Habari za Punde

Dk Mwinyi: Tuendane na kasi ya wawekezaji


 

NA MWASHAMBA JUMA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaagiza watendaji wa Serikali wanaotoa huduma viwanja vya ndege vya kimataifa vya Abeid Amani Karume waendane na kasi ya wawakezaji ili kuimarisha huduma kwa wageni wanaoingia na kutoka viwanjani hapo.

Dk. Mwinyi alitoa maagizo hayo alipofungua maduka na huduma za makampuni ya kimataifa ya  DNATA, kwenye jengo jipya la terminal 3 uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Kisauni Zanzibar.

Aliwataka Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)watoa huduma za afya pamoja na benki wanaohudunia viwanjani hapo, kutumia mifumo ya kisasa kuimarisha huduma zao ili kuwaondoshea ushumbufu wageni wanaokaa mdamrefu kusubiria huduma.

“Naiagiza Idara ya Uhamiaji kupunguza muda wa wanaosafiri, wanakaa uwanjani muda mrefu kabla hawajatoka, waboreshe mfumo wa kielektroniki ufanyekazi vizuri zaidi au washirikiane na wadau wetu hawa kuangalia namna ya kuondosha usumbufu kwa wageni” Aliagiza Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi pia aliwataka TRA kuongeza bidii kuhakikisha huduma zao zinakwenda haraka ili kuenda sambamba na kasi ya huduma zainaotolewa sasa na wadau wakimaifa.

“Niwatake Mamlaka ya Mapato Tanzania, waongeze bidii kuhakikisha huduma zao zinakwenda haraka kama inavyotakiwa, watu wa Afya pamoja na benki zinazotoa huduma hapa kwa upande wetu Serikali, lazima tufanye vyema zaidi ili tuendane na kasi ya wenzetu hawa waliotoka nje ya nchi” Alisihi, Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi alieleza Serikali ilifanya uamuzi sahihi kushirikiana na makampuni binafsi yenye hadhi, utaalamu na uzoefu wa kutoa huduma viwanja vya ndege duniani na kuongeza uamuzi huo umesaidia kuboresha huduma viwanjani hapo hali iliyosaidia Serikali kuongeza mapato yake.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajivunia mafanikio makubwa iliyofikiwa katika kuimarisha uchumi wake kwa kuongezeka safari za ndege za moja kwa moja za Mashirika ya ndege za Kimataifa kufikia na kueleza hadi sasa Mashirika ya ndege 34 yanafanya safari zake kuja Zanzibar kwa kutumia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Aidha, alieleza hadi mwaka jana idadi ya abiria ilifikia milioni 1.8 ikilinganishwa na milioni 1.3 kwa mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 38 ambalo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea Zanzibar.

Dk. Mwinyi alieleza, kuongezeka safari za ndege na abiria pia kumeongeza mapato ya Serikali kufikia shilingi Bilioni 8.1 kutoka kwenye robo ya kwanza naya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 (Julai – Disemba 2022) ikilinganishwa na makusanyo ya robo ya pili mwaka 2019 ambayo yalikua Bilioni 2.5.

Alisema licha ya jitahada kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu tofauti kuwekeza kwenye viwanja hivyo, bado utoaji wa huduma ulikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo usimamizi hafifu wa utoaji huduma, ukosefu wa taaluma na ubunifu pamoja na kukosekana kwa vifaa vya kisasa vya utoaji wa huduma za mizigo na abiria, hali iliyosababisha usumbufu kwa wageni na wenyeji waliokua wakitumia uwanja huo pamoja na kuchangia kupotea mapato ya Serikali.

Katika hatua nyengine Rais Mwinyi, alisifu hatua ya Mamlaka ya Viwanja vya ndege, Zanzibar (ZAA) kuuunga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kuwa mwanachama wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (Airport Council International – ACI mnamo mwaka jana.

Hata hivyo, alisema kuungwa kwa Uwanja huo kimataifa kutasaidia kupimwa ubora wa utoaji wa huduma zake kwa kulinganishwa na Viwanja vyengine vya ndani ya Afrika na kueleza matarajio ya Serikali kukiwezesha Kiwanja cha Ndege Pemba, kutumika kwa Ndege za Kimataifa hali aliyoieleza kwamba itaifungua Pemba kiuchumi.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed alisema Uwekezaji wa huduma za uendeshaji viwanjani hapo ulianza harakati zake tokea Novemba 25 mwaka 2021 baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuingia makubaliano ya mkatana na makampuni ya Emirate ya Dubei kwa lengo la kudumisha huduma za ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa kiwango cha Kimataifa, kuongeza idadi ya abiria watakaingia nchini, na kujenga maduka na mikahawa ya kisasa viwanjani hapo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya DNATA, Emirate Leisure Retail na MMI, Steve Allen, alisema Zanzibar sasa inatengeneza ukurasa mpya wa historia ya visiwa vyake kwa kuimarika vivutio vya utalii kupitia huduma bora wanazozitoa viwanjani hapo.

Kampuni ya “DNATA” inatoa huduma za ndege na kuendesha ukumbi wa abiria wa Daraja la Biashara kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Kampuni ya “Emirates Leisure” inatoa huduma ya uendeshaji wa Migahawa na kampuni ya “Segap/Egis” ya Ufaransa inatoa huduma ya msaada wa kiufundi wa uendeshaji na usimamizi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar.

Makampuni hayo, yameisaidia kutoa ajira 400 kwa vijana wa Zanzibar ambao wanatoa huduma mbali mbali viwanjani hapo baada ya kupatiwa mafunzo kupitia Kampuni ya Dnata kuhusiana na utoaji bora wa huduma za viwanja vya ndege vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.