Habari za Punde

Mti wa Matambiko.

 

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Nikiwa Wilayani Lushoto kati ya mwaka 2016-2018 Rais wa Awamu ya tatu Benjamin Mkapa alikuwa na makaazi yake ambayo yalikuwa nje kidogo na mji huu kama unakwenda Mlola. Eneo la makaazi ya Mzee Mkapa palikuwa na bonde zuri kwa kilimo cha bustani.

Kama yalivyo maeneo mengi ya wilaya ya Lushoto wanalima sana mabondeni mbogamboga kama kambichi, viazi mviringo, karoti, nyanya, vitunguu, pilipili hoho, nyanya chungu, bamia, bilinganya, maharage mabichi na hata brukolini.

Nakumbuka hata hii brukolini nilikuwa siifahamu mie mtoto Mbagala, kufika Lushoto nilitambua maana ilikuwa inasafirisha hadi Ujerumani na inaipatia Halmashauri ya Lushoto pesa nzuri. Hata msaada ya ujenzi wa sehemu yenye majokofu ya kuhifadhia mbogamboga hizo Lushoto walijengewa kwa mkopo.

Kilimo cha bustani cha Lushoto kinashangaza maana kinafanyika mno kipindi cha kiangazi tu. Kipindi cha masika inakuwa ngumu kuyadhibiti maji na mafuriko yanayosomba mbegu na mazao milimani na mabondeni.

Mzee Mkapa kwake palikuwa panalimwa sana na alikuwa analitumia vizuri bonde hilo mithili na yeye alikuwa mzaliwa wa Lushoto.Kwa hiyo bonde hilo walilima viazi na mboga mboga zingine. Huku wakivuna, zinapakiwa katika mafuso na kusafirishwa kwenda Dar es Salaam au Arusha.

Wakifika pale geti la Halmashauri ya Lushoto-Nyasa, viroba vinahesabiwa kimoja baada ya kingine wanalipa na kuondoka zao kwa amani kabisa.

Unaweza kutambua kuwa ni viazi vilivyolimwa mbele ya nyumba ya Mzee Mkapa kama mtendaji wa kata husika alipita katika hilo na akavihesabu wakalipa ushuru na kuwapa lisiti. Mafuso hayo yakipita Nyasa wanakaguliwa ndiyo utatambua hii lisiti nambari kadhaa wa kadhaa ni ya kata ambapo makaazi ya Mzee Mkaapa yao.

“Shamba gani hili mmepata viazi vingi hivi?”

Shamba mbele na makaazi ya Mzee Mkapa wanajibu madereva wa fuso. Hii inasaidia kujua hata uzalishaji wa kila kata wa mazao.

Mzee Mkapa alikuwa anafika kwenye makaazi yake, muda mwingine yupo mwenyewe, muda mwingine anakuja na mama Anna Mkapa

Mara zote kiongozi mkubwa kama yeye anapofika kwenye wilaya kwa utaratibu anapokelewa kwa heshima zote na viongozi wa wilaya hasa hasa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na waalikwa wa kamati hiyo ambao ni Afisa TAKUKURU na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika pia hata CCM wenye serikalia yao anakuwepo mwenyekiti wa wilaya na  katibu wake.

Anapokuja kiongozi aliyeshika nyadhifa kubwa, ukiwa mongoni mwa niliowataja hapo juu lazima ujitahidi sana unakuwepo. Hapo anaweza kuuliza au kupatiwa ripoti ripoti ya hali ya wilaya ilivyo. Akiwa nyumbani kwake anaweza kumtembelea mzee mwenzake au wazee wenzake wanaweza kwenda kumtembelea.

Kama umebahatika kukaa jirani na wazee wengi kama huyu huwa ni wakweli na hawapendi kuficha jambo. Huwa hawapendi mtu aharibiwe kupitia mkono au kauli yake.

Kuna siku alikuja Mzee Mkapa akapokelewa vizuri, mimi na wezangu tukashiriki karibu sana, tukajipanga foleni akianza mkuu wa wilaya na katibu tawala na siye wengine wa mwisho mwisho.

Mzee alipofika tukamsalimia kwa kumpa mikono na shikamoo yake na tukaingia hadi sebuleni kwake. Kwa umri ambaye kidogo alikuwa analingana na Mzee Mkapa nadhani alikuwa mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Lushoto wakati huo Balozi Mstaafu Abdi Mshangama (mzee mmoja mrefu mweupe) sidhani yeye kama shikamoo ilimtoka nadhani wanalingana.

Tukiwa tunaingia sebuleni kwake.Mzee Mkapa akasema.

“Mkurugenzi Kazimbaya upo? Nikajibu nipo shikamoo.”

Mzee Mkapa akajibu marahaba huku akicheka.

“Kwanini umeukata mti wa matambiko?” Akasema kwa kunong’ona.

“Nikajibu kweli tulitaka kuukata maana ulikuwa unaharibu nyumba ya serikali. Katibu Tawala wa Mkoa Injinia Zena Said aliwasiliana na sisi tukawa tumeupunguza matawi tu, lakini tumesitisha zoezi hilo mheshimiwa.”

“Unataka shemeji zako wakatambike wapi?”

Watu wengine tuliombatana nao wakawa wanacheka.Hapo tupo sebuleni nyumbani kwa Mzee Mkapa-Lushoto, viongozi wetu wakubwa wanajianda kumsomea taarifa ya wilaya.

“Jamani mimi nimechoka sana, sasa naombeni mniache nikapumzike.”

Mzee Mkapa akasema. Basi kila mmoja wetu tukatoka ndani na kuwasha magari yetu na kurudi nyumbani maana ilikuwa siku ya mapumziko.

Jambo hilo lilinipa tafakari mno na Mzee Mkapa wilayani Lushoto alikuwa na marafiki zake wakubwa watatu, wa kwanza Brigedia Hassan Ngwilizi,wa pili ni Diwani Lukozi wa wakati huo Marehemu Karim Mahanyu na wa tatu ni Baba Askofu Mstaafu Stephern Munga wa Dayosisi ya Kiinjili ya Kilutheri ya Kaskazini Mashariki..

Wakati huo Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania alikuwa John Pombe Magufuli na Jamii ya Watanzania walikuwa wakiamini kuwa aliyekuwa anamuweza Magufuli vizuri ni Mkapa.

Nikasema moyoni kama zengwe la Mti wa Matambiko lipo kwa Mkapa maana yake Magufuli analo, sikuwa na amani siku hiyo nikawa najua kuwa hapo siku za kutumbulia zinahesabika tu, lakini je ukweli unajulikana?

Nikajiuliza jambo hili kwa kina na namna kuweza kulipata vizuri, nikasema hawa rafiki zake watatu mmoja kati hao lazima atakuwa na jibu. Basi nikamfuata Karim Mahanyu alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Uongozi na Fedha ya Halmshauri hii pia alikuw akiumri hajazinidi sana, nikajua tu tutaelewana tu.

“Kweli kuna wazee wa kimila walikwenda kwa mzee wanalalamikia kuwa mti wao wa kutambika umekatwa.”

Nikamuuliza mzee akasemaje? “Mzee akauliza vyombo, walipompa jibu akaliachia hapo hapo.”

Akaniuliza kwani kumetokea nini? Nikamueleza Karim Mahayu vile alivyoniambia Mzee Mkapa siku tuliyompokea na simu ya Injini Zena Said Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga wakati huo.

Karim Mahanyu alikuwa mtu mmoja siyo msemaji, mkimya mno na alikuwa ndiyo mara nyingi viazi vikivumwa katika makaazi ya Mzee Mkapa anasimamia zoezi hilo mwanzo mwisho.

Nikasema sasa mheshimiwa,mbona pale pana ua wa wavu, geti la chuma na mlinzi mwenye bunduki mchana na usiku?Mnatambika muda gani?

Pale tunaokoa jengo na mabati yanaoza kutokana na matawi na majani ya mti ule.

Mheshimiwa karim Mahanyu akasema.

“Hayo mambo, wewe achana nayo, ili mradi mti upo. Muda wetu wa kutambika tunaujua wenyewe.”

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.