Habari za Punde

Dodoma Yaweka Mikakati Kukuza Sekta ya Elimu * Yajipanga Kukabiliana na Utoro Shuleni 2023

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa Mhe. Rosemary Senyamule akifungua kikao kilichofanyika katika ukumbi  wa Jengo la mkapa na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo bajeti ya Mkoa, Elimu, Afya, Kilimo, Maji na Mazingira.  

Baadhi ya wajumbe walioshiriki katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Kulia ni Bi. Dionisia Mjema Kamishna Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta Fedha kutoka Wizara ya Fedha akifuatilia mawasilisho katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jengo la Mkapa

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiongoza kikao cha  Kamati ya  Ushauri ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa  Jengo la Mkapa na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Elimu, Afya, Kilimo, Maji na Mazingira.  

Mkoa wa Dodoma umejidhatiti kukabiliana na utoro wa wanafunzi shuleni kupitia maazimio yaliyowekwa kwa mwaka 2023 kupitia kikao cha pili cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jengo la Mkapa chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Katika kikao hicho, agenda ya elimu imejadiliwa kwa kina na kupewa msukumo madhubuti ikiwa ni miongoni mwa ajenda nane za kikao hicho kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo bajeti ya Mkoa, Elimu, Afya, Kilimo, Maji na Mazingira.  

Mkoa wa Dodoma unakabiliwa na changamoto kubwa ya utoro kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari huku sababu kubwa zikitajwa kuwa ni ukosefu wa chakula shuleni, Wazazi/Walezi kutoipa thamani stahiki elimu hivyo kutowajibika kwa malezi ya watoto wao, Viongozi wa Vijiji kushindwa kutimiza wajibu wao wa kudhibiti utoro shuleni na umbali mrefu wa kwenda na kurudi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema licha ya changamoto hizo katika sekta ya elimu, Wilaya ya Bahi imefanikiwa kushika nafasi ya kumi kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2022.

“Naipongeza sana Halmashauri ya Bahi kwa kushika nafasi ya kumi kwa mpangilio wa ufaulu wa Halmashauri kitaifa kwani wameifaharisha Mkoa mzima wa Dodoma. Natoa shime kwa Halmashauri nyingine kwenda kujifunza Bahi namna walivyofanya na kufanikiwa kuingia kwenye kumi bora za kitaifa. Pia tukafanye kazi kubwa kuhakikisha watoro wanarudi shuleni mwaka 2023” Amesema Mheshimiwa Senyamule.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa Dkt. Fatuma Mganga naye ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kutoa msukumo kwa walimu kufundisha kwa bidii kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu.

Akitoa maoni yake juu ya maazimio ya mwaka 2023, Afisa Elimu Mkoa Bw. Gift Kyando amesema “Mwaka ujao tunaazimia wanafunzi wote watakaomaliza elimu ya msingi kurudi mapema shuleni kwa ajili ya kujiandaa na masomo ya kidato cha kwanza tofauti na ilivyokua mwaka huu kwani mitihani ilichelewa badala ya kufanyika mwezi Septemba imefanyika mwezi Oktoba ila mwakani itafanyika kama kawaida mwezi Septemba”

Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameziagiza Halmashauri kuongeze kasi ya kukusanya mapato na kutoa asilimia kumi. “Naziagiza Halmashauri zote kwa kushirikiana na wadau kuendelee kutengeneza madawati ili kupunguza upungufu uliopo, Halmashauri zikamilishe usimamizi wa sheria ndogondogo za upatikanaji wa chakula shuleni pamoja na kudhibiti utoro, kila shule itenge eneo la kuzalishia chakula kwa wanafunzi, vyuo vya ufundi viimarishwe” Alisisitiza Mhe. Senyamule.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.