Habari za Punde

KOBE…KOBE… KOBE…

 

Na.Adeladius Makwega-CHAWA

Hapo zamani za kale huku Ukwereni alikuwapo mfalme ambaye Mungu alimjalia kuwa na binti Mrembo. Binti huyu alipofikia umri wa kuvunja ungo mfalme hakuhitaji mahari yoyote kwa yule aliyemuhusudi binti huyo kumuoa.

Mfalme alitoa sharti moja kwa yule atakayeweza kuupanda mti mkubwa hadi kileleni hapo nyumbani kwake na kuyachuma matunda yake na kushuka salama ndiye atakayeweza kumuoa binti mfalme.

Wengi walimuhusudi binti mfalme, hata kama mwanakwetu angekuwapo katika nchi ya Wakwere wakati huo na yeye angeshiriki katika kinyang’anyiro hicho kwa namna alivyokuwa mrembo huyo binti mfalme. Hapo mwanakwetu angekuwapo angekosa sifa moja tu ya Ukwere maana Waluguru, Wapogoro, Wazaramo, Wazigua na Wadoe hawakuruhusiwa.

Hapo sasa kila Mkwere alijaribu bahati nasibu hiyo kutoka kwa mfalme. Wasaidizi wa mfalme walinadi sifa hizo kuwa sharti lilikuwa anayeshiriki lazima awe kiumbe hai kutoka nchi ya Wakwere.

Waliposhindwa Wakwere wote mfalme alicheka sana, sasa wanyama nao walifika kuitafuta bahati hiyo ya kumposa binti huyu wakisema kuwa nao ni viumbe hai katika nchi hiyo, miongoni mwao alikuwapo Twiga, Nyati, Tendo, Fisi na Chui.

Sasa hapo yakawa maajabu katika nchi ya Wakwere kweli binti mfalme anaozeshwa kwa wanyama? Wanyama hao wakapanga foleni kando ya mti huo mwisho wa siku hakuna aliyeweza kupanda hata mita moja ya kisiki cha mti huo. Mwanakwetu kinyanga’anyiro kikaendelea wanyama wanajiuliza na binadamu kutoka kona zote nne katika nchi ya Wakwere yenye upande na pwani na bara wakijiuliza kweli wamemkosa binti mfalme?

Mjadala huo wa viumbe hai isipokuwa mimea tu yaani ulioruhusiwa na mfalme ili binti yake aolewe ulimuibua Kobe huko alipo na kufika katika uwanja wa kumtafuta bingwa wa kumuoa binti mfalme. Kobe alipofika hapo akawaeleza nia yake kwamba anaomba na yeye ashiriki katika shindano hilo. Mfalme hakuwa mbaguzi alimruhusu hapo hapo. Mwanakwetu Chui alicheka mno akasema Kobe tumeshindwa sie mabingwa  wa kuwinda na kuhifadhi nyama katika miti mikubwa utaweza wewe unayetambaa ardhini?

Kobe aliruhusiwa pale alipogusa kisiki cha mti ule alikuwa na nguvu kama sumaku umati wa wanyama na binadamu ukashuhudia Kobe akipanda kwa kasi mti huo. Umati kando ya mti wa mfalme ilisikika kwa shangwe wakisema Kobee… Kobee… Kobee…huku wanyama wengine wakishangilia kwa miluzi ya shangwe.Maajabu Kobe alipanda kwa kasi kubwa mno na kufika kilele cha mti huo na kuyafikia matunda kuthibitisha kuwa amefika juu ya mti huo akachuma tunda moja na kulila, huku maganda aliyatupa chini.

Sauti chini ya mti huo ni ile ile ya “ Kobee… Kobee… Kobee…”

Kobe akachuma tunda moja na kushuka nalo chini na alipofika hapo alimkabidhi mfalme. Simulizi zinatapakaa jamani ehe mfalme huku anaozesha binti yake Kobe, wakumbuka majirani wa Wakwere wale Waluguru, Wapogoro, Wazaramo, Wazigua na Wadoe wanashanga huyu ndugu yetu vipi?

Maajabu mnyama amuoe binadamu? Hayo yakionekana kama mazingaombwe lakini ndiyo yaliyokuwa yanatokea.

Kumbuka watu wapo uwanjani wanatazama Kobe analikabidhi tunda la mti ule kwa mfalme, binfi mfalme akawa analia inakuwaje tena leo anaolewa na Kobe? Kilio hicho cha binti mfalme kiliibua shangwe kutoka kwa wanyama wakisema si mmetangaza wenyewe, siye tulikuwa tunajilia majani mkatualika na mmetupa nafasi sote hapo lazima Kobe akabidhiwe jiko lake na aondoke nalo msituni.

Mfalme hakuwa mtu wa kigeugeu akasema nilitoa ahadi mbele yenu na ahadi yangu ni ilani lazima binti yangu aolewe na yule aliyeweza kuupanda mti huo na kunikabidhi matunda ya mti huo. Hiyo ni nadhili yangu sasa imetimia.

Harusi ikaandaliwa vizuri sana katika makazi ya mfalme nao waalikwa kutoka kwa machifu wa Waluguru, Wapogoro, Wazaramo, Wazigua na Wadoe walikuwapo huku wanyama kutoka msitu wa Wakwere wakifika kumchukua bibi harusi binti mfalme.

Kobe akachukua jiko lake binti mfalme, huku binti mfalme akiondoka na kwa unyonge, shingo upande, walipofika huko binti mfalme akagoma kulala na Kobe kwani akisema ni mchafu, ananuka, anakula matope na udongo, kutembea hawezi na maneno kede kede. Kobe hakulidhishwa na mkewe kwa visa vyake, akafunga safari hadi kwa mfalme kumueleza hilo. Binti mfalme alielezwa kumuheshimu mumewe na kumpa haki zake zote, hali hiyo ilizidi kumnyima raha binti mfalme, ndoa hiyo badala ya kuwa ya kuraha ikawa ya karaha.

Binti mfalme akajiuliza maswali mengi anafanyaje? Akilini mwake alikumbuka kuwa mama yake alimfundisha kuwa katika maisha mambo yakiwa magumu na yamekuzidi kimo lazima umtafute fundi wa kuyatatua. Hivyo alimuaga mumewe Kobe kuwa anakwenda kusalimia wazazi kumbe alikwenda kwa mganga.

Safari hadi kwa mganga na kumueleza shida zake na mume tangu alivyoozeshwa na baba yake. Mganga akamjibu kuwa siku ya ndoa hiyo na yeye alikuwa mwalikwa na anatambua kila kitu. Mganga akamwambia kuwa huyo mumewe siyo kobe kama unavyomuona bali ni miongoni mwa matajiri wakubwa kuliko hata mfalme mwenyewe ili maisha yaende katika nchi hiyo aliamua kuwa na umbo la kobe. Binti Mfalme akafurahi mno akimuomba mganga ampe mbinu ya mumewe Kobe aweze kurudi kuwa binadamu.

Mganga akaomba apewe kitu cha thamani ili aifanye kazi hiyo, mke wa Kobe akampa mganga mikufu saba ya dhahabu naye mganga alifurahi sana na kuifanya kazi hiyo.

“Ukifika nyumba tayarisha pombe, weka katika mtungi chini ya kitanda mnacholala na mumeo, wakati wa kulala mumeo atasikia harufu nzuri ya pombe, akishaisikia atatamani kuinywa, utamtengea atakunywa, akinywa atalewa na kuuchapa usingizi. Wewe utakuwa na jukumu la kuyaondoa magamba yake yote mwili mzima. Ukimaliza kazi hiyo yachome moto magamba yote na yakiwa yanaungua mumeo atabadilika na kuwa binadamu.”

Kweli mke wa Kobe(Binti Mfalme) alirudi nyumbani kwake na kuyatekeleza masharti yote ya mganga, pombe ilitengeneza na mtungi uvunguni, Kobe akaenda kulala na mkewe akaisikia harufu ya pombe na akatengewa , akanywa,  akalewa na magamba kuondolewa, yakachomwa moto mwanakwetu muda huo huo. Kobe akabaki na nyama tu magamba yalipoungua na kumalizika Kobe akabadilika na kuwa binadamu na madhari ya pango ikawa hekalu kubwa sana zaidi ya nyumbani kwa falme wa Wakwere. Binti Mfalme na mumewe wakaisha maisha mema ya yenye furaha tele.

Nchi ya Wakwere wanaona kila kinachoendelea,wanyama wanashangilia wamewashinda binadamu kwa kumposa binti mfalme. Sasa wanyama wamebaki njia panda Kobe kawa binadamu tajiri pangoni hayupo sasa yupo katika hekalu.

Mabinti wa Kikwere majumbani kwao migogoro ya ndoa ikaanza wakiomba talaka kwa waume zao na kutamani kuolewa na makobe. Kweli waliolewa na kobe hao na kwenda kuishi maisha ya mapangoni wakivumilia kuwa kuna siku na wao watakuwa na maisha mazuri kama yale ya binti mfalme. Huku wanyama wakimsaka ndugu yao Kobe aliyebadilika na kuwa binadamu.

Kobe wanawake walilamikia wanaume zao kuchukuliwa na binadmu nao binadamu wanaume wakilamikia wanawake zao kuomba talaka na kuolewa na kobe huko hakukuwa na amani mambo yalivurugika na hakuna lililoweza kufanyika tena si kwa binadamu wala wanyama.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

(NB Kwa utafiti zaidi juu ya simulizi za makabila ya Tangayika unaweza kumsoma Stephern A Lucas mahusiano ya Utani Tanzania 1973.)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.