OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 11.11.2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi
wa msikiti wa Rahman kuweka utaratibu maalum wa kuwawezesha walimu wa Madrasa,
ili waweze kujikimu na kutekeleza vyema majukumu
yao.
Alhaj Dk. Mwinyi amewaeleza hayo waislamu baada ya kukamilisha ibada ya sala ya Ijumaa, iliofanyika ‘Masjid
Rahman’, uliopo Kijichi Mkoa Mjini
Magharibi Unguja.
Amesema kuna umuhimu kwa uongozi wa msikiti huo kuweka utaratibu maalum utakaowawezesha waislamu
kutoa michango yao kwa ajili ya kuwawezesha walimu wanaofundisha katika madrasa
ya msikiti huo ili waweze kujikimu kimaisha na kutekeleza vyema majukumu yao ya
kufundisha.
Alisema katika hali ilivyo hivi sasa katika misikiti mingi nchini, walimu wa madrasa wameachwa
bila ya msaada wowote na hivyo kushindwa kujikimu kimaisha, huku wakibeba dhima
kubwa ya kufundisha watoto dini ya Mwenyezi Mungu.
“Sasa huyu mtu tunamkabidhi watoto wetu kusomesha kitabu cha Mwenyezi
Mungu, ataishi vipi bila ya kumuwezesha?”, alihoji Alhaj Mwinyi.
.
Aidha, alisema hatua hiyo inapaswa
kwenda sambamba na kuwawezesha maimamu pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuutunza
msikiti huo kwa kuufanyia matengenezo ya mara kwa mara pale vifaa ikiwemo
mifereji inapoharibika.
Alhaj Mwinyi alisema pamoja na
msikiti huo kutumiwa kwa ajili ya sala, lakini pia inapaswa kutumika kwa
shughuli nyenginezo za eibada.
Alitumia fursa hiyo kuwashukuru
wafadhili waliofanikisha ujnezi wa msikiti huo, sambamba na kutoa shukrani kwa heshima
aliyopewa ya kuufungua.
Nae, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti
wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume alimshukuru Rais Alhaj Dk. Mwinyi kwa kuungana na waislamu na kushiriki katika
ibada tofauti katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake, ikiwemo ufunguzi
wa misikiti katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba, na hivyo akawaomba waislamu kuendelea
kumuombea dua.
Mapema, Khatibu katika sala hiyo ya
Ijumaa, Sheikh Omar Abdi Abdalla aliwataka waislamu kufuata maamrisho ya Mwenyezi
Mungu na kuonyesha uchamungu wao kwa kuepuka yale yote aliyoyakataza.
Aidha, aliwataka waislamu kuwa na
mwamko katika kutafuta elimu ya dini yao, sambamba na kuwa na msimamo wa kushukuru
neema za Mwenyezi Mungu, ikiwemo uwepo wa amani nchini.
Msikiti huo wa ‘Masjid Rahmman
ulifunguliwa Ijumaa iliopita, ambapo Rais Alhaj Dk. Mwinyi aliwakilishwa.
Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment