Habari za Punde

Taasisi zisizo za kiserikali zina mchango mkubwa katika uimarishaji wa huduma za kijamii                                                          STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

 

Zanzibar                                                                                 30, Agost, 2022

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ushiriki wa Taasisi zisizo za kiserikali katika uimarishaji wa huduma za Kijamii ni muhimu, kwa kuzingatia kuwa Serikali haina uwezo wa kuwafikia wananchi wote.

 

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Viongozi wa Taasisi za Milele Zanzibar Foundation na IFRAJ waliofika kumsalimia pamoja na kuelezea kwa kkna shughuli mbali mbali zinazofanywa na Taasisi hizo.

 

Amesema kwa kipindi kirefu sasa taasisi hizo zimekuwa zikifanya kazi kubwa ya kuisaidia Serikali, hususan katika uimarishaji wa sekta za huduma ya jamii.

 

Alizipongeza Taasisi hizo kwa kufanya kazi  kubwa na kuwa taasisi zinazofanya vyema zaidi hapa nchini katika kuisaidia Serikali katika uimarishaji wa sekta za huduma za jamii, ikiwemo Afya, elimu, maji na Uwezeshaji wajasiriamali. 

.

“Ninaridhika na kazi kubwa mnayofanya kwa kuwa inagusa vipaumbele vya Serikali katika kuimarisha huduma za jamii”, alisema.

 

Alieleza kufurahishwa kwake na kazi kubwa inayofanywa na taasisi hizo katika kujenga mifumo pamoja na kuzingatia umuhimu wa ujenzi wa miundombinu, uwepo wa rasilimali watu na mahitaji ya vifaa katika sekta hizo.

 

Dk. Mwinyi alieleza kuwa Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama, hivyo hatua inayochukuliwa na taasisi hizo ya kusaidia upatikanaji wa Pampu pamoja na uchimbaji wa visima ni ya kupongezwa.

 

Alipongeza taasisi ya IFRAJ kwa ujenzi wa nyumba 500 za makaazi  ya binadaamu na kusema hatua hiyo ni muhimu katika kuisaidia jamii.

 

Aidha,  alitoa shukrani kwa ujenzi wa Misikiti na Madrasa katika maeneo mbali mbali hapa nchini, na kusema  hatua inasaidia uendelezaji wa Dini ya Kiislamu.

 

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali itatoa msukumo ili kufanikisha ujenzi wa Barabara ya Birikau Kisiwani Pemba pamoja na kuuagiza Uongozi  Kikosi cha Kuzuia Magendo KMKM kutoa elimu kwa wamiliki wa Boti za kusafirishia wananchi katika maeneo ya Visiwa Kisiwani Pemba, ili kuwahakikishia usalama katika safari za baharini.

 

Mapema, Mkuu wa Miradi wa Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Khadija Ahmeid Sharrif alisema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia jamii kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo ya uimarishaji wa Afya, elimu, maji pamoja na uwezeshaji Ujasiriamali.

 

Alisema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia uimarishaji wa Afya ya mama na mtoto kwa kuendeleza ujenzi wa Vituo vya Afya katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba, kusaidia vifaa vya tiba pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta hiyo.

 

Aidha, alisema Taasisi hiyo inatoa msukumo mkubwa katika maendeleo ya  sekta ya elimu nchini kwa kufanikisha ujenzi wa majengo ya skuli pamoja na kutoa kusaidia upatikanaji wa mbinu sahihi za kufundishia ,pamoja na kufanya tafiiti.

 

Vile vile alisema taasisi imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wajasiriamali, wakiwemo akinamama na vijana katika kustawisha kilimo cha zao Mwani pamoja na kulifanyia usarifu wa zao hilo ili kuwaongezea kipato.

 

Nae, Meneja wa taasisi ya IFRAJ Abdalla Said Abdalla alisema taasisi hiyo imekuwa ikijishughulisha na ujenzi wa nyumba za makaazi kwa wananachi wenye kipato cha chini, ambapo hvii sasa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 500 zinazogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 7.5.

 

Aidha, alisema taasisi hiyo pia imekuwa ikijishughulisha na ujenzi wa nyumba za Ibada ikiwemo Misikiti na Madrasa katika maeneo mbali mbali nchini, kusaidia wajene na mayatima pamoja na kutoa chakula kwa wanafunzi wa tutu.

 

Vile vile  imekuwa ikisadia ujenzi wa Kliniki, ujenzi wa majengo ya skuli, kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kwa kuchimba visima na kusaidia upatikanaji wa Pampu pamoja na kusaidia huduma muhimu wakati wa majanga, ikiwemo matukio ya moto.

                

Katika hatua nyengine, Ahmeid aliomba Serikali kusaidia Wataalamu watakaoweza kutoa elimu kwa wamiliki wa Boti za kusafirishia wananchi kwenye Visiwa ili kuepusha ajali, huku akibainisha azma ya taasisi hiyo kusaidia upatikanaji wa Vazi la Uokozi (life Jacket).   

 

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.