Habari za Punde

Ufungaji wa mafunzo mafupi ya ulinzi wa mifumo ya kompyuta na kuzuia wizi wa mitandao

Mkurugenzi kutoka Kitengo cha Usalama wa Mitandao katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhandisi Stephen Wangwe amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la udukuzi wa taarifa katika mitandao jambo ambalo linapelekea matatizo makubwa kwa Taasisi na watu binafsi  ikiwemo upotevu wa fedha.

Alizungumza hayo, wakati wa ufungaji wa mafunzo mafupi ya ulinzi wa mifumo ya kompyuta na kuzuia wizi wa mitandao, yaliyofanyika katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), Mbweni Zanzibar.

Alisema kumekuwa na tovuti nyingi zinazotumwa katika mitandao ya kijamii ambayo wananchi wengi bila kufahamu hufuata na kujiunga na tovuti hizo, na hatimae hupelekea kudukuliwa taarifa zao, hivyo amewataka wananchi kuwa makini katika utumiaji wa mitandao.

Katika hatua nyengine, Mkurugenzi Wangwe amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuyatumia vyema katika kuisaidia serekali, pamoja kuhakikisha wanaweka mbele uzalendo wa nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia(KIST), Bi Latifa Ufuzo amesema mafunzo hayo yatawaimarisha na kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa ndani na nje ya Taasisi katika ulinzi wa mifumo.

Alieleza kuwa, ipo haja ya kujenga misingi imara ya kuhakikisha kila kitengo cha Tehama kinakuwa na ulinzi wa kutosha ambapo miongoni mwa misingi hiyo ni kupatiwa mafunzo ya ulinzi wa mifumo na kompyuta.

Nae Mkufunzi wa Mafunzo hayo Bwana Yussuf Kileo amesema bara la afrika lina kazi kubwa ya kuhakikisha mifumo inapata ulinzi wa kutosha kwani matukio mengi hutokea Afrika, ikiwemo uporaji wa fedha kupitia mitandao.

Amesema miongoni mwa sababu zinazopelekea uporwaji wa fedha katika mitandao ni uwekezaji wa fedha katika mitandao ambayo hata wamiliki wake hawafahamiki.

Hivyo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuineza elimu walioipata ili jamii iweze kujilinda na uhalifu unaofanywa na wadukuzi wa mitandao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.