Habari za Punde

RC Kusini Unguja awasisitiza wananchi kutoa ushirikiano zoezi la sensa ya watu na makaazi

 

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid amewasisitiza wananchi wa Wilaya ya Kusini kutoa mashirikiano makubwa kwa makarani wa Sensa siku ya zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi itakapofika ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

Mkuu wa Mkoa huyo aliyasema hayo katika Bonanza la kuhamasisha Sensa ya Watu na Makaazi lililofanyika huko katika uwanja wa Jamhuri Makunduchi Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja lililoandaliwa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi ((CCM) Wilaya kwa mashirikiano ya pamoja na Ofisi ya Wilaya ya Kusini.

Katika maelezo yake Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa tayari wananchi walio wengi wamepata mwamko juu ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022 na kusema kwamba kwa Wilaya hiyo pamoja na Mkoa wake ana matumaini makubwa kwamba zoezi hilo litafanyika vizuri.

Alieleza kwamba kwa vile tayari siku ya tarehe 23 imeshatangazwa rasmi kwamba ni siku ya mapumziko hivyo ni vyema wananchi wakaitumia vizuri siku hiyo ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kusini Rajab Yussuf Mkasaba aliwasisitiza wananchi wa Wilaya hiyo kutofanya makosa na badala yake washiriki vyema katika zoezi hilo muhimukw amaendeleo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa Sensa.

Alieleza kwamba zoezi la Sensa lina umuhimu mkubwa kwani litatoa fursa kwa Serikali kupanga na kupeleka maendeleo zikiwemo huduma za kijamii kwa wananchi wake.

Mkasaba alieleza matumaini yake kwamba zoezi hilo kwa Wilaya hiyo litafanikiwa kwani tayari maandalizi mazuri yanaendelea kufanyika na kutoa pongezi kwa wananchi mbali mbali waliojitokeza katika Bonanza hilo ambalo lilifana.

Nao viongozi wa CCM wa Wilaya hiyo waliwanasihi wananchi kuhakikisha wanahesabiwa siku itakapofika ili kuweza kuisaidia Serikali kufanya shughuli zake kwa ustadi zaidi ikiwemo kuwapelekea maendeleo endelevu wananchi popote pale walipo.

Mapema katika bonanza hilo michezo mbali mbali ilifanyika ikiwa ni pamoja na mashindano ya kufua na kukuna nazi, mbio za magunia, mashindano ya kibuli, mchezo wa kuigiza ulioongozwa na msanii mahiri maarufu Makombora, uvutaji kamba, nage pamoja na pambano la mpira wa miguu kati ya Jimbo la Paje na Makunduchi.

Baada ya kumalizika kwa mashindano hayo mgeni rasmi alitoa zawadi kwa washindi ikiwemo timu ya Paje ambayo iliifunga Makunduchi mabao mawili kwa moja.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.