Habari za Punde

TADB yawafikia Wakulima Zanzibar

Mkurugenzi Idara ya Kilimo na uhakika wa Chakula   Hamad Masoud Ali akizungumza na wavuvi,wafugaji na wakulima (hawamo pichani) wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya  fursa zinazopatikana katika benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania wakati wa maonyesho ya kilimo yanayoendelea huko Dole Wilaya ya Magharibi A.
Afisa Maendeleo ya Biashara Mkuu Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania  TIDB kanda ya Zanzibar Ashura Akim  akizungumza na wavuvi,wafugaji na wakulima (hawamo pichani) kuhusiana na fursa zinazopatika katika benki hiyo wakati wa maonesho ya kilimo yanayoendelea huko Dole Wilaya ya Magharibi A.
Mkulima wa Mbogamboga Kijiji cha Mpapa Skudhani Khamis Makame akichangia mada wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wavuvi,wafugaji na wakulima yaliyoandaliwa na Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania  TIDB na kufanyika Viwanja vya maonesho ya kilimo yanayoendelea huko Dole Wilaya ya Magharibi A.
Wananchi mbali mbali wakitembelea mabanda ya maonesho ya kilimo yanayoendelea huko Dole Wilaya ya Magaharibi A.
Bwana Shamba kutoka Wizara ya Kilimo Makame akitoa elimu ya mbogamboga kwa wananchi waliojitokeza kutembelea mabanda ya maonesho ya kilimo yanaendelea huko Dole Wilaya ya Magharibi A .

Na Fauzia Mussa    Agosti 07,2023

Wakulima wameshauriwa kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza  ikiwemo kupata mikopo na elimu   ili kuboresha kilimo chao.

Akizungumza wakati akifungua semina fupi ya wakulima,wafugaji  na wavuvi katika  Viwanja vya maonesho ya Wakulima Dole Mkurugenzi Idara ya Kilimo na uhakika wa Chakula   Hamad Masoud Ali amesema wakulima hao wamekua wakishindwa  kufikia malengo kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kukiboresha kilimo.

Aidha amesema kuwa wakulima wengi wa Zanzibar wamejikita katika kilimo cha kujikimu (chakula) hivyo uwepo wa Benki ya maendeleo ya  Kilimo Visiwani kutawasaidia wakulima hao kutoka katika kilimo cha zamani na kuweza kulima kisasa.

Alielezea kuwa  Semina hiyo itawasaidia wakulima  kujua fursa mbali mbali zinazopatikana katika benki hiyo ,hivyo amewataka wadau hao wa kilimo kuwa watulivu na wasikivu ili  kupata elimu ya kutosha ili kuleta mabadiliko ya  kilimo Nchini.

Hata hivyo Mkurugenzi Hamad  aliwasisitiza wakulima hao kuchukua mikopo na kuitumia  katika malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kununua mbegu bora,dhana za kulimia  na mbolea za kisasa ili  kupata mazao yenye tija.

"tumieni fursa hii benki imeshakuja kopeni nunueni matrekta muachane na vijembe vidogo,nunueni mbegu bora ,pamoja na mbolea ili kupata mazao mengi na faida zaidi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla"alifahamisha Mkurugenzi

Mapema aliwataka wajumbe wa semina hiyo kuwa mabalozi wazuri kwa wakulima wengine na kuwataka  kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia benki hiyo.

Nae Afisa  Maendeleo ya Biashara Mkuu Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania  TADB kanda ya Zanzibar Ashura Akim amesema Tasisi hiyo imeanzishwa kwa lengo la  kuwapatia  wakulima, wavuvi na wafugaji  mikopo itakayowatoa  katika kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha biashara

vile vile alisema kuwa taasisi hiyo imeanzishwa ili kuwasaidia wakulima kuweza kulifanya   Taifa kuwa na chakula timilifu hivyo aliwataka wakulima hao kujitokeza kwa wingi kuchukua mikopo ya muda mrefu,mfupi na muda wakati.

 "kilimo ndio uti wa Mgongo wa Taifa ,hili ndilo limetusukuma kuleta huduma zetu Visiwani nawashauri mujiunge kwenye vikundi ili  muweze kutambulika na kuipata fursa hii.

akizungumzia suala la riba katika mikopo hiyo Afisa huyo amesema taasisi inatoza asilimia 10 ya riba katika mkopo na  wapo katika harakati za kupata leseni ya islamic bank ili kuweza kuwadhamini wakulima ambao hawahitaji mkopo ulio na riba.

Alifahamisha kuwa katika kuhakikisha  kilimo kinaendelea , na wakulima wanaachana na kilimo cha kutegemea Mvua benki hiyo inatoa mikopo ya vifaa kama trekta,mashine za maji ,maziwa na kusindikia samaki.

akizungumzia baadhi ya masharti ya mkulima kuweza kupata Mkopo huo amesema kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mkulima amelima  alau kwa misimu miwili na kuwa amejisali katika vikundi vinavyotambulika.

aidha alifahamisha kuwa benki hiyo imekuwa ikishirikaina bega kwa bega na serikali kuweza kupata mabwana shamba wa kuwapatia elimu wakulima juu ya mbinu bora za kulima kilimo chenye tija .

Mkuu wa kitengo cha  Wakulima Mstaafu Othman Ali Maulid  amesema wakulima wa Zanzibar wanauhitaji mkubwa wa rasilimali fedha  hivyo uwepo wa benki ya maendeleo ya kilimo visiwani kutawanyanyua wakulima hao na kujikomboa kiuchumi.

Vile vile alisema  kupitia benki hiyo wanatarajia   mageuzi makubwa  kwa wakulima wadogo wadogo kwa  kuweza kulima ,kuvua na kufuga kibiashara na kukifanya kilimo hicho kua na tija na kuchangia usalama wa chakula katika Nchi.

amesema wakulima walio wengi wa Zanzibar ni wakulima wenye hali za chini hivyo kuweka masharti magumu kama kuweka hati za nyumba na mashamba wakati wa kupatiwa mkopo huo  kutakwamisha juhudi zao za kutaka kupiga hatua za kimaendeleo kupitia kilimo.

Nao washiriki wa semina hiyo wameiomba benki ya maendeleo ya kilimo  kuweka masharti nafuu ya mkopo kwani huko nyuma wakulima wengi walishindwa kupata mkopo kutokana na kutokukidhi masharti .

Waliongeza  kuwa  miongoni mwa faida za kuwepo maonesho ni pamoja na wananchi kupata elimu kuhusiana na mambo mbalimbali hivyo waliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata fursa kama  hizo.

Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania TADB ni Taasissi inayomilikiwa na Serikli ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania  iliyoanzishwa mwaka  2015 ikiwa na lengo la kuwapatia mikopo wakulima, wavuvi , wafugaji na watu wote wanaojihusisha na kuyaongeza thamamani mazao yanayotokana na  kilimo,Ufugaji na Uvuvi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.