RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi, akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Kwahani Zanzibar Mhe.Ahmada Yahya Abdulwakil, baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Mabuluu Mfereji wa Wima Ng’ambo Station Wilaya ya Mjini Unguja leo 4-8-2023
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameendelea
kuihimiza jamii juu ya umuhimu wa kudumisha amani na kubeba imani ya dhati ndani ya mioyo yao kwa
mustakbali wa taifa na ustawi wa jamii bora kwa maendeleo ya uchumi endelevu
nchini.
Al hajj Dk. Mwinyi, alitoa nasaha hizo kwenye
Msikiti
Mabuluu
Mfereji wa Wima, Mkoa wa Mjini Magharibi, alikojumuika pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu
kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.
Rais, Al hajj Mwinyi,
aliieleza Imani na amani ni vitu viwili vinavyokwenda sambamba na kutegemeana
wakati wote, hivyo aliisihi jamii kadri wanapokusanyika
pamoja kwenye maisha yao ya kila siku, wasichoke kuamini na kuendelea kuhimiza amani
ya nchi na kuidumisha muda wote katika kuyaendea mazuri yote kwa ustawi wa
jamii njema na taifa kwa ujumla.
“Imani na amani vinakwenda sambamba, amani ndio dini yetu, Uislamu unatutaka
tueneze amani wakati wote, amani ikikosekana mambo mengine yote hayawezekani na
hili tunalijua kutokana na wenzetu wanayoyapitia huko kwenye mataifa ya
wenzetu, tunaona sehemu zenye vita hata ibada hazifanyiki, ili ipatikane amani
lazima tuwe na Imani ndani ya nyoyo zetu” alisisitiza Al hajj Mwinyi.
Al hajj Dk Mwinyi
alieleza, kila mmoja anawajibu wa kuitunza na kueneza amani kwa mustakbali wa taifa
na ustawi wa jamii iliyobora.
Pia, aliwahimiza
waumini hao kuendelea kuliombea taifa na viongozi kwa ujumla ili kuendelea kuwaongoza
vyema na kuyatekeleza yote waliyowaahidi wananchi.
Rais Al Hajj
Mwinyi alieleza, viongozi wanamajukumu makubwa na kubeba dhima kubwa hivyo, aliwasihi
wanaumini hao na jamii kwa ujumla wasichoke kuwaombea mazuri na kuzidi
kuwaombea kheir kwa Mwenyezi Mungu (S. W).
Akitoa nasaha za
Ijumaa, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi
ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisifu juhudi za Rais
Al Hajj Dk. Mwinyi kwa Imani aliyoijenga kwa waumini wa dini ya kiislamu na
taifa kwa ujumla ikiwemo kujumuika nao pamoja kwenye ibada katika misikiti
mbalimbali nchini sambamba na kuwaboresha ustawi wa maendeleo na uchumi
wananchi wote.
Alisema juhudi
zote hizo ni Imani yake kwa Wazanzibari na taifa lote, hasa jitihada za
kuendelea kuimarisha huduma za jamii, uchumi na maendeleo ikiwemo ujenzi wa
miundombinu imara na kuboresha mawasiliano.
Naye, Khatibu wa
sala ya Ijumaa msikitini hapo, Sheikh Abdul Karim Said Abdulla aliihusia jamii
kuendelea kupendana na kutendeana mema kwa kujizuia kuudhiana na kutendea mabaya.
Aliwashajihisha waumini
hao kuendeleza mshikamo kwa kudumisha amani, umoja na upendo baina yao kwa
ustawi wa jamii iliyo njema.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment