Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Al-hajj Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia waumini wa Masjid Hasana Amani kwa wazee baada ya Ibada ya Swala ya Ijumaa Leo tarehe 09/09/2022
Na Ali Mohammed , OMPR
Waislamu na Wananchi kwa ujumla wametakiwa kuwasimamia vijana wao katika mienendo yao ya kila siku kwa maslahi ya taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito huo alipojumuika na Waumini katika Masjid HASSANA Amani kwa wazee wakati wa Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Ameeleza kuwa ni wajibu wa kila muislamu na mzanzibari kuifatilaia mienendo ya vijana wao ili kuhakikisha wanaishi kwa nidhamu na kupata waumini na viongozi bora wa baadae.
Mhe. Hemed amesema kuwa kila mzazi au mlezi anawajibu wa kushirikiana na jamii inayomzunguka ili kuendeleza silka na utamaduni wa mzanzibari katika malezi kwa vijana pamoja na kutumia busara kwa wanaowaongoza ili kupata jamii bora.
Alhajj Hemed amewataka waumini na wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya Nane inayoongozwa na Dkt Hussein Mwinyi juu ya kupambana na udhalilishaji na madawa ya kulevya hasa kwa vijana wetu.
Akizungumzia suala la maendeleo Alhaj hemed amesema waislamu na wazanzibar ni vyema kuwa na utamaduni wa kuuliza pale ambapo hawafahamu ili kujua nini azma ya serikali kwa wananchi wake juu ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha Mhe. Hemed amewataka waumini kutoa mashirikiano kwa serikali katika kuitunza amani na utulivu uliopo nchini usiweze kupotea kwa maslahi ya vizazi vya sasa na baadae.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka waislamu na wazanzibar kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kuiombea Dua nchi yetu pamoja na kumuombea Dua rais wa Zanzibar Dkt. Husein Mwinyi ili aweze kutimiza yale yote aliyoyaahidi kwa wananchi wake.
Kwa upande wake Imamu wa Msikiti huo Sheikh. Mussa Mabrouk amewataka Waumini na madereva anaoendesha vyombo vya moto kuwa makini katika uendeshaji wao ili kupunguza ajali zisizokuwa za lazima ambazo zinasababisha vifo na ulemavu wa kudumu.
Amesema ni wajibu kwa kila muumini kufanya matendo mema huku akijua kuwa ipo siku ataulizwa ni jinsi gani aliishi katika mgongo wa ardhi,pia Mtume Muhamad S.A.W amesema kuwa “yeyote atakae mdhulumu mwenzake au kujidhulumu yeye mwenyewe basi hatoingia peponi”.
No comments:
Post a Comment