Habari za Punde

Watu Wenye Ulemavu Iringa wataka Elimu Jumuishi.

Makamu Mwenyekiti Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) mkoa wa Iringa Leo Sambala akiongea wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali uliondaliwa na shirika lisilo la kiserikali la IDYDC na kufadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali linalotekeleza mradi wa Inclusive Media Project unaofadhiliwa na Internews Tanzania
Moja ya washiriki wa mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali uliondaliwa na shirika lisilo la kiserikali la IDYDC na kufadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali linalotekeleza mradi wa Inclusive Media Project unaofadhiliwa na Internews Tanzania akichangia mada wakati wa mkutano huo
Picha ya pamoja ya washiriki wa Mkutano huo.

Na Fredy Mgunda,Iringa.

CHAMA cha watu wenye ulemavu Tanzania (CHAWATA) mkoa wa Iringa wameiomba serikali kuweka mfumo wa elimu jumuishi kwa walemavu ili kutatua changamoto ambazo wanazokabiliana licha kuwa bado kunachangamoto kubwa ya miundombinu ya elimu hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali uliondaliwa na shirika lisilo la kiserikali la IDYDC na kufadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali linalotekeleza mradi wa Inclusive Media Project unaofadhiliwa na Internews Tanzania  katika mkoa wa Iringa, Makamu Mwenyekiti Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) mkoa wa Iringa, Rukia Makweta alisema kuwa watoto wenye mahitaji maalumu kuchanganyikana na wengine inatengeneza umoja na kuondoa unyanyapaa kwa kuwa tayari wamezoeana na kupendana pamoja na kupewa ushirikiano kutoka kwa wenzao..

Makweta alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria namba tisa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010, inataka haki sawa kwa watu wenye ulemavu ikiwamo elimu, ajira, nafasi za uongozi na kuboresha miundombinu na kwa mujibu wa jarida ya Shirika la Kuhudumia watoto Duniani (Unicef), kati ya watoto watano ni wawili tu wapo shuleni hali ambayo inahitaji elimu jumuishi kuwavutia wengi zaidi.

Aliongeza kuwa katika suala la elimu walemavu wengi wanakabiliana na miundombinu isiyo rafiki ambayo ni kikwazo katika upataji wa elimu kwa walemavu waliowengi nchini.

Mmoja ya wanafunzi wenye ulemavu wa kuona, Kephason alisema shule jumuishi anayosoma bado ina changamoto za kimiundombinu  na kupelekea kuwa na ugumu kutoka sehemu moja hadi nyingine awapo kwenye  mazingira ya shule na kupelekea kukosa ari ya kuendelea na masomo kama wanafunzi wengine na kuitaka serikali kufanya jitihada madhubuti kurekebisha hili kwani kwa mwenendo huu wanafunzi wengi wenye ulemavu wanaamua kuacha shule ili kuepukana na changamoto za kimiundombinu wanazokutana nzao mashuleni kwani huwaathiri kisaikolojia pia.

“Elimu jumuishi imepewa kipaumbele zaidi kuliko aina nyinginena inachukuliwa kama njia bora” alisema.

Aidha Makweta alisema kuwa sehemu kubwa ya jamii nchini imeendelea kukumbatia utamaduni wa kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu kwa madai mbalimbali ikiwamo ya kuhofia aibu au kuwaona hawatakuwa na uwezo wa kushiriki shughuli za kijamii ikiwamo elimu.

Naye Katibu wa Shirika la watu wenye Ulemavu, (SHIVYAWATA), Leo Sambala alisema kuwa moja ya changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni miundo mbinu isiyo rafiki kwenye shule nyingi za msingi na sekondari ni kati ya vikwazo vinavyoikabili elimu hiyo mkoani hapo  na kuongeza kuwa kama suala la miundombinu halitapewa uzito, watoto hao watashindwa kujifunza ipasavyo.

“Ni kweli shule zetu zinakabiliwa na miundombinu isiyo rafiki, hakuna vifaa vya kujifunzia hasa kwa walemavu wasioona, hapa hakuna kujifunza kwani walemavu wa kutoona wanahitaji vifaa maalum ambavyo sio kila shule inavyo, kwa hiyo huyu hatajifunza kama ataingia darasani na kukosa vifaa hivyo.” Alisema Sambala.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Elimu Jumuishi kutoka shirika lisilo la kiserikali la  Iringa Development of Youth Disabled and Children Care (IDYDC)linalotekeleza mradi wa Inclusive Media Project mkoa wa Iringa na kufadhiliwa na Internews Tanzania  , Reuben Magayane alisema kuwa lengo la mradi ni kutumia vyombo vya habari  kupaza sauti juu ya elimu jumuishi na kuibua maswala ya makundi maalumu na walemavu kupitia vyombo vya habari.

Alisema kuwa jambo ambalo limekuwa halipewi kipaumbele kwenye vyombo vya habari huku ikiiasa jitihada jumuishi kutoka kwa waandishi wa habari,jamii na serikai ili kufikia lengo la elimu kwani Msingi wa mafunzo mbalimbali katika jamii ni chachu ya kuondoa mawazo mgando juu ya watu wenye mahitaji maalumu kuwa hawawezi, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kutoa ushirikiano hitajika kwa watu wenye mahitaji maalumu hasa katika upande wa elimu.

Alisema kuwa katika kikao hicho moja ya changamoto ambayo imejitokeza ni ukosefu wa miundombinu rafiki ya kujifunzia katika shule jumuishi nchini hivyo ni moja ya njia ambazo zinaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wanafunzi na  watu wenye ulemavu.Wilaya ya IringaKwa muda mrefu kumekuwa na kampeni mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu hasa juu ya haki zao za msingi ikiwamo elimu.

Magayane alisema kuwa kumekuwa na kampeni mbalimbali juu ya watu wenye ulemavu kupata miundombinu rafiki lakini bado kilio cha watu wenye ulemavu kupata mahitaji yao muhimu ili waishi kama makundi mengine kwenye jamii hakikomi.

Aliongeza kuwa changamoto lukuki ikiwamo miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wanaoishi na ulemavu, ni moja ya vilio vinavyowafanya baadhi kushindwa kupata elimu na mkoa Iringa ni kati ya mikoa inayokabiliwa na changamoto nyingi katika utoaji wa elimu jumuishi kubwa ikiwa miundombinu isiyo rafiki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.