Habari za Punde

Uwasilishwaji wa Mabadiliko ya Mtaala wa Elimu ya Maandalizi na Msingi Zoezi Lililowashirikisha Kamati za Skuli Maandalizi,Msingi na Viongozi.


Mabadiliko ya mtaala wa kufundishia Skuli za maandalizi na Msingi yamezingatia stadi, maarifa na mwelekeo ili mwanafunzi apate ujuzi katika suala zima la kujifunza.

Hayo yameelezwa na mwezeshaji ambae pia ni Mkuu wa mafunzo ya Mitaala Taasisi ya Elimu Zanzibar; Bibi Hafsa Aboud Talib katika zoezi la kuwasilisha mabadiliko ya mtaala wa elimu ya maandalizi na msingi lililoshirikisha kamati za skuli za maandalizi na msingi,viongozi wa dini, masheha,  wazazi na wadau wengine wa elimu katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Dr. Shein iliyopo Wingwi Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Bi Hafsa amesema zipo sababu mbali mbali zinazopelekea kubadilika kwa Mtaala  zikiwemo mahitaji yaliyopo katika nchi husika na kukamilika kwa kipindi cha kutumika mtaala huo. Hivyo, suala la  malalamiko ya wazazi kuhusu idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa elimu ya Maandalizi na Msingi ni miongoni mwa sababu zilizopelekea mabadiliko hayo.

Bi Hafsa amesema, kufuatia mabadiliko hayo wanafunzi wa Madarasa ya Elimu ya Maandalizi watasoma vitendo 6 vya kujifunza badala ya masomo 8, wanafunzi wa Elimu ya Msingi wa awali watasoma masomo 6 badala ya 8 na Msingi juu watasoma masomo nane (8) badala ya masomo kumi na mbili (12) yanayofundishwa kabla ya mabadiliko hayo.
Akifafanua Idadi hiyo ya masomo Bi Hafsa amesema wanafunzi wa Msingi juu ( kuanzia darasa la 5 hadi la 6) hivi sasa wanasoma masomo ya Kiswahili, Dini, Kiingereza, Kiarabu, Geography, Math, Sayansi, ICT, Historia, Uraia, Elimu Amali na Michezo.
Amesema kufuatia mabadiliko ya mtaala uliozingatia umahiri( competence) badala ya masomo hayo 12 kwa msingi wa juu ambao kwa mtaala mpya ni kuanzia darasa la 4 hadi darasa la 7, masomo yatakayofundishwa  ni Kiswahili, Kiingereza, Sanaa za Ubunifu na Michezo, Dini, Kiarabu, Math, Science and Technology na  Sayansi Jamii.

Kwa upande wake Mratibu wa Taasisi ya Elimu Pemba Bi Asha Soud Nassor amesema; Kufuatia mabadiliko ya mtaala walimu watapatiwa mafunzo ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Aidha, Bi Asha amesema matarajio ya Taasisi ni kukamilisha mchakato wa maandalizi ya mtaala huo hadi ifikapo December mwaka huu wa 2022 ili ifikapo January mwaka 2023, mtaala mpya uweze kutumika rasmi.

Nae, ndugu Khamis Rashid Ali ambae ni miongoni mwa  wenyeviti wa kamati za skuli walioshiriki zoezi hilo wamempongeza sana muwezeshaji kwa umahiri alionao juu ya uwasilishaji wa dhana ya elimu ya mtaala kwa kuhakikisha washiriki wote wamepata uelewa juu ya dhana ya mtaala na mabadiliko yake. Wameelezea matumaini yao juu ya ubora wa mtaala huo kutokana na kuzingatia malalamiko mbalimbali ya wanajamii kuhusu mtaala uliyopo sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.