Habari za Punde

Ujio wa Timu ya Madaktari Bingwa kutoka China ni Faraja na Fursa Adhimu ya Kuimarisha Sekta ya Afya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Madaktari wa Kichina waliofika  Ikulu Jijini Zanzibar  kujitambulisha leo, wakifuatana na Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi Zanzibar Mhe.Zhang Zhisheng (wa pili kulia)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ujio wa timu ya madaktari bingwa kutoka China ni faraja na fursa adhimu ya kuimarisha sekta ya Afya Zanzibar.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na timu ya madaktari hao walioongozwa na Balozi Mdogo wa China anayepo Zanzibar, Zhang Zhisheng chini ya kiongozi wa madaktari hao Dk. Zhao walipofika kujitambulisha.

Alisema ushirikiano uliopo baina ya China na Zanzibar ni wa kihistoria na wa muda mrefu, na aliishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kuiungamkono Zanzibar hususan kwenye sekta ya afya, kwa msaada wa vifaa vya kisasa na teknolojia mpya ya kufanya operesheni bila upasuaji pamoja na huduma nyingine za uchunguzi na kitabibu.

Rais, Dk. Mwinyi aliwapongeza madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya Zanzibar ya kuwahudumia wananchi kwa kuwatibu kwa kutumia utaalamu wa kisasa. Alisema Madaktari hao mbali ya kutoa mbinu za kibingwa pia wanasaidia maeneo mbalimbali ya afya ikiwemo kutoa vifaa vya kisasa kwenye hospitali hizo, utaalamu kwa madaktari wazawa na kuweka miundombinu sawa ya hospitali.

Dk. Mwinyi aliiomba serikali ya China kuisaidia Zanzibar madaktari bingwa kwani serikali imejiimarisha zaidi kwenye sekta ya Afya kwa kuongeza hospitali za wilaya Unguja na Pemba hivyo, aliwaomba madaktari hao  kuongeza nguvu na utaamu kwenye hospitali hizo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi mdogo wa China, Zhang Zhisheng alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuiongoza Zanzibar kuwaletea maendeleo wananchi wake na kueleza wanashuhudia mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Naye Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, aliishukuru timu ya madaktari hao kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kukubali kujitoa kuongeza nguvu kuimarisha sekta ya afya nchini.

Naye, Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya Dk. Msafiri Marijani alieleza madaktari hao ni wataalamu wa masuala ya ENT, operesheni kwa kinamama bila kupasua, macho, meno, uzazi na magojwa megine ya kinamama, wataalamu wa mionzi pamoja na wa uchunguzi wa magonjwa ya kansa pamoja na wakalimali ambao watakuwepo Zanzibar kwa mwaka mmoja wakishirikiana nao kwenye hopaitali za Mnazi Mmoja na Abdalla Mzee, Pemba pamoja na kuongeza nguvu na utaalamu kwa hospitali za Kivunge na Chakechake Pemba.

Dk. Marijani alieleza mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na ujio wa madaktari wao mbali na matibabu kwa wananchi lakini kuanzishwa kitengo cha madaktari bingwa watakaofanya oparesheni bila ya kumpasua mgonjwa katika hospitali za Mnazi Mmoja na Abdalla Mzee.

Alisema kwa mara ya kwanza Mnazimmoja wametumia upasuaji bila kupasua ambao ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Sambamba na kusifu vifaa vipya vya kitaalaamu kutoka kwa timu hiyo aliyoieleza kwamba imeongeza uweledi na ufanisi wa hali ya juu.

 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, kiongozi wa timu ya madaktari hao, Dk. Zhao waliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na uongozi wa Wizara ya Afya kwa ushirikiano waliowaonesha tokea wamefika Zanzibar mwenzi Septemba mwaka jana pamoja na kusifia ukarimu wa watu wa Zanzibar waliobahatika kukutaana nakueleza hakika ni watu wakarimu na wenye kuenzi utamaduni, umoja na upendo kwa wageni.

Dk. Zhao ambae pia ni mtaalamu wa upasuaji wa magonjwa yote, alieleza kipindi kifupi walichofika Zanzibar kwa ushirikiano wa madaktari wenyeji wa Mnazi Mmoja na Abdalla Mzee wamefanikiwa kutibu wagonjwa wengi wa maradhi mbalimbali na kufanikiwa kutibu kesi nyingi zilizokua zikiwasumbua wananchi wa Zanzibar waliofika vituo humo kwaajili ya matibabu.

Alieleza anatumai uwepo wao utapunguza kesi nyingi ninazowasumbua wananchi na kuwataka kuitumia fursa  ya uwepo kwa kufika kwa wingi kwenye hospitali za umma ili wapate matibabu na ushauri wa kitaalam

Timu ya madaktari bingwa 32 kati yao 12 watashirikiana na madaktari wazawa kwenye Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na madaktari tisa watakwenda kuongeza nguvu kwenye hospitali ya Abdalla Mzee, Pemba kwa kufanya kazi begakwa bega baina yao.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.