Habari za Punde

Wizara ya Fedha na Mipango Yaaza Kuwanoa Wajumbe wa Timu Kuu za Maandalizi ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru akifungua warsha elekezi  ya siku 4 kwa wajumbe wa Timu kuu za Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambazo zinajumuisha Timu za Uandishi na Uhariri, yenye lengo la kuwaongeza uwezo ili kupata dira na mpango mzuri wa muda mrefu, warsha hiyo inafanyika katika ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee Tower, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa Timu kuu za Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambazo zinajumuisha Timu za Uandishi na Uhariri wakifuatilia kwa umakini wakati wa warsha maalumu ya kuwajengea uwezo zaidi wajumbe hao ili kufanikisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, warsha hiyo inafanyika katika ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee Tower, jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru (katikati), Kamishna wa Idara ya Mipango ya Taifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Mursali Milanzi (kulia) na Kamishna msaidizi wa Idara ya Mipango ya Taifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Royal J. Lyanga (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Timu kuu za Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambazo zinajumuisha Timu za Uandishi na Uhariri, waliohudhuria warsha elekezi iliyolenga kuwaongeza uwezo ili kupata dira na mpango mzuri wa muda mrefu, warsha hiyo  ya siku 4 inafanyika katika ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee Tower, jijini Dar es Salaam.

Na. Joseph Mahumi, WFM, Dar es Salaam

Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Timu Kuu za Uandishi na Uhariri wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuhakikisha zinakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu machakato wa maandalizi ya Dira hiyo. Warsha hiyo elekezi ya siku 4 inafanyika katika ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee Tower, jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru amesema kuwa warsha hiyo ni msingi madhubuti wa kufanikisha maandalizi ya Dira ya mpya Taifa ya Maendeleo.

 

“Matumaini yangu kwamba kupitia warsha hii mtapata muda mzuri wa kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili kwa kina kuhusu maono ya Taifa letu kwa kizazi cha sasa na kijacho”, alisema Bw. Mafuru.

 

Alisema anaamini kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kakimilifu na kutoa mawazo mazuri kwa kujifunza kupitia Dira za nchi zinazoendelea na zilizoendelea kwa kuwianisha na mazingira ya Tanzania.

 

Bw. Mafuru aliongeza kuwa maandalizi ya Dira 2050 yameanza mapema ikizingatiwa kuwa Dira tunayoendelea kuitekeleza kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 itafika ukomo mwaka 2025.

 

Alisema maandalizi ya Dira yanajumuisha hatua na shughuli nyingi ambazo zinahitaji muda mwingi hivyo zoezi hilo linapaswa kufanywa haraka na kwa kuzingatia muongozo na mpango kazi wa maandalizi ya Dira ili kufikia lengo lililokusudiwa.

 

Bw. Mafuru aliwasihi wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa ubunifu, weledi na kujituma kwa kuzingatia Hadidu za Rejea zilizoandaliwa.

 

“Nasisitiza utendaji kazi wa majukumu yenu ufanyike kwa ushirikiano ili kutengeneza timu bora na ya ushindi, mara zote jumuiya au jamii isiyo na umoja huishia kwenye migogoro na mifarakano”, aliongeza Bw. Mafuru.

 

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Mipango ya Taifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Mursali Milanzi amesema kuwa warsha hiyo elekezi itakayofanyika kwa siku 4, wajumbe watarajie kupata nguvu zaidi ya maarifa kutokana na kuwepo kwa wajumbe wa aina tofauti ikiwemo vijana pamoja na wajumbe walioandaa Dira inayoishia.

 

“Tumeona kwamba kabla ya kwenda kuandaa Dira moja kwa moja tuchukue wajumbe wa maandalizi kupeana muelekeo namna gani ya kutekeleza jukumu hili la kitaifa” aliongeza Dkt. Milanzi

 

Mmoja wa wajumbe wa Timu za Uandishi na Uhariri maandalizi ya Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo, Dkt. Gladness Salema ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, alisema kuwa wanaimani mafunzo hayo yatawapa matazamio mazuri katika kuandaa Dira na pia wana imani Serikali itapata Dira na mpango mzuri wa muda mrefu kwa maendeleo ya nchi.

 

“Warsha hii imetupa nafasi ya kukutana na wajumbe wazoefu ambao walishiriki katika kuandaa Dira iliyopita na tunaamani katika kubadilishana uzoefu kupitia warsha hii basi tutafanikiwa kupata kilicho bora”, aliongeza Dkt. Salema

 

Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea na taratibu mbalimbali za Maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa 2050 itakayoleta maono ya watanzania kwa miaka 25 ijayo kwa kushirikisha wadau wote muhimu.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.