Na.Is-Haka Omar. Zanzibar.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekishauri Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) kuweka mazingira rafiki kwa nchi yake kutoa kipaumbele cha kuwekeza Zanzibar katika nyanja za uvuvi,kilimo,utalii na mafuta na gesi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi wakati akizungumza na Balozi mdogo wa China Zanzibar Zhang Zhisheng huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Dk.Mabodi, amesema China ina fursa nyingi za kiuchumi zinazokwenda sambamba na falsafa ya uchumi wa buluu ambao ndiyo kipaumbele cha Serikali ya awamu ya nane katika kukuza uchumi wa nchi.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi, amesema nchi ya China kupitia Chama chake wamekuwa na urafiki wa kihistoria na CCM hivyo wana mchango mkubwa katika ustawi wa maendeleo ya Zanzibar kiuchumi,kisiasa na kijamii.
“ CCM na CPC tumekuwa marafi wa miaka mingi na urafiki wetu umeleta mafanikio kwa pande zote mbili mfano ni kwamba Vijana wetu wengi wamekuwa wakienda China kupata elimu na mafunzo tofauti na wao pia wamewekeza kwa baadhi ya maeneo nchini.
Hivyo mazungumzo yetu ya leo ni sehemu ya kudumisha mahusiano yetu kwa vyama na serikali zetu kwa ujumla ili kuhakikisha wananchi wetu wananufaika.”, alisema Dk. Mabodi.
Alisema licha ya CCM kunufaika na fursa mbalimbali bado inahitaji kuendelezwa kwa mpango wa mafunzo ya uongozo kwa makada na watendaji wake ili wakajifunze masuala mbalimbali nchini China.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alieleza kwamba uimara wa vyama vya Kikomunisti Duniani unatokana na utekelezaji kwa vitendo dhana ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambapo CCM na CPC wanatakiwa kuanzisha miradi ya pamoja ya kiuchumi ili vyama vyao viendelee kujitegemea.
Pamoja na hayo aliwatakia heri,mafanikio na maazimio mema kwa Chama cha CPC katika mchakato wao wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho unaoendelea hivi sasa.
Naye Balozi mdogo wa China Zanzibar Zhang Zhisheng, ameipongeza CCM kwa juhudi zake za kuisimamia vizuri serikali ya awamu ya nane ya Zanzibar inayoendelea kuimarika kiuchumi.
Balozi Zhisheng, alisema CPC kupitia Serikali yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar kwa kila hatua ya maendeleo ili wananchi wa pande zote mbili wanufaike.
Pamoja na hayo alipongeza mafanikio yaliyofikiwa nchini chini ya mfumo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa uliosaidia kudumisha amani,umoja na mshikamano.
Sambamba na hayo ameahidi kuhakikisha anafanikisha mpango wa ujenzi wa Chuo Cha Kisasa cha Makada cha CCM ili aweke kumbukumbu ya kudumu ya urafiki wa CPC na CCM sambamba na uwepo wake Zanzibar.
No comments:
Post a Comment