Habari za Punde

DC Moyo Ndio Chanzo cha Miradi Mingi Kutokukamilika kwa Wakati

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akizungumza wakati kulifungua  Kongamano la Kujadili namna gani ya kujiepusha na vitendo vya rushwa katika jamii.

Na Fredy Mgunda, Iringa.

SERIKALI imewataka wadau wa maendeleo pamoja na Taasisi mbalimbali kuupitia mkakati wa kitaifa dhidi ya Rushwa na kujitathimini ili kuona namna gani wanashirikiana na katika kutokomeza vitendo vya rushwa nchini.

Akizungumza katika kongamano la kukuza maadili, na vita dhidi ya Rushwa mkoani Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa hatua ya kujitathimini mara kwa mara itasaidia kukuza maadili katika taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukemea na kuchukua hatua atakayejihusisha na vitendo vya rushwa.

Kiongozi huyo wa Wilaya ya Iringa alisema kuwa kuwepo kwa vitendo vya Rushwa kunaifanya serikali kushindwa kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kuwahudumia wananchi kikamilifu, kwa kuwa baadhi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutumika isivyo sahihi kutokana na rushwa.

Moyo alisema kuwa Rushwa ni chanzo cha miradi mingi ya maendeleo yenye manufaa kwa jamii kutokukamilika kwa wakati huku akitumia jukwaa hilo kuwakumbusha wadau kuupitia mkakati wa kitaifa dhidi ya rushwa.

Alisema kuwa maadhimisho hayo ya siku ya maadili na haki za binaadam ni fursa nzuri kwa kila mmoja kujitafakari namana gani amezingatia maadili katika shughuli anazofanya ikiwemo ushiriki wake katika kupinga vitendo vya rushwa kwani uchumi wa nchi umekuwa ukidumazwa na vitendo hivyo vya rushwa.

Awali Kamanda  wa Taasisi ya kuzuia na kupamabana na Rushwa mkoa wa Iringa Domina Mkama akimkaribisha mgeni wa heshima ameeleza lengo la kongamano hilo kuzisaidia taasisi na jamii kufanya kazi bila kutoa au kupokea rushwa.

Aidha Kiongozi huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa Amewahimiza washiriki wa kongamano hilo wakiwemo wawakilishi kutoka klabu za wapinga rushwa vyuoni kuwahakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika vita dhidi ya Rushwa kwa kuielimishja jamii kutambua athari za rushwa kwa maendeleo ya taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea wakati kongamano la kujadili namna gani ya kujiepusha na vitendo vya rushwa katika jamii.
Kamanda  wa Taasisi ya kuzuia na kupamabana na Rushwa mkoa wa Iringa Domina akiongea wakati kongamano la kujadili namna gani ya kujiepusha na vitendo vya rushwa katika jamii
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Moyo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kulifungua Kongamano la kujadili namna gani jamii inatakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa katika maisha ya kila siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.