Amosy Zephania Mei 17, 2022 ulitembelea maeneo ya ujenzi wa jengo hilo na kupata maelezo kuhusiana na ujenzi huo.

Mhandisi wa ujenzi wa jengo hilo Grace Musita alisema, ujenzi wa jengo hilo la Wizara ya Ardhi alioueleza kuwa umegawanyika sehemu tatu unaendelea vizuri na mwishoni mwa mwezi Mei 2022 wanatarajia kumwaga silabu kwenye sehemu ya kwanza.

‘’Ujenzi wa jengo unaendelea vizuri na changamoto kubwa ilikuwa ujenzi wa  sehemu ya chini ambayo tumeshaimaliza na mwishoni mwa mwezi huu wa tano tunatarajia kumwaga silabu kwenye sehemu ya kwanza ya jengo’’ alisema Grace.

Uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi za ghorofa za Wizara eneo la Mtumba awamu ya pili ulifanywa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa wiki ya maadhimisho ya miaka 60 tangu Tanzania ipate uhuru.

‘’Tunataka mji huu wa Serikali uwe rafiki, unaovutia na mabao tunaweza kuusemea popote na ndiyo maana ujenzi wa miundo mbinu yote muhimu unaendelea kwa kasi ukiwemo wa barabara, maji pamoja na umeme‘’ Mhe Majaliwa alifafanua wakati wa uzinduzi awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi hizo.

Rais Samia Suluhu Hassan aliidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 300 kwa ajili ya kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu na majengo ya ghorofa yatakayotumiwa na wizara mbailmbali katika mji wa serikali Mtumba.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Mji wa Serikali ilikamilika April 2019 na kuwezesha Wizara na Taasisi mbalimbali kuhamisha ofisi zake mkoani Dodoma.

Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha akishuka ngazi wakati timu ya Menejimenti ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilipokagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Wizara unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Michael Luena (Kulia) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Ardhi Amosy Zephania (kushoto) wakati timu ya Menejimenti ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilipokagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Wizara linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Mji wa Serikali Mtumba  Dodoma
Timu ya Menejimenti ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiwa katika picha ya pamoja wakati ilipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Wizara unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma
Muonekano wa ujenzi wa jengo la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.