Habari za Punde

Milango iko wazi kupatikana kwa Sheria mpya ya habari Z’bar

Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wakifanya mazoezi ya kunyoosha viungo kwa ajili ya kujiweka sawa kuendelea na majadiliano.
Mkufunzi wa maswala ya habari Zanzibar Bi Hawra Shamte akiwasilicha mapendekezo ya wadau kuhusu changamoto za sheria ya habari.
Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa akisistiza jambo wakati wa mkutano huo kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa sheria mpya ya habari.

Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ

Katibu wa Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar Mussa Kombo Bakari amesema tume hiyo ipo itayari kushirikiana kwa karibu na wadau wa habari Zanzibar ili kupatikana kwa sheria bora ya habari inayoendana na wakati uliopo sasa.


Kauli ya katibu huyo imekuja kufuatia mkutano maalumu ulioandaliwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na shirika la Internews Tanzania wenye lengo la kuongeza ushawishi wa upatikanaji wa sheria mpya ya habari visiwani hapa sambamba na kuonesha changamoto zilizo kwenye sheria ya habari inayoendelea kutumiwa ya mwaka 1988.


Alisema kulingana na wakati ulipo  kuna kila sababu ya wadau hao kukaa pamoja na kuziorodhesha changamoto ndani ya sheria hiyo kwa lengo la kupatikana kwa sheria mpya ambayo itakwendana na mazingira halisi.


Sambamba na hayo katibu huyo alisema wao kama tume ya kurekebisha sheria visiwani hapa watahakikisha wanafanya upembuzi wa kina kila kila kipengele ambacho kimewasilishwa na wadau kama changamoto ili waweze kupata kitu ambacho kitakua bora zaidi kwenye sheria mpya.


Awali akiwasilisha baadhi ya changamoto ndani ya sheria hiyo mkufunzi wa maswala ya habari visiwani hapa Bi Hawra Shamte alisema sheria ya habari inayoendelea kutumiwa ni sheria ambayo imekua ikikandamiza uhuru wa yombo vya habari kwa miaka mingi.


Akitolea mfano miongoni mwa vipengele kwenye sheria hiyo alisema  “Kifungu cha 27(1) Afisa polisi yeyote anaweza kukamata gazeti lolote, popote linapopatikana, ambalo limechapishwa au ambalo anashuku kuwa limechapishwa, kinyume na sheria. “


Kupitia mfano huu mkufunzi alisema kipengele hicho kinatoa mamlaka makubwa kwa Afisa wa jeshi la polisi asiekua maalumu kukamata na kuzia usambazwa wa gazeti.

Alisema katika zama zilizopo sasa kuendelea kumpa mamlaka Afisa polisi kuzuia gazeti au taarifa ni kukiuka pia haki ya kikatiba hivyo iwapo kutakuwa na kosa vyombo vya habari vilipaswa kuwajibishwa kupitia bodi maalumu ambayo nayo pia inapaswa iwe huru.


Sambamba na hilo pia alisema kupitia sheria hiyo hiyo pia imempa mamlaka makubwa waziri wa habari Zanzibar kufungia chombo chochote cha habari atakapoona kuwa kinakwenda kinyume na kisha kutoa taarifa za kukifungia chombo hicho kwa siku 14.


Kifungu cha 30 (i) Endapo Waziri anaona kuwa ni kwa manufaa ya umma au kwa maslahi ya amani na utulivu, anaweza kuamuru kufungiwa kwa gazeti... na gazeti hilo litakoma kuchapishwa kuanzia tarehe iliyotajwa. ” alifafanua.


Akiedelea kufafanua kuhusu hoja hii alisema mamlaka anayopewa waziri ni makubwa sana ambayo asingepeswa kabisa kupewa uwezo wa kukifungia chombo cha habari ukizingatia mawaziri wengi si wanataaluma halisi hivyo inaweza kutokea jambo ambalo anahisi yeye ni kosa lakini ukitazama kiuhalisia halikua kosa ambalo adhabu yake iwe ni kufungiwa kwa chombo.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa alisema licha ya madai sheria mpya ya habari kudaiwa kwa miaka mingi lakini anaamini kwa wakati ulipo sasa madai hayo yanakwenda kufikia malengo yake.


Alisema jamii na Serikali kwa ujumla wanapaswa kufahamu kuwepo kwa sheria mpya ya habari kutaongeza usawa na uwajibikaji katika kila jambo na kupelekea kuchochea watu kuwajibika hivyo kuwa sehemu ya chanzo kikubwa cha maendeleo ndani ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.