SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza dhamira yake ya kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu kupitia Wizara yake ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alieleza dhamira hiyo
kwenye ufunguzi wa mradi wa kuwajengea uwezo vijana kwa lengo la kuwawezesha
kujiajiri na kuajirika kwenye sekta ya uchumi wa buluu huko ukumbi wa Golden
Tulip, Uwanja wa ndege, Zanzibar.
Dk. Mwinyi alisema, Serikali inaendeleza jitihada mbali mbali kwa kuhakikisha
inatoa elimu bora nchini katika kufikia dhamira hiyo kwa kuchukua hatua za
kuboresha miundombinu ya skuli mpya ikiwemo ujenzi wa Skuli mpya za ghorofa kwa
Unguja na Pemba na mafunzo kwa walimu.
Hatua
nyengine, Rais Dk. Mwinyi alieleza ni kuzipatia huduma muhimu skuli hizo
ikiwemo, upatikanaji wa vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia, matumizi bora
ya TEHAMA na kuwapatia vijana ujuzi na maarifa utakao wawezesha kuyakabili
maisha yao na kunyanyua uchumi wa nchi.
“Kama hatutowaandaa vijana
wetu, wakawa weledi wa kujua wanachokifanya, hatutofikia dhamira yetu ya
kuhakikisha watu wote wakiwemo vijana wanashiriki na kunufaika na Uchumi wa
Buluu” aliasa Rais Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi alitaja sehemu ya
ujenzi wa mradi huo ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha kisasa cha
Ubaharia na majengo utawala, ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa kike kwenye Taasisi
ya Sayansi na Teknolojia Karume yenye ukubwa wa ghorofa tatu na uwezo wa
kuhudumia wanafunzi 500 kwa wakati mmoja, ujenzi wa madarasa ya kusomea na
karakana zinazohusiana na masomo ya mafuta na gesi.
Aliongeza ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya amali na
vifaa vyote vinavyohitajika kwa programu zitakazotolewa na vyuo hivyo ambavyo vinatarajiwa kujengwa kwenye Wilaya za Mkoani (Chambani), Wilaya ya
Micheweni (Tumbe Mashariki), Wilaya ya Kati (Jendele) na Wilaya ya Kaskazini B
(Panga Tupu).
Shughuli nyengine za mradi huo wa SEBEP, Rais Dk. Mwinyi
alizitaja ni pamoja kuwajengea uwezo watendaji wa Taasisi zinzozoshiriki kwenye
mradi huo kwa kuwapatia nafasi
za kuongeza taaluma zao, ujenzi wa kituo cha kuwapa vijana mafunzo ya kuanzisha
na kuendeleza biashara zao (incubation
centre) na vifaa vyake eneo la Kizimbani Unguja, ambacho kitakuwa chini ya
usimamizi wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) na taasisi ya SMIDA imepewa
jukumu la kuwapatia mafunzo mbalimbali vijana hao.
Rais Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo inatoa nafasi kwa
Vijana wa Zanzibar kupata fursa ya mafunzo ya amali na ufundi wa fani mbali mbali zikiwemo zinazohusiana na
Uchumi wa Buluu.
Pia alitoa wito kwa vijana kuitumia vyema fursa ya
mradi huo kujipatia ujuzi ili wanufaike na soko la ajira kwenye sekta ya uchumi
wa buluu kwa kuweza kujiari na kupata sifa za kuajiriwa.
Dk. Mwinyi alisema mradi huo utaongeza upatikanaji wa
wafanyakazi wenye taaluma kwenye shughuli za Utalii ambayo ni Sekta
kiongozi katika uchumi wa Zanzibar
pamoja na kuiwezesha Zanzibar kuzitumia vyema rasilimali zake za asili ikiwemo
bahari, mafuta na gesi asilia katika kukuza pato la taifa na upatikanaji wa
ajira kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu.
Mradi wa kuwajengea
uwezo vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri na kuajirika kwenye sekta ya
uchumi wa buluu SEBEP
unafadhiliwa kwa asilimia 90 na washirika wa maendeleo (AfDB) na asilimia 10 unafadhiliwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, unatarajiwa kutumia dola za Marekani
milioni 54 sawa na fedha za Tanzania shilingi bilioni 126.379.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU - ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment