SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuwapatia wakulima pembejeo na huduma nyengine za kilimo, ili kuwaondoshea changamoto
kuelekea mapinduzi ya kijani kwa uchumi endelevu.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Nane Nane kwa mwaka
2023, yanayoendelea Kizimbani, Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema, Serikali inawajibu wa kuwawezesha vijana
na wanawake kwenye shughuli zao za kilimo na kuitaka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuandaa utaratibu
mzuri wa kuweka takwimu zao kwa lengo la kuhakikisha inapotoa pembejeo ziwafikie
wahusika kwa urahisi na kwa wakati muafaka.
Aidha, Rais
Dk. Mwinyi ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuzitengeneza
barabara zote zilizomo kwenye viwanja vya Maonesho ya Nane Nane Kizimbani, kwa
kiwango cha lami ili kuyaongezea hadhi Maonesho ya mwakani.
Alisema,
Serikali inawajibu wa kuhakikisha ardhi ndogo ya kilimo
ilioyopo inatumika kwa ufanisi ili izalishe na kuongeza tija.
“Umefika wakati tuwe na takwimu sahihi ya ukubwa wa ardhi ya kilimo
tuliyonayo ili tuweze kuweka mipango mizuri ya kuitumia” Alilisistiza Dk.
Mwinyi.
Akizungumzia
hali halisi ya uzalishaji kilimo nchini, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali
imeweka jitihada mbalimbali kufanikisha sekta hiyo na kueleza kuwa na matokeo
yenye tija. Alieleza ongezeko la uzalishaji wa mboga
mboga na matunda nchini kutoka tani 64,820 mwaka 2021 hadi tani 66,304 mwaka
2022, muhogo umeongezeka kutoka tani 181,668 mwaka 2021 hadi tani 202,519 mwaka
2022.
Kwa upande wa mifugo Rais Dk. Mwinyi alisema, ongezeko la ng’ombe
waliochinjwa kutoka 25,916 mwaka 2021 hadi 27,326 mwaka 2022, kuku waliochinjwa
wameongezeka kutoka 751,073 mwaka 2021 hadi 1,130,591 mwaka 2022 na mayai
yaliyozalishwa yameongezeka kutoka 15,723,843 mwaka 2021 hadi 21,659,078 mwaka
2022.
Alisema, hizo ni dalili nzuri za mafanikio katika sekta ya Kilimo na
Ufugaji kwa Zanzibar.
Alieleza lengo la Serikali kufanya Maonesho ya Kilimo ni kuhimiza kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuelimisha jamii juu
ya umuhimu wa mbinu bora za kilimo ikiwemo matumizi ya teknolojia ya
umwagiliaji maji na zana za kisasa kwa madhumuni ya kuongeza uzalishaji kwa
mazao ya chakula na biashara ili kupata tija zaidi na kuwapa faida kubwa
wakulima na Taifa kwa jumla na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo ili
kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi
aliwasihi vijana kutumia fursa ya Maonesho hayo kujifunza zaidi ili wahamasike
na kujiajiri kwenye sekta ya kilimo kwa lengo la kuwa na uhakika wa chakula katika
kupiga hatua za maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwenye maonesho
hayo, Waziri
wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis alisema,
wizara inajitahidi kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali katika
kuimarisha sekta ya kilimo nchini kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 145 ya
Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025.
Mapema
akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili
na Mifugo, Seif Shaaban Mwinyi aliwashauri vijana na wanawake kuzitumia fursa
zinazopatikana kwenye Mradi wa mashamba makubwa ya pamoja (BBT) ulioanzishwa na
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ili
kujiendeleza kiuchumi na kuyafikia mapinduzi ya kilimo.
Uzinduzi wa Maonesho
ya Nane Nane kwa mwaka 2023 ulikwenda sambamba uzinduzi wa Mkakati wa
kilimo chini ya kaulimbiu isemayo
“Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo
endelevu ya chakula”
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU-ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment