Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amemuapisha Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali na Naibu Kadhi Mkuu Sheikh.Othman Ame Chum Ikulu leo.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Sheikh Hassan Othman Ngwali kuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar, hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 12-5-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Sheikh Othman Ame Chum kuwa Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, hafla hiyo ya kuapishwa iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 12-5-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha Kadhi Mkuu wa Zanzibar  Sheikh Hassan Othman Ngwali pamoja na Naibu Kadhi Mkuu Sheikh Othman Ame Chum, kufuatia uteuzi  aliofanya kwa watendaji hao mnamo Mei 5, mwaka huu.  

Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu, jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla.

Wengine waliohudhuria, ni pamoja na Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zena Ahmeid Said, Mawaziri, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini pamoja na Wanafamilia.

Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya hafla hiyo kumalizika, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, aliwataka wananchi kujenga mashirikiano na Mahakama ya kadhi ili kuiwezesha kufikia utoaji wa maamuzi ya haki.

Alisema Mahakama ya  Kadhi haihusiki na maamuzi ya utoaji talaka, na hivyo kusababisha matukio mengi ya talaka nchini, na kubainisha kuwa ` kwa kiasi kikubwa imejikita katika jukumu la kufanya suluhu kati ya wanandoa  wanapohitilafiana na pale inaposhindikana ndipo huamuru utoaji wa talaka.

Aidha, alisema Mahakama hiyo imejipanga kuendeleza darsa maalum ili   kutoa taaluma, ikiwa ni hatua ya kudumisha ndoa na hivyo akasisitiza umuhimu wa wananchi wenye nia ya kufunga ndoa kupata mafunzo hayo kabla ya kufunga ndoa.

“Wanapopata mafunzo ya ndoa inakuwa wepesi kwao kutatua migogoro inapojitokeza”, alisema.

Nae, Naibu Kadhi Mkuu Sheikh Othman Ame Chum alisema  matokeo ghasi ya utoaji wa talaka kwa wanandoa husababisha kusambaratika kwa familia na watoto kukosa malezi bora ya baba na mama.

Alitoa wito kwa kuitaka jamii kurudi katika maadili mema na malezi ya zamani ili kuepuka kusambaratika kwa familia.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.