Habari za Punde

Mhe Hemed akutana na UVCCMMakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameupongeza Uongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa mipango yake madhabuti ya kuandaa vijana wenye nidhamu, na utii katika ngazi mbali mbali za Uongozi.

Mhe. Hemed ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ameeleza hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Jumuiya hiyo Ofisini kwake Vuga wakiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndg. Muhamed Ali Muhamed (Kawaida).

 

Amesema ni jambo lililowazi kuwa Jumuiya hiyo ina jukumu kubwa la kuandaa na kulea Vijana kuwa Viongozi Imara na wenye Maadili ambapo tokea kuasisiwa kwake mwaka 1978 tayari Viongozi wengi Nchini wamepitia katika Jumuiya hiyo.

 

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa amewahakikishia kuwapa mashirikiano ya kila namna kwa kuiunga Mkono Jumuiya hiyo ili iweze kufanikisha Shughuli zake za kila siku.

 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa UVCCM kwa kuandaa mpango mkakati ambao umelenga kuiletea mabadiliko Jumuiya hiyo kwa kufanya mapitio ya miradi na kutayarisha mpango mkakati ambao utakuwa na tija zaidi kwa jumuiya hiyo

Amesema kuboreshwa kwa vitega uchumi hivyo kutarahisisha  uendeshaji wa shughuli za Chama na Jumuiya zake pamoja na kupatikana ajira zitakazowanufaisha vijana nchini.

 

Mhe. Hemed ameutaka Uongozi huo kuendelea kuwaelimisha Vijana dhamira ya uwepo wa Jumuiya hiyo ikiwemo kutekeleza na kutimiza shabaha na madhumuni ya Chama Cha Mapinduzi, kuhakikisha kuwa vijana wanaandaliwa katika misingi ya kuthamini umoja wa Taifa, kuwaanda vijana kuwa wanachama safi na Viongozi bora wa CCM na Serikali na kuwa raia wema wa taifa pamoja na kuendelea kuhamasisha Amani na Utulivu iliyopo Nchini.

 

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka kueleza mazuri yanayofanywa na Serikali katika ujenzi wa Miradi ya maendeleo ili Wananchi wafahamu dhamira Njema ya Serikali zao.

 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amempongeza Mwnyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu Mwenyekiti CCM Bara Ndg. Abdulrahman Kinana kwa kuendelea kutoa maelekezo kwa lengo la kukijenga na kukiendeleza  Chama Cha Mapinduzi.

 

Akizimgumza kwa niaba ya Viongozi hao Mwenyekiti wa umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Ndg. Mohamed Ali Mohamed (Kawaida) amemueleza Mhe. Hemed kuwa UVCCM inaimani na kasi ya Serikali zote mbili zinazoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kuwaletea maendeleo watanzania na kuahidi kuendelea kuunga Mkono juhudi hizo kwa maslahi ya Taifa.

 

Aidha Ndg. Kawaida amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kufanyika  Mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa demokrasia nchini  na kueleza kuwa fursa hiyo itumike kuhamasisha umoja na mshikamano na kuepuka kuwagawa watanzania.

 

Katika kikao hicho Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekabidhi Kompyuta kwa Wilaya zote kumi na mbili za Zanzibar Kichama ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa kwa Jumuiya hiyo kwa lengo la kuimarisha utendaji.

 

…………………………

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

01/03/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.