Mkuu wa Operesheni na Huduma za Kibinadamu,kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Haji Faki Hamduni pamoja na maofisa wake wakifika katika nyumba iliotokea ajali ya moto kwa kuwafariji huko Chukwani nje kidogo mwa jiji la Zanzibar JanuarI 30,2023 .
Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar 30/01/2023
Nyumba moja imeteketea kwa moto katika maeneo ya chukwani nje kidogo na mji wa Zanzibar na vitu kadhaa vimeungua na hadi sasa haijajulikana gharama ya vitu hivyo.
Akizungumza na waandishi wa Habari Mkuu wa Operesheni na Huduma za Kibinadamu, kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Haji Faki Hamduni Alisema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyoanza kwenye kisambazaji cha umeme (Main switch) iliopo katika ghala la kuhifadhia vifaa vya nyumbani.
Amewataka wananchi kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hichi cha kiangazi chenye upepo na joto kali na kutoa taarifa mapema katika taasisi husika mara tu wanapoona hitilafu ya umeme ili kuweza kunusurika watu na mali zao .
Nae Mkaazi wa nyumba hiyo Abdulhabib Abrahman Said amesema amesikitika na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote yaliyotokea kupata mtihani huo ambao haukuutegemea kutokea.
Alisema wakati alipotoka nyumbani kuelekea katika harakati zake za Maisha, hakuona ishara yeyote ya hitilafu ya umeme na ndani ya nyumba hiyo mlikuwa hamna mtu mwengine.
‘Wakati nipo kituoni nikisubiri dalala akapita jirani yangu na vespa akaniambia wewe vipi mbona uko huku kwako kunaungua moto ndio nikashtuka na kurudi nyumbani na kufika tu nilipiga mayowe kuwaita majirani kuja kunisaidia, kwani ilikuwa asubuhi mapema majira ya saa 12:45 watu bado hawajatoka nje “alisema Abdulhabib.
Akizungumzia thamani ya vitu vilivyoteketea alisema hawezi kujuwa thamani yake kwa haraka kwa vile kulikuwa na vitu vingi vya thamani ikiwemo vitanda viwili vya futi sita kwa sita, viti, meza ya kulia ,sofaseti, mashine ya kufulia, kabati milango miwili na vitu vingine ambavyo hakuweza kuvikariri kwa haraka .
Nae Sheha wa Shehia ya Chukwani Sleiman Mohamed Mwinyi amewataka wananchi wake ikitokea tatizo lolote hasa la moto wapige namba 114 ya Kikosi cha Uokozi na Zimamoto ili kupatiwa msaada wa haraka .
Hata hivyo Sheha huyo alimpongeza mfanyakazi wa shirika la umeme kwa kitendo cha ushujaa alichokifanya kutoa msaada wa haraka kukata nyaya za umeme ili kunusuru athari ya moto kusambaa Zaidi.
No comments:
Post a Comment