Habari za Punde

Mawaziri wa Tanzania na Afrika Kusini Washiriki Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax kwa pamoja na Mwenyekiti mwenza Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor wamefungua Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Bi-National Cooperation) kati ya Tanzania na Afrika Kusini – ngazi ya Mawaziri uliofanyika tarehe 15 Machi 2023 jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Picha ya Pamoja Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor na Waheshimiwa Mawaziri kutoka Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Bi-National Cooperation) kati ya Tanzania na Afrika Kusini uliofanyika tarehe 15 Machi 2023 jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Mawaziri wa kisekta wa Serikali za Tanzania na Afrika Kusini wamekutana jijini Pretoria, Afrika kusini kushiriki Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Bi-National Cooperation - BNC) ngazi ya Mawaziri kati ya nchi hizo uliofanyika tarehe 15 Machi 2023.

Mkutano huu wa siku moja ulitanguliwa na mkutano ngazi ya wataalamu uliofanyika tarehe 13 na 14 Machi 2023 ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa na jukumu la kuandaa taarifa kwa ajili ya mkutano wa ngazi ya Mawaziri.

Mkutano wa Mawaziri umepitia na utawasilisha taarifa katika itakayojadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika mkutano wa Wakuu wa Nchi hizo unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 Machi 2023.

Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ngazi ya Mawaziri ulifunguliwa kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Mwenyekiti mwenza Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor ambao wameongoza ujumbe wa nchi hizo mbili katika mkutano huo.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Dkt. Tax ameeleza kuwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaonesha nia ya dhati ya mataifa hayo ya kuendeleza ushirikiano wa kihistoria na kidiplomasia uliopo.

“Mkutano huu unatoa fursa ya kujadili na kuamua masuala ya msingi ya kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya nchi na watu kupitia muingiliano uliopo katika shughuli mbalimbali za kijamii, biashara na uwekezaji” alisema Dkt. Tax

Pia akaeleza mkutano huo wa BNC utaweka msisitizo katika masuala ya ustawi wa jamii wa mataifa hayo mawili pamoja na watu wake.

Mkutano huo utajadili masuala ya ushirikiano yenye tija kwa nchi hizo na kupelekea maamuzi yatakayoleta matokeo chanya na kutoa ufumbuzi wa changamoto za wananchi.

Dkt. Tax amesema sekta binafsi ni chachu katika kuendesha uchumi wa nchi, pia ni wadau muhimu kwa sekta za umma hivyo ni jukumu la Serikali kuwezesha upatikanaji wa mazingira mazuri ya biashara ili ziweze kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wa Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Nalendi Pandor ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Afrika kusini umejengwa na historia yenye uhalisia iliyoasisiwa tangu enzi za harakati za kupinga ubaguzi wa rangi pamoja na za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Ameongeza kuwa Afrika Kusini itaendelea kushirikiana na Tanzania hususan katika shughuli za kijamii, kiuchumi na masuala ya kiutamaduni.

“Napongeza jitihada za mshikamano zilizooneshwa na wafanyabiashara wa Afrika Kusini na Ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania kwa kusaidia madawati 400 katika shule za Wilayani Kongwa na vifaa wezeshi vya usafi katika shule ya miyembeni mwaka 2018” alisema Dkt. Pandor.

Aidha, akaeleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zina matamanio makubwa ya kukuza uchumi utakaotengeneza ajira na kuondoa umasikini na kujenga usawa wa hali ya kimaisha kwa wananchi wake.

Vilevile, Tanzania na Afrika Kusini zina mtazamo unaofanana katika masuala ya usalama, uchumi na misimamo ya kimaendeleo ya kikanda na kimataifa hivyo, BNC ni sehemu ya jitihada zitakazowezesha kuongezeka kwa miradi ya maendeleo na mshikamano imara utakaopelekea kukuza na kuimarisha ushirikiano uliopo.

Mkutano wa BNC unajadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika sekta mbalimbali za ushirikiano zilizokubaliwa na nchi hizo. Sekta hizo ni pamoja na; Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha na Uchumi, Nishati, Mifugo na Uvuvi, Madini, Habari, Mawasiliano na teknolojia ya mawasiliano, Kilimo, Uchukuzi, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Maji na Misitu, na Afya.

Kwa pamoja viongozi hao walizitaka sekta zilizopo katika maeneo hayo ya ushirikiano kuhakikisha wanatekeleza na kutatua kwa wakati masuala ya kiutendaji ili kuruhusu sekta hizo kustawi kiuchumi na kuyafikiwa kwa wakati malengo ya Wakuu wa Nchi katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini.

Mkutano huu unaenda sambamba na kongamano la biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini litakaalofanyika tarehe 16 Machi 2023 na kuhusisha  maonesho ya huduma na biashara kutoka sekta za umma na sekta binafsi ambapo washiriki wapatao 136 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano na maonesho hayo jijini Pretoria, Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.