Habari za Punde

Kikao cha Kamati Maalum ya CCM Zanzibar Yajadili Majina ya Wagombea Ubunge Jimbo la Amani Zanzibar

Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein (kulia)alipokuwa akiongoza kikao cha siku moja cha   Kamati Maalum ya  Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar  kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Afisi ya Kuu ya CCM Kisiwandui Jijini Zanzibar (kushoto) Mjumbe  wa Kamati Kuu ya CCM Taifa pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi. [Picha na Ikulu] 17Nov 2022.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein,leo ameongoza Kikao Maalum cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.

 

Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi Kuu ya CCM,Kisiwandui Zanzibar.

 

Pamoja na mambo mengine Kikao kitapokea na kujadili mapendekezo ya Wana CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge katika Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Amani Zanzibar.

 

Uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Amani unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Marehemu Mussa Hassan Mussa wa Chama Cha Mapinduzi, aliyefariki dunia mnamo Octoba 13,mwaka huu.

 

Chama Cha Mapinduzi kikiwa ni miongoni mwa vyama vya kisiasa nchini kinatekeleza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 71(1) pamoja na kifungu cha 39(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.

 

Pamoja na hayo kufuatia kuwepo kwa nafasi hiyo Chama Cha Mapinduzi kinalazimika kuhakikisha kwamba kinashiriki kikamilifu katika Uchaguzi huo kwa kuweka mgombea wake ili kutekeleza matakwa ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la mwaka 2020 Ibara ya 5 (1).

 

Ibara hiyo ya Katiba ya CCM inakitaka Chama   kushinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande wa pili.

 

Viongozi mbali mbali walioudhuria kikao hicho ni pamoja Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

 

Wengine ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeil Ali Maulid pamoja na Wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.