Habari za Punde

SMZ Kuvipa Zabuni ya Ujenzi Vikosi vya Serikali katika Ujenzi wa Madarasa Kazin Ambayo Wameifanya Vizuri.

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  ameeleza sababu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuvipa zabuni ya ujenzi vikosi vyake vya Serikali katika ujenzi wa madarasa kazi ambayo wameifanya kwa ufanisi mkubwa.  

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa madarasa yaliyojengwa kwa fedha za UVIKO-19, huko Kihinani, Jimbo la Mfenesini, Mkoa wa Mjini Magharibi. Ikiwa ni siku yake ya mwanzo ya ziara yake anayotatajia kuifanya Unguja Na Pemba.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwamba suala la Serikali kutotangaza tenda kwa ujenzi huo ilikuwa na maana kubwa kwani ilitambua viko vikosi vyake ambavyo vina uwezo mkubwa katika ujenzi kikiwemo kikosi hicho cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).

Hivyo, Rais Dk. Mwinyin alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa kikosi hicho kwa hatua zake hizo za ujenzi ikiwa ni pamoja na kupunguza kiasi cha fedha za ujenzi wa madarasa hayo tofauti na Kampuni ambazo zilitaka kila darasa lijengwe kwa TZS milioni 50 na badala yake JKU imejenga kwa TZS milioni 20  kwa kila darasa.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kutokana na hatua hizo za ujenzi wa madarasa hayo itapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi katika madarasa ambapo hapo awali darasa moja lilikuwa likitumika na wanafunzi 200 na badala yake darasa moja litakuwa na watoto sizaidiya 55.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali ina mkakati maalum wa kuongeza kiwango cha elimu na badala ya kukamilika madarasa hatua itakayofuata ni kuongeza idadi ya walimu ambapo Serikali inatarajia kuajiri walimu wapatao 4,000, hivi karibuni.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya kujenga Chuo kipya cha kisasa cha Ualimu  ili walimu waweze kufundisha kwa ufanisi mzuri zaidi kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kwa kuwaahidi vijana wa JKU walioshiriki katika ujenzi huo kwamba mara tu ajira zitakapotangazwa wao ndio watakuwa wa mwanzo kutokana na kazi kubwa waliyoifanya.

Rais Dk. Mwinyi alipokea ombi la Mbunge wa Jimbo hilo la kujengewa barabara mbili za ndani katika ombi ambalo Rais alilipokea na kulikubali na kuahidi kutekelezwa.

Nao viongozi wa Jimbo hilo la Mfenesini walitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake anazozichukua ikiwa ni pamoja na kuwapelekea miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo ikiwemo miradi ya elimu, barabara, maji na mengineyo ambapo Mbunge wa Jimbo hilo Zubeda Khamis Shaibu alitoa ombi la kujengewa barabara zao mbili za ndani.

Nao viongozi mbali mbali wa Serikali walieleza mafanikio hayo yaliyopatikana kwa kupunguza changamoto mbali mbali na kumpongeza Rais kwa juhudi zake anazozichukua.

Nae mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Fatma Mohammed Makame, alitoa maombi yake kadhaa ikiwemo kujengwa kwa skuli ya Sekondari katika eneo hilo pamoja na uzio huku akiahidi kuongeza juhudi katika ufundishaji ili kuongeza ufaulu pamoja na kuitunza.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi aliweka jiwe la msingi katika hospitali mpya ya Wilaya, iliyopo Mbuzini, Wilaya ya Magharibi A, na kusema kwamba kuimarika kwa huduma za afya kunahitaji hospitali za rufaa kama hizo zinazojengwa na Serikali.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba maendeleo ya nchi yanahitaji kwa kiasi kikubwa huduma za afya pamoja na elimu na ndio maana Serikali anayoiongoza imeweka kipaumbe katika sekta hizo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha inafanya kazi ya kuimarisha huduma za jamii.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Amour Suleiman Mohammed alieleza kwamba hospitali hiyo imejengwa kwa fedha za mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo zina lengo la kuhuisha uchumi baada ya janga la UVIKO-19, ambapo ujenzi wake unafanywa na Kampuni ya CRJE kutoka China.

Alieleza kwamba ujenzi wa hospitali hiyo umetengewa TZS Bilioni 3.9 ambapo hadi kufikia sasa jumla ya TZS Bilioni 2.4 zimeshalipwa sawa na asilimia 62 ambapo hii sasa ujenzi huo tayari umeshafikaia asilimia 80 na unahusisha majengo yatakayoweza kutoa huduma tofauti za afya.

Alieleza huduma ambazo zitatolewa katika hospitali hiyo zikiwemo huduma za wagonjwa wa dharura, huduma za wagonjwa mahututi (ICU), huduma za wagonjwa wa ndani zikiwemo wodiza watoto chini ya mwezi mmoja, wodi ya watoto, mama wajawazito, watu wazima wanawake na wanaume, wodi ya wagonjwa wa maradhi ya kuambukiza na huduma nyengiezo.

Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi alipokea ombi la Mwakilishi wa Jimbo la Bububu Mudrik Ramadhan Soraga la kujengwa barabara inayotoka Mndo hadi Kiboje Manzese.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi alitembelea mradi wa uhuishaji na uimarishaji wa mfumo wa maji safi Zanzibar ambao unajenwga na Kampuni Megar Ingeniaring kutoka India ambao thamani wa TZS Bilioni 27.8 utakaosaidia katika vijiji vya Dole, Kizimbani, Sharifumsa, Kizimbani, Bububu pamoja na maeneo mengine ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mradi huo utamaliza sehemu kubwa ya tatizo la maji katika Mkoa wa Mjaini Magharibi ambapo matarajio ifikikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji kwa asilimia kuwba utaongezeka na kusisitiza kwamba mradi huo ni vyema ifikapo Januari unakamilika kwa wakati kama mkaba ulivyoainisha.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alitembea barabara ya Mwera hadi Kibondemzungu ambayo ni ya mfano inayojengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni miongoni mwa baraara za ndani zenye urefu wa kilomita 275.9 zinazojengwa Unguja na Pemba.

Rais Dk. Mwinyi alisema hatua ya Serikiali ya kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami ni kuondokana na changamoto ya ujenzi wa barabara kwa kifusi na hatimae kuharibika wakati wa mvua.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alitoa taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Mkoa huo huko katika ukumbi wa Chuo cha Utalii, Maruhubi na kueleza mafanikio pamoja na changamoto za Mkoa huo.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.