Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi Akabidhiwa Ripoti ya CAG, ZAECA Yatakiwa kujitathmini

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia baada ya kukabidhiwa Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Othman Abass Ali, hafla hiyo iliyofanyika leo 27-8-2022 katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Mamlaka ya Kuuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi  (ZAECA) kujitathmin juu ya utendaji wake, kutokana na kuwepo kwa matukio kadhaa ya Wizi wa mali za Serikali na Uhujumu Uchumi ambapo taasisi hiyo imeshindwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu  Zanzibar, baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoishia mwezi  Juni 30, 2021. 

Amesema ni muhimu kwa taasisi hiyo kujitathmin juu ya utendaji wake wa kazi, kwa kigezo kuwa kumekuwepo kesi nyingi za Wizi wa mali za Serikali na Uhujumu Uchumi, ambapo mbali  na kukabidhiwa kuzishughulikia lakini hakuna mrejesho kwa kipindi kirefu sasa.

Alisema kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya kesi hizo watuhumiwa wamekiri kuhusika na matukio hayo na wengine kukubali kurejesha fedha serikalini, lakini hakuna hatua za kisheria zilizobainishwa kuchukuliwa.

Dk. Mwinyi alitolea mfano wa tukio la Wizi wa fedha lilitokea ZRB kupitia mfumo wa Mtandao, ambalo hadi sasa halijaainishwa hatua zilizochukuliwa na kusema utamaduni huo umefanya vitendo kama hivyo kujirejea mara kwa mara.

“......bado hawajaisaidia serikali kumekuwa na matukio kadhaa kuripotiwa ndnai ya kipindi cha miaka miwili sasa”. Alisema.

Dk. Mwinyi aliagiza hatua thabiti zichukuliwe dhidi ya watu wote watakaohusihwa na matukio ya wizi wa fedha za umma, na kusema kamwe nchi haiwezi kuendelea kwa namna hiyo ikiwa kila mahali kuna matukio ya wizi.

Aliwataka Viongozi wote walioko serikalini kuona ukubwa wa tatizo hilo na kutaka hatua za msingi kuchukuliwa kwa wote waliohusika.

Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ilifanya uamuzi wa kuondoa jukumu la Wizara ya Afya kununua dawa na jukumu hilo kulikabidhi Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, lakini inashangaza Uongozi wa Hospitali hiyo nao unanunua dawa hizo kwa wauzaji wale wale waliokuwa wakichangia upotevu wa fedha nyingi za  Serikali.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa dhati CAG Dk. Othman Abass Ali kwa moyo wa kujitolea na kubainisha kasoro mbali mbali zilioko katika Wizara na taasisi za Serikali.

“Laiti kama kazi inayofanywa na CAG  ingefanywa na vyombo vyengine vinavyohusika, matukio kama haya yasingejirudia”, alisema.

Rais Dk.Mwinyi alisema serikali imepokea taarifa hiyo na ushauri wenye nia ya kupunguza au kuondoa kabisa  matatizo hayo, hivyo akatumia fursa hiyo kumtaka Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmeid Said kuwafikishia watendaji wote wa Wizara na Taasisi za serikali mapendekezo yaliotolewa na CAG.

Mapema, akiwasilish taarifa ya ukaguzi, Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Dk. Othman Abass alitoa mapendekezo mbali mbali, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na wimbi la Wizi wa Fedha  za Serikali pamoja na kasoro zinazopelekea kusababisha upotevu wa fedha za Serikali.

Alisema kuna umuhimu kwa Serikali kuanzisha mfumo wa Uwekaji  zabuni ili kuepuka madeni feki, pamoja na kuishauri Serikali kuvunja mikataba yote ya Ununuzi na Usambazaji wa Dawa na Vifaa tiba  inayotumiwa na Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ili kuokoa fedha nyingi za Serikali zinazoendelea kupotea.

Aliishauri serikali kuanzisha mfumo mpya wa upokeaji dawa na usambazaji wake ili kuepuka kupokea dawa zilizopitwa na muda na zisizofaa kwa matumizi ya Afya Binadamu, jambo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara.

Aidha, Dk. Abass alishauri taasisi zote za Serikali zinazotekeleza miradi ya Maendeleo kufanya upembuzi yakinifu ili kuhakikisha thamani ya fedha inayotumika kufanikisha miradi hiyo inaendana na kazi inayoyofanyika.

Katika Ripoti hiyo Dk. Abass aliwasilisha matukio mbali mbali yaliojiri katika kipindi hicho, huku akibainisha Mabilioni ya Fedha za Serikali  zilivyoibiwa au kupotea kutokana na kasoro za kiutendaji.

Miongoni mwa Wizara ilioelekezwa shutuma nzito ya Wizi wa Fedha  izo ilikuwa ni Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 1.3 zimeibiwa baada ya kutolewa  katika Akaunti ya Wizara na kuelekezwa katika akaunti za makampuni mbali mbali bila ya kazi yoyote kufanyika.

Aidha, aeneo jengine ambalo limenyooshewa kidole kujiri kwa upotevu mkubwa wa fedha za Serikali ilikuwa ni Mashirika ya Umma , ikiwemo Mfuko wa Hifadhi ya JAMII (ZSSF) uliohusishwa  na hatari ya kufilisika kutokana na mwenendo mbaya wa urudishaji mikopo katikamaeneo tofauti, ikiwemo  ujenzi wa majengo, uendeshaji wa miradi kadhaa isioleta tija, km vile uwekezaji  katika Hoteli Pemba pamoja na kuwakopesha wafanyakazi wake bila kuzingatia kanuni.

Vile vile Shirika la Bandari nalo likahusishwa na upotevu wa fedha nyingi za Serikali, ambapo pamoja na kasoro mbali mbali zilizobainika,  limehusishwa na upotevu wa zaidi ya shilingi Milioni 732 kwa kushindwa kukusanya mapato kutokana na uwekaji wa bidhaa, ambapo pale wafanyabiashara wanaposhindwa kutoa bidhaa zao Bandarini, huzunguka na kuzinunua bidhaa hizo kwa kiwango kidogo cha fedha pale zinaponadiwa kwa  na hivyo  kuipotezea serikali mapato.

Idara ya pencheni jamii nayo ni miongoni mwa zilizobainika kuwa na kasoro na upotevu mkubwa wa fedha, kutokana na kushindwa kurejesha Hazina bakaa ya fedha, kuwepo matumizi Hewa ya takriban shilingi Milioni 75 huku kukiwa  hakuna wazee waliolipwa .

Akigusia juu ya Uhakiki wa Mafao ya Viinua Mgongo na Pencheni kwa wastaafu wa Serikali na Mashirika ya umma, Dk.  alisema eneo hilo lina changamoto nyingi, ikiwemo ya kutokuwepo kwa taarifa sahihi za wastaafu pamoja na baadhi ya wastaafu, hususan kutoka Vikosi vya SMZ  kuendelea kulipwa mishahara hata baada kustaafu kazi.

Dk. Abass aliiitaja Wizara Afya kuhusika na uwasilishaji wa madeni feki katika uhakiki wa  Zabuni za Madawa na Vifaa Tiba.

Alisema kuna matukio kadhaa kwa Wizara hiyo kuwasilisha kwake madeni ya kiwango cha juu cha Zabuni lakini pale yanapohakikiwa hubainika kiwango halisi kuwa cha hali ya chini.

Alitolea mfano wa deni la zabuni ya shilingi Bilioni 4.922 lililowasilishwa kwake lakini baada ya kufanya uhakiki ikabainika kuwa deni halali ilikuwa ni shilingi Milioni 886.68.

“Kuwepo kwa deni danganyifu lililoripotiwa Wizara Afya, tulimtaka Mkurugenzi wa Bohari athibitishe kwa maadishi.....baada ya wiki tulisikia amekufa”, alisema.

Mapema, CAG alitoa taarifa kuhusiana na Gawio la serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi kufuatilia gawio hilo ili kupata ufumbuzi.

Alisema amebaini kiasi cha shilingi Bilioni 4.8 hazijapokelewa na serikali kutokana na Gawio hilo ambapo SMZ ilipaswa kupokea shilingi Bilioni 57.6, wakati ambapo fedha zilizotoka ni shilingi Bilioni 52.8.

Akigusia juu ya usimamizi wa Fedha za Muungano kupitia Akaunti ya pamoja ya fedha , Dk. Abassa alibainisha kutokuwepo kwa maoni kutoka serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yangepaswa kuwasilishwa ili yafanyiwe kazi na SMT , hivyo hatua hiyo imemfanya ashindwe kubaini kiwango halisi  cha fedha kilichotumika kufungua Akauni hiyo.  

Katika taarifa hiyo Dk. Abass alibainisha kasoro kadhaa za kiutendaji zilizobainika pamoja na kiwango kikubwa cha upotevu wa Fedha katika Wizara na taasisi za Serikali pamoja na Vikosi vya SMZ ikiwemo JKU, Mafunzo, KMKM, Zimamoto pamoja na Kikosi cha Valantia.

Aidha, aliorodhesha miradi kadhaa ya Maendeleo iliobanika kuwa na Dosari, ikiwemo kufanya matumizi ya ziada ya fedha zilizotengwa katika bajeti, ununuzi hewa wa vifaa pamoja na baadhi ya taasisi kushindwa kuwalipa fidia wananachi, mbali na fedha za kazi hiyo kutengwa.

Akitoa Mfano aliutaja Mradi wa kudhibiti VVU, akisema  mradi huo ulipangiwa kutumia kiasi cha shilingi Milioni 48.2 kwa ajili ya ununuzi wa dawa aina ya Methadone lakini katika ukaguzi aliofanya hakubaini taarifa yoyote ya kupokelewa kwa dawa hizo, mbali na fedha hizo kulipwa

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.