Habari za Punde

Serikali Inafanya Jitihada Kuhakikisha Inawainua Wanawake na Wajasiriamali Katika Nyanja Mbalimbali

Na Maulid Yussuf WMJJWW  Zanzibar 

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bi.Siti Abbas Ali amesmea Serikali inafanya jitihada kuhakikisha inawainua wanawake na wajasiriamali katika nyanja mbalimbali.

Murugenzi Siti ameyasema hayo wakati alipofungua mafunzo ya wajasiriamali wadogo wadogo katika ukumbi wa Studio za kurikodia Rahaleo Mjini Unguja ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani. 

Amesema katika jitihada hizo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi ameweka fedha maalum kwa ajili ya kuwapatia mikopo nafuu wajasiriamali wadogo wadogo ili kuwainua kiuchumi na  kuendeleza biashara zao.

Hivyo amewaomba wajasiriamali kuitumia vyema fursa hiyo ya kujipatia mikopo kwa kujikusanya kwa pamoja na kufuata masharti yaliopo ili kuijua mitaji yao na kendeleza biashara zao.

Amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto itaendelea kuwasimamia wajasiriamali hasa wanawake ili kuhakisha mikopo hiyo wanaipata kwa wakati na kuinua mitaji katika biashara zao.

Aidha amesema kuwa asilimia kubwa ya wajasiriamali waliopo nchi ni wanawake ukilinganisha na wanaume, hivyo ni vyema kuwa mstari  mbele katika ktengeneza bidhaa zenye ubora na kutangaza bidhaa zao kwa lengo la kupata masoko.

Amesema katika ujumbe wa mwaka huu wa siku ya wanawake duniani unahamasisha  matumizi ya teknolojia katika kujikwamua kiuchumi kwa wanwake, hivyo ni  vyema kutumia simu zao vizuri kutangaza bidhaa zao .

Nae Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Usawa wa Kijinsia na kuwainua wanawake UN WOMEN,  bibi Lucy Tesha, amewapongeza wajasiriamali kwa kuonesha ushiriki wao katika mafunzo hayo.
 
Amesema Shirika lao limekuwa likisaidia masuala mbalimbali katika kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia na kuwainua wanawake kiuchumi kwa lengo la kuondoa mtazamo chanya wa kuwa mwanamke hawezi kitu.

Pia amezipongeza Serikali zote mbili kwa  kuwatambua kina mama na wanawake na hivyo imeoona haja ya kuunda Wizara maalum inayoshughulikia masuala yao.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Jinsia katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Bi halima Abdulrahman amesema  Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo wadogo, kuwasaidia wanawake katika kujitambua na kujua namna ya kufanya biashara zao 

Amesema kuna pengo kubwa  baina ya wanawake katika matumizi ya teknolojia, hivyo ujumbe wa mwaka huu upo katika kuamasisha wanawake kutumia teknolojia katika kutafuta masoko. 

Nao wajasiriamali wanawake wamewashauri wanawake wenzao kuacha ubaguzi kwa kuwatumikisha watoto wao wanawake na kuwaacha watoto wanaume kwani yanaweza kuwaathiri kisaikolojia.

Wamesema wamekuwa wakipata changamoto kubwa wanapohitaji mikopo kutokana na vikwazo vikubwa vilivyopo vinavyowafanya kukosa mikopo, hivyo wamemuonba mhe Rais kufuatilia kwa makini suala hilo kwani malengo yaliyowekwa kwa wajasiriamali hayo hayafikiwi.

Raya Idrisa Ahmada mhadhiri msaidizi wa Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA
akitoa maada ya teknolojia amesema hivi sasa matumizi ya teknolojia hayaepukiki, hivyo ni vyema wajasiriamali wadogo wadogo kuamka kutumia teknolojia kwa kutangaza bidhaa zao ili kutafuta masoko na kuinua mitaji yao.

Amewataka kuhakikisha wanatangaza bidhaa zao katika nyanja mbalimbali na sio kusubiri makongamano au maonesho kwanj hayataweza kuinua kipato chao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.