Habari za Punde

Viongozi Watendaji wa Maendeleo ya Jamii Wapigwa Msasa

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Wizara hiyo Jijini Dar Es Salaam tarehe 08/09/2022.
Afisa Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo akitoa mada katika mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Jijini Dar Es Salaam tarehe 08/09/2022.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WMJJWM 

Na WMJJWM, Dar Es salaam                                                                                                                   

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka watendaji wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Waziri Gwajima ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi na watendaji wa Wizara hiyo yanayofanyika Jijini Dar Es salaam tarehe 08-09/09/2022.

Amesema mafunzo hayo yana lengo la wakumbusha mambo mbalimbali yanayowahusu ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuongeza tija na matokeo katika utendaji wao.

"Matarajio yangu baada ya mafunzo haya kila mmoja atazingatia kikamilifu mipaka yake ya madaraka na kutekeleza wajibu wetu kama viongozi wa Umma kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo; 
Tutajenga na kuimarisha mshikamano na ushirikiano katika kazi  ili kuimarisha viwango vya utoaji wa huduma kwa wananchi wetu" amesema Mhe. Dkt. Gwajima.  

Ameongeza pia mada zitakazowasilishwa ni muhimu katika utendaji wa majukumu ya viongozi hao na zitawapa fursa ya kujikumbusha kuhusu jinsi wanavyoweza kuboresha utendaji wao kama watumishi wa Umma.

Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima amempongeza Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Devotha Sanga kwa umahiri wake wa kupambana na vitendo vya ukatili akiwa anasimamia Dawati la Jinsia kituo cha Polisi Kigamboni Mkoani Dar Es Salaam na kuwataka watendaji wa maeneo tofauti pamoja na Jamii kushirikiana kwa pamoja kutokomeza vitendo hivyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaimarisha watendaji na viongozi ni kuongeza ufanisi ili kuleta matokeo endelevu katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Watumishi wote wa Wizara watapata mafunzo haya, hatuachi wengine nyuma" amesema Dkt. Chaula.

Akiwasilisha mada ya uongozi kwa viongozi hao Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya uongozi Kadari Singo amesema pamoja na kufanya kazi kwa misingi ya taaluma, viongozi wanatakiwa kuwekeza ushirikiano na mahusiano mazuri na watumishi walio chini yao.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.