Habari za Punde

Michuano ya 17 Kombe la Mapinduzi Yatimua Vumbi leo Kati ya Timu ya KVZ na Mlandege Timu Hizo Zimetoka Sare ya Bao 1--1

Mchezaji wa Timu ya Mlandege akimpita beki wa Timu ya KVZ wakati wa mchezo wa Kombe la Mapinduzi uliofanyika leo katika Uwanja wa Amaani Jijini Zanzibar Timu hizo zimetoka sare ya bao 1--1.

Na. Mwanajuma Juma -Zanzibar.

TIMU za soka za KVZ na Mlandege zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa michuano ya kombe la mapinduzi iliyoanza jana visiwani Zanzibar.

Mchezo huo ambao ulichezwa uwanja wa Amaan saa 10:15 za jioni mchezaji Mukrim Juma Madai wa KVZ alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilionekana kushambuliana kwa vipindi hadi mapumziko walikuwa hawajafungana.

Hata hivyo katika mchezo huo Mlandege ilionekana kuwazidi wapinzani wao kwa kila idara huku wachezaji wake wakileta mashambulizi ya mara kwa mara lakini umakini mkubwa ulioneshwa na mlinda mlango wa KVZ Ibrahim Abdalla Rashid akaokoa mashuti yaliyokuwa yakilengwa langoni mwake.

Mlandege ambayo inafundishwa na kocha Abdalla Mohammed Juma 'Bares', wachezaji wake walitengeneza mashambulizi Manne ya nguvu ambayo mawili yalikoswa na Abdulnassir Asaa ambalo moja liligonga posi dakika ya 38 na moja likachezwa na mlinda mlango wa KVZ.

Mashambulizi mengine mawili ambayo Mlandege watajutia ni yale ya Yussuf Suleiman dakika ya 15 na Masoud Khamis Haji dakika ya 24 ambayo yaliokolewa na mlinda mlango wa KVZ.

Kwa upande wa KVZ wao katika kipindi cha kwanza walitengeneza nafasi moja dakika ya tatu kupitia mchezaji wake Rahim Shomari ambalo alilipaisha juu .

Kipindi cha pili kilianza na mashambulizi yakaendelea ambapo dakika ya 46 Mohammed Said Mohammed 'Mesi' akaifugia timu yake bao la kuongoza ambalo dakika mbili baadae wakasawazishiwa baada ya mlinzi wa KVZ Mukrim Juma Madai kujifunga wakati wa kuokoa mpira uliopigwa na Abdulnassir Asaa Gamal na kuingia moja kwa moja wavuni.

Leo kutakuwa na michezo miwili ambapo saa 10:15 Namungo itacheza na Chipukizi na saa 2:15 Singida itapambana na KMKM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.