Habari za Punde

Tuwe na mfumo unaolinda usalama wa wanahabari wanawake - Wito

 Na Khadija Khamis –Maelezo  Zanzibar ,11/08/2022.

 

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe.Tabia Maulid Mwita amesema kuwepo kwa mfumo unaolinda usalama wa wanahabari wanawake na sera za jinsia ndani ya vyombo vya habari   kutasaidia kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia .

 

 Akiyasema hayo wakati akifungua mkutano kwa Wadau wa Habari za kijinsia pamoja na waandishi wa habari ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wanawake Tanzania  (TAMWA )katika Ukumbi wa Kariakoo Wilaya ya Mjini.

 

Amesema Mkutano huo unania njema ya kawainua wanawake na vijana katika vyombo vya habari kwa kuangalia mazingira ya utendaji kazi za wanahabari Zanzibar ,Sheria za Habari, usawa wa Kijinsia na majadiliao ya kuondoa ukatili.

 

 Aidha alisema ukatili wa kijinsia ndio chanzo cha wanahabari kushindwa kutimiza majukumu yao  yakiwemo uandishi wa habari zinazolenga usawa wa kijinsia .

 

Alifahamisha kuwa taarifa zinaonyesha wanawake wengi hukwepa tasnia ya habari  lakini iwapo kutakuwa na sera za jinsia itapelekea wanawake kujitokeza  kufanya kazi na kudumu katika sekta ya habari.

 

Waziri Tabia alieleza kuwa sera ya habari  kwa sasa inahitaji sera inayokwenda sambamba na  mabadiliko ya teknolojia  ya duniani hivyo Serikali na Wadau wa habari hakuna budi kushirikiana kuandaa sera zinazokwenda na wakati na zinazolinda maslahi ya wanahabari .

 

Nae  Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji  Sleman Abdalla Salum amewataka wamiliki wote wa vituo vya utangazaji kuanza kutoa huduma ya kuweka mkalimani kama ambavyo kanuni za utangazaji zinavyotaka .

 

Alisema kuwa Tume ya utangazaji itafuatilia kwa ukaribu kuona watu wenye ulemavu  wanapatiwa haki yao ya msingi na kikatiba ya kupata taarifa na utoa maoni yao juu ya masuala mbali mbali ya maendeleo .

 

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania  (TAMWA) Dr Rose Reuben amasema lengo la chama hicho ni kuwasaidia wanawake  kufikia katika ngazi za kutoa maamuzi jambo ambalo litasaidia  kusikika na kutetea haki zao.

 

Akitoa mada kwa waandishi wa habari wanawake kujuwa sheria inayowalinda  kwa kudaiwa rushwa ya ngono  ni kosa la jinai na kuwataka kuvunja ukimywa kwa unyanyasaji wa kijinsia katika vyombo vya habari.

 

Mkutano huo wa wadau wa habari ni wa siku moja wenye lengo la kujadili Ajenda ya kitaifa ya suala ya kijinsia ndani ya vyombo va habari pamoja na  usalama wa wanahabari wakiwepo kazini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.