RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameziomba Kampuni za
Bakhresa kupitia sekta ya usafirishaji kuboresha usafiri wa baharini kwa
kuanzisha safari maalumu za Pemba – Unguja - Tanga kwa safari za haraka na kila
siku.
Alisema Wananchi wa Pemba wamekua na shida ya muda
mrefu ya usafiri wa baharini, aliomba wawekewe usafiri wa uhakika ili kuwapunguzia
usumbufu huo.
Dk. Mwinyi alitoa ombi hilo alipozindua boti mpya ya
kisasa ya Kilimanjaro VIII kwenye viwanja vya Hotel Verde, Mtoni Wilaya ya
Mjini.
Alisema, wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeleza jitihada
za kuitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto ya usafiri salama na wa uhakika kwa
Unguja – Pemba, kipindi hiki kampuni ya Azam iendelee kuwapunguzia usumbufu wa
usafiri wananchi wa visiwa hivyo.
“Ombi langu kwenu ni kwamba, tuna uhaba mkubwa wa
usafiri wa Unguja na Pemba, ninaomba kwa sababu mumeongeza vyombo basi kuwe na
safari maalumu za Unguja na Pemba, wananchi wa Pemba wangependa kutumia muda
mfupi, vyombo wanavyotumia sasa vinachukua muda mrefu sana na pia havipo siku zote,
tunaomba Azam mtusaidie kupunguza hili tatizo wakati Serikali inajipanga
kufanya kwa upande wake”
Alisema, safari za Unguja, Pemba na Tanga ni muhimu
kwa kutoa huduma kwa wanachi.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza Serikali inathamini mchango wa sekta binafsi
katika utekelezaji wa mipango ya serikali ya maendeleo na ukuzaji wa uchumi.
Alitumia fursa hiyo kuzihakikishia kampunzi za Bakheresa kupata
ushirikiano kutoka Serikalini ili miradi waliyowekeza kuona inaleta faida kwao
na nchi kwa ujumla.
Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi aliziagiza,
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA) washirikiane na Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini ya Tanzania Bara (SUMATRA), kuongeza
ufanisi na kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri wa baharini unaendelea
kuwepo.
Pia alisema Serikali kwa awamu zote za uongozi, imejitahidi kuimairisha
miundombinu na mazingira mazuri kwa kutoa huduma bora za usafiri wa baharini pamoja
na wajibu wa kusimamia usalama wa abiria na mizigo kwa vyombo vinavyotumia
usafiri huo.
Dk. Mwinyi, aliwanasihi wananchi kuacha kutumia vyombo vya usafiri wa
baharini visivyozingatia usalama wao na kuacha kutumia bandari bubu kwani
kunahatarisha maisha yao na ni kinyume cha sheria.
Akizingumzia ufinyu wa bandari ya Malindi, Rais Dk. Mwinyi alieleza
Serikali imechukua jitihada kuimarisha eneo kupunguza msongomano wa
abiria kwa kuipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto hiyo kwa kutekeleza mradi wa
Ferry Terminal katika eneo la Maruhubi kwa kujenga kituo kipya cha kisasa kwa
ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza bandari ya Malindi baada ya shughuli za
mizigo kuhamia bandari ya Mangapwani itatengenezwa upya ili iendane na dhamira
ya Serikali ya kuufanya Mji Mkongwe na maaneo yake kuwa sehemu maalum ya kuendeleza
Sekta ya Utalii.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na
Uwekezaji, Mudrik Soraga alisema Serikali imejipatia mafanikio makubwa kwenye
sekta ya uwekezaji na kufanikiwa kuleta wawekezaji wenye mitaji mikubwa ya
zaidi ya dola za Marekani 373.5 na tayari imesajiliwa.
Naye, Mkurugenzi wa Azam Marine, Abubakar Azizi amesema kampuni zao
zimewekeza mtaji mkubwa wa zaidi ya dola za Marekano milioni 120 ili
kuwafikishia huduma bora Watanzania pamoja na wageni wanaotembelea nchini
kupitia sekta zake za biashara.
Alisema boti ya Kilimanjaro VIII “The Falcon of sea” inauwezo wakuchukua
abiria hadi 11, 000 kwa siku, ina madaraja ya VIP, Royal na daraja la kawaida.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment