Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imekuja na Mkakati Maalumu wa Kuwahusisha Viongozi wa Dini na Taasisi za Kidini katika Kupambana na Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu ambayo imeacha majeraha na vilio kwa kundi kubwa la wahanga wa biashara hiyo.
Adhma hiyo imebainishwa leo jijini Dodoma wakati wa Semina ya Elimu kuhusu biashara hiyo haramu na Afisa Mwandamizi, Ahmad Mwendadi kutoka Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu iliyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi huku zoezi hilo likianza katika mkoa wa Dodoma na likitegemewa kufika hadi Visiwani Zanzibar.
“Sasa hivi tumeanza na viongozi wa dini ili waweze na wenyewe kutusaidia katika kuelimisha wananchi kwasababu viongozi wa dini wana uwezo kwanza ni watu wanaokubalika katika jamii ambazo wanaishi na ambazo wanafanyia kazi lakini vilevile tunaamini kwa kuwatumia wao elimu itawafikia walio wengi hapa nchini,tumeanza na mkoa wa Dodoma lakini tunatarajia kuifikia mikoa mingine hapa nchini ikiwemo kule Visiwani Zanzibar kwani kupambana na uhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu ni suala la muungano…” alisema Mwendadi
“… kwa maana hiyo sekretarieti kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tukiongozwa na Waziri wetu ambae ndiye msimamizi wa sheria ya usafirishaji haramu wa binadamu Mheshimiwa Masauni tunataka kuhakikisha kwamba angalau sehemu kubwa ya nchi kila kaya inafikiwa na elimu ya usafirishaji haramu wa binadamu ili kupunguza tatizo hili hapa nchini”, aliongeza Mwendadi
Wakizungumza katika semina hiyo washiriki mbalimbali waliipongeza serikali kuwajumuisha viongozi na taasisi za kidini huku wakitoa maoni yao juu ya kadhia hiyo ambayo ni sawa na makosa mengine ya jinai ambayo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Hawa watu ambao wanafanya kazi kwa ajili ya usafirishaji haramu wa watu ulimwenguni wana mtandao wa hali ya juu ulimwengu mzima na sisi vilevile, viongozi wa dini tukiungana vilevile tukishirikiana na serikali na wadau wengine wasiopenda uonevu wa watu wengine ni vizuri tukiunga mitandao ya hali ya juu ili kuweza kuwa na sisi tunapiga hatua katika mtandao wetu kukomesha biashara hiyo” alisema Padri Josephat Kabutta wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment